The chat will start when you send the first message.
1Mwezi wa saba ulipofika, wana wa Isiraeli wakikaa mijini mwao, ndipo, watu walipokusanyika Yerusalemu kama mtu mmoja.[#Ezr. 2:64.]
2Akaondokea Yesua, mwana wa Yosadaki, pamoja na ndugu zake waliokuwa watambikaji na Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na ndugu zake, wakaijenga meza ya kumtambikia Mungu wa Isiraeli, wapate kuteketeza juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose aliyekuwa mtu wa Mungu.[#Ezr. 2:2; 1 Mambo 3:17-19; 2 Mose 27:1; 3 Mose 6:9.]
3Wakaiweka hiyo meza ya kutambikia hapo penye misingi yake. Kwa kushikwa na woga wa wenyeji wa hiyo nchi, wakamtolea Bwana hapo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, hizo ng'ombe za tambiko wakazitoa za asubuhi na za jioni.
4Kisha wakala sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa; wakazitoa ng'ombe za tambiko za kila siku kwa hesabu iliyowekwa ya ng'ombe za tambiko zipasazo kila siku moja.[#3 Mose 23:34; 4 Mose 29:12-38.]
5Baadaye makaitoa nayo ng'ombe ya tambiko isiyokoma kutolewa ya kila siku, nazo za miandamo ya mwezi, nazo za sikukuu zote za Bwana zilizowekwa kuwa takatifu, nazo za kila mtu aliyetaka mwenyewe kumtolea Bwana kipaji cha tambiko.
6Siku ya kwanza ya mwezi wa saba ndiyo, waliyoanzia kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, lakini Jumba la Bwana lilikuwa halijawekewa misingi.
7Kisha wakachanga fedha za kuwapa mafundi wa kuchonga mawe na miti, nao Wasidoni na Watiro wakawapa vilaji na vinywaji na mafuta, walete miti ya miangati toka kwao Libanoni wakiipitisha baharini hata Yafo, kwani Kiro, mfalme wa Wapersia, aliwapa ruhusa.
8Katika mwaka wa 2 wa kuja kwao penye Nyumba ya Mungu huko Yerusalemu katika mwezi wa pili ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na Yesua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine walipoanza kazi za kuijenga pamoja na watambikaji na Walawi nao wote waliorudi Yerusalemu wakitoka kwenye kutekwa; wakaweka Walawi waliokuwa wa miaka ishirini na zaidi kuwa wasimamizi wa kuziangalia hizo kazi za Nyumba ya Bwana.
9Yesua na wanawe na ndugu zake na Kadimieli na wanawe waliokuwa wana wa Yuda wakasimama kama mtu mmoja wakiwaangalia watu wa kazi pale penye Nyumba ya Mungu. Vilevile wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao waliokuwa Walawi.[#Neh. 10:9.]
10Waashi walipoanza kuyapigilia mawe ya misingi ya Jumba la Bwana wakaweka hapo watambikaji waliovikwa mavazi yao, wakishika matarumbeta, nao Walawi waliokuwa wana wa Asafu, wakishika matoazi, wamtukuze Bwana na kumwimbia wimbo wa Dawidi, mfalme wa Isiraeli.
11Wakaitikiana na kumtukuza na kumshukuru Bwana kwamba: Bwana ni mwema, upole wake ni wa kale na kale, nao huwakalia Waisiraeli. Nao watu wote pia wakapaza sana sauti za kupiga shangwe, wamtukuze Bwana, kwa kuwa misingi ya Nyumba ya Bwana iliwekwa.[#2 Mambo 5:13; 7:3; Sh. 118:1.]
12Lakini wengi wao watambikaji na Walawi nao waliokuwa vichwa vya milango, ndio wazee walioiona Nyumba ya kwanza wakalia machozi kwa sauti kuu, misingi ya Nyumba hii ilipowekwa machoni pao, lakini wengine wengi wakazipaza sauti zao za kupiga shangwe na kelele za furaha.[#Hag. 2:3.]
13Lakini watu hawakuweza kuzipambanua sauti za shangwe zenye furaha nazo sauti za vilio vya wale watu, kwani watu walizidisha sana kuzipaza sauti zao za shangwe; hizo sauti zikasikilika hata mbali.