The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:
2Wewe mwana wa mtu, hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyoiambia nchi ya Isiraeli: Mwisho uko! Huo mwisho unazijia pande zote nne za nchi hii.
3Sasa mwisho unakujia, nikiyatuma makali yangu, yakujie, nikupatilizie njia zako zote na kukulipisha machukizo yako yote.
4Jicho langu halitakuonea uchungu, wala mimi sitakuhurumia, kwani nitakulipisha njia zako, machukizo yako yatokee kwako katikati; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.
5Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kibaya kimoja kitakapopita, mtaona, kibaya kingine kinakuja!
6Mwisho unakuja! Mwisho huo unakuja, ukuamkie! Tazama tu: unakuja!
7Siku yako mbaya inakuja ukaaye katika nchi hii; wakati unakuja, siku iko karibu, nayo ni ya mastuko, siyo ya kupiga vigelegele milimani.[#Yoe. 1:15.]
8Sasa bado kidogo nitakumwagia machafuko yangu yenye moto, niyatimize kwako makali yangu, nikikupatilizia njia zako na kukulipisha machukizo yako yote.
9Jicho langu halitokuonea uchungu, wala mimi sitakuhurumia nikikulipisha njia zako, machukizo yako yatokee kwako katikati; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana apigaye.
10Itazami hiyo siku! Utaiona, inakuja! Siku mbaya imetokea! Fimbo imechanua, majivuno yamechipuka.[#Yes. 10:5.]
11Ukorofi umeinuka kuwa fimbo ya kuwapiga wasiomcha Mungu; hakuna chao kilichosalia, wala cha mali zao, wala cha urembo wao, wala cha utukufu wao, waliokuwa nao.
12Wakati umekuja, siku imetimia, ndipo asifurahi mwenye kununua, wala asisikitike mwenye kuuza, kwani makali yenye moto yanazijia mali zao zote.
13Kwani mwenye kuuza hatakipata tena alichokiuza, ingawa awepo na kukaa mwenye uzima, kwani hayo yaliyofumbuliwa kwa ajili ya mali zao zote hayageuki, kwa ajili ya manza, walizozikora, hakuna atakayejikalisha uzimani kwa nguvu zake.[#3 Mose 27:24.]
14Yapigeni tu mabaragumu na kuyatengeneza yote! Hakuna atakayekwenda vitani. Kwani makali yangu yenye moto yamezijia mali zao zote.
15Panga ziko nje, magonjwa mabaya na njaa zimo nyumbani; alioko shambani atakufa kwa panga, naye aliomo mjini njaa na magonjwa yatamla.
16Nao watakaopona kwa kukimbia watakuwa milimani kama hua walioko mabondeni, hao wote watakuwa wanalia kila mtu kwa manza zake yeye, alizozikora.
17Mikono yote italegea, nayo magoti yote yatayeyuka kuwa kama maji.
18Watajifunga magunia, wakipigwa na bumbuazi sana, nyuso zao zote, zitaiva kwa kuona soni, navyo vichwa vyao vyote vitakuwa vimenyolewa.[#Yes. 15:2; Yer. 48:37.]
19Fedha zao watazitupa barabarani, nazo dhahabu zao zitakuwa kama zenye uchafu, kwani dhahabu zao na fedha zao hazitaweza kuwaponya siku hiyo, Bwana atakapochafuka, wala hazitazishibisha roho zao, wala hazitayajaza matumbo yao, kwani ndizo zilizowaponza, wazikore manza zao.[#Fano. 11:4; Sef. 1:18.]
20Uzuri wa hayo mapambo yao ukawatia majivuno, wakayatumia kuvitengeneza vinyago vyao vichukizavyo kwa kutapisha kwao. Kwa hiyo nimezigeuza kuwa kwao kama zenye uchafu.
21Kisha nitazipa mikononi mwa wageni, wazipokonye, namo mwao wasionicha katika nchi hii, waziteke, kisha wazichafue.
22Nami nitaugeuza uso wangu, usipatazame, wakipachafua palipokuwa urembo wangu; ndipo, wanyang'anyi watakapopaingia, wapachafue.
23Fanyiza minyororo! Kwani nchi hii imejaa mashauri ya damu, nao mji huu umejaa makorofi.
24Nami nitaleta walio wabaya kuliko wamizimu wengine, wazichukue nyumba zao; nayo majivuno yao wenye nguvu nitayakomesha, patakatifu pao pakitiwa uchafu.
25Mwangamizo unakuja; ndipo, watakapotafuta pa kuponea, wasipapate.
26Teso litafuatwa na teso jingine, zile habari mbaya zitafuatwa na habari mbaya nyingine; ndipo, watakapotafuta mfumbuaji, azifumbue, lakini watambikaji watapotelewa na Maonyo, nao wazee hawatajua mizungu.
27Mfalme ataomboleza, naye aliye mkuu kituko kitakuwa vazi lake, nayo mikono ya watu wa nchi hii itastushwa; nitakapowalipisha njia zao na kuwakatia shauri liyapasalo mashauri yao, ndipo watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.