Ezera 5

Ezera 5

Nyumba ya Mungu inajengwa tena.

1Ndipo, wafumbuaji Hagai na Zakaria, mwana wa Ido, waliokuwa wafumbuaji, walipowafumbulia Wayuda waliokaa Yuda na Yerusalemu mambo hayo katika Jina la Mungu wa Isiraeli aliyewajia.[#Hag. 1:1; Zak. 1:1.]

2Ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na Yesua, mwana wa Yosadaki, walipoondokea, wakaanza tena kuijenga Nyumba ya Mungu mle Yerusalemu, nao wafumbuaji wa Mungu wakawa nao wakiwashikiza.

3Siku hizo wakawajia Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa, na Setari-Bozinai pamoja na wenzao, wakawauliza: Ni nani aliyewatolea amri ya kuijenga nyumba hii na kuzimaliza kuta hizi?

4Ndipo, tulipowaambia hayo majina ya watu waliolijenga jengo hili.

5Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa limewaelekea wazee wa Wayuda, wao wasiwakataze kujenga, mpaka amri ya Dario ifike, wapate barua kwa ajili ya jambo hili.[#5 Mose 11:12; 1 Fal. 8:29.]

Barua kwa mfalme Dario.

6Mwandiko wa pili wa barua, waliyoituma kwa mfalme Dario akina Tatinai, mtawala nchi zilizoko upande wa huku wa jito kubwa, na Setari-Bozinai na wenzake Waafarsaki waliokaa upande wa huku wa jito kubwa.

7Katika barua hiyo, waliyoituma kwake, yalikuwa yameandikwa haya: Salamu zote kwa mfalme Dario!

8Na ijulikane kwa mfalme, ya kuwa tumekwenda katika nchi ya Yuda mle mjini, Nyumba ya Mungu mkuu ilimo, nayo inajengwa kwa mawe makubwa ya kuchonga, nazo kuta zake zinapigiliwa mbao. Kazi hizi zinafanywa kwa bidii, zinaendelea vizuri kwa nguvu za mikono yao.

9Ndipo, tulipowauliza wazee wale na kuwaambia haya: Ni nani aliyewaagiza kuijenga nyumba hii na kuzimaliza hizi kuta?

10Tukawauliza nayo majina yao, tukujulishe; yakaandikwa majina yao walio vichwa vyao.

11Nazo hizi ndizo habari, walizotupasha kwamba: Sisi tu watumwa wake Mungu wa mbingu na nchi; nasi tunaijenga Nyumba hii iliyojengwa kale, sasa yapata miaka mingi, naye aliyeijenga na kuimaliza alikuwa mfalme mkuu wa Waisiraeli.

12Lakini kwa kuwa baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, akawatia mikononi mwa Mkasidi Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akaibomoa Nyumba hii, nao walio ukoo wake akawateka na kuwahamisha kwenda Babeli.[#2 Fal. 25:9.]

13Lakini katika mwaka wa Kwanza wa Kiro, mfalme wa Babeli, mfalme Kiro akatoa amri ya kuijenga tena Nyumba hii ya Mungu.[#Ezr. 1:1.]

14Navyo vyombo vya Nyumba ya Mungu vya dhahabu na vya fedha, Nebukadinesari alivyovitoa Yerusalemu humu Jumbani na kuvipeleka jumbani mle Babeli, mfalme Kiro akavitoa jumbani mle Babeli, akampa mtu aitwaye Sesebasari, aliyemweka kuwa matawala nchi;[#Ezr. 1:8.]

15akamwambia: Hivi vyombo vichukue kwenda navyo, kaviweke Jumbani mle Yerusalemu, nayo Nyumba ya Mungu na ijengwe hapo, ilipokuwa.

16Ndipo, yule Sesebasari alipokuja, akaiweka misingi ya Nyumba ya Mungu humu Yerusalemu; toka hapo hata leo inajengwa, lakini haijaisha bado.

17Sasa vikiwa vyema kwake mfalme, na wachunguze nyumbani mwa vilimbiko vya mfalme huko Babeli, kama ni kweli, ya kuwa mfalme Kiro aliagiza kuijenga Nyumba hii ya Mungu humu Yerusalemu. Kisha mfalme na atume kwetu jibu la kutuambia ayatakayo, yafanyike katika jambo hili.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania