Ezera 8

Ezera 8

Wasafiri wenzake Ezera.

1Hawa ndio wakuu wa milango ya baba zao na hesabu ya vizazi vyao waliopanda na mimi kutoka Babeli katika siku za ufalme wa mfalme Artasasta.[#Ezr. 7:1,7.]

2Kwa wana wa Pinehasi: Gersomu; kwa wana wa Itamari: Danieli; kwa wana wa Dawidi: Hatusi

3wa wana wa Sekania; kwa wana wa parosi: Zakaria, tena pamoja naye wakaandikwa wa huo udugu waume 150;[#1 Mambo 3:22.]

4kwa wana wa Pahati-Moabu: Elihoenai, mwana wa Zeraya, tena pamoja naye waume 200;[#Ezr. 2:6.]

5kwa wana wa Sekania: mwana wa Yahazieli, tena pamoja naye waume 300;[#Ezr. 2:8.]

6kwa wana wa Adini: Ebedi, mwana wa Yonatani, tena pamoja naye waume 50;

7kwa wana wa Elamu: Yesaya, mwana wa Atalia, tena pamoja naye waume 70;

8kwa wana wa Sefatia: Zebadia, mwana wa Mikaeli, tena pamoja naye waume 80;

9kwa wana wa Yoabu: Obadia, mwana wa Yehieli, tena pamoja naye waume 218;

10kwa wana wa Selomiti: mwana wa Yosifia, tena pamoja naye waume 160;[#Ezr. 2:10.]

11kwa wana wa Bebai: Zakaria, mwana wa Bebai, tena pamoja naye waume 28;

12kwa wana wa Azgadi: Yohana, mwana wa Katani, tena pamoja naye waume 110;

13kwa wana wa Adonikamu wako waliochelewa, majina yao ni haya: Elifeleti, Yieli na Semaya, tena pamoja nao waume 60;

14kwa wana wa Bigwai: Utai na Zabudi, tena pamoja nao waume 70.

15Nikawakusanya penye mto uendao Ahawa, tukakaa huko kambini siku tatu; nilipowakagua hawa watu na watambikaji, sikuona huko wana wa Lawi.

16Ndipo, nilipotuma wakuu wa milango, akina Eliezeri, Arieli, Semaya na Elnatani na Yaribu na Elnatani na Natani na Zakaria na Mesulamu na wafunzi Yoyaribu na Elnatani,

17nikawaagiza kwenda kwa Ido aliyekuwa mkuu wa mlango mahali panapoitwa Kosifia, nikawatia vinywani mwao maneno ya kumwambia Ido na ndugu zake na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walioko kule Kosifia, watuletee watakaoitumikia Nyumba ya Mungu wetu.[#Ezr. 2:43.]

18Kwa kuwa mkono wa Mungu ulikuwa nasi, ukatusaidia vema, wakatuletea mtu mwenye akili wa wana wa Mahali, mwana wa Lawi, mwana wa Isiraeli, naye Serebia na wanawe na ndugu zake, watu 18;[#Ezr. 7:6.]

19tena Hasabia na pamoja naye Yesaya wa wana wa Merari na ndugu zake na wana wao, watu 20;

20tena watumishi wa Nyumbani mwa Mungu, Dawidi na wakuu waliowapa Walawi, wawatumikie, hawa watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa 220, wao wote walikuwa wameandikwa majina yao.[#1 Mambo 9:2.]

Mfungo.

21Hapo penye mto wa Ahawa nikatangaza mfungo, tujinyenyekeze mbele ya Mungu wetu na kumwomba, atuongoze sisi na watoto wetu na mali zetu zote kwenye njia inyokayo.

22Kwani nalipatwa na soni za kumwomba mfalme, atupe kikosi cha askari na wenye kupanda farasi, watusaidie njiani kupigana na adui, kwa maana tulikuwa tumemwambia mfalme kwamba: Mkono wa Mungu wetu huwasimamia wote wamtafutao, uwapatie mema; lakini nguvu zake na makali yake huwatokea wote waliomwacha.[#Ezr. 7:6.]

23Tukafunga mfungo na kumwomba Mungu, atupatie hayo mema, naye akatuitikia.

Vipaji, walivyoitolea Nyumba ya Mungu.

24Kisha nikachagua katika wakuu wa watambikaji watu 12, ndio Serebia na Hasabia na pamoja nao ndugu zao kumi,

25nikawapa na kuzipima zile fedha na dhahabu na vile vyombo, Nyumba ya Mungu wetu ilivyotolewa, walivyovitoa mfalme na wenzake wa njama zake na wakuu wake nao Waisiraeli wote walioonekana huko.

26Nikawapa mikononi mwao na kuzipima: fedha vipande 650, ndio shilingi kama milioni 7 na 800000, na vyombo vya fedha vipande 100, ndio shilingi kama milioni na 200000, na dhahabu vipande 100, ndio shilingi kama milioni 22;

27tena vinyweo vya dhahabu 20, kima chao ni dariko 1000, ndio shilingi kama 40000, tena vyombo viwili vizuri vya shaba vilivyometuka kama dhahabu, kima chao kilikuwa sawa na dhahabu.

28Nikawaambia: Ninyi m watakatifu wa Bwana, navyo hivi vyombo ni vitakatifu, nazo hizi fedha na dhahabu ni vipaji, alivyotolewa Bwana Mungu wa baba zenu.

29Kwa hiyo mviangalie sana na kuvilinda, mpaka mtakapovitoa na kuwapimia wakuu wa watambikaji na Walawi na wakuu wa milango ya Isiraeli kule Yerusalemu katika vyumba vya kando penye Nyumba ya Bwana.

30Ndipo, watambikaji na Walawi walipozipokea hizo fedha na dhahabu, walizopimiwa pamoja na vyombo, wavipeleke Yerusalemu katika Nyumba ya Mungu wetu.

Kufika Yerusalemu.

31Kisha tukaondoka hapo penye mto wa Ahawa siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza kwenda Yerusalemu, nao mkono wa Mungu wetu ukatusimamia, ukatuokoa njiani mikononi mwa adui zetu namo mwao wanyang'anyi.

32Tulipofika Yerusalemu tukapumzika siku tatu.

33Siku ya nne hizo fedha na dhahabu pamoja na vyombo zikapimwa Nyumbani mwa Mungu wetu, akapewa mtambikaji Meremoti, mwana wa Uria, mkononi mwake; pamoja naye alikuwako Elazari, mwana wa Pinehasi, tena pamoja nao hawa walikuwako Walawi Yozabadi, mwana wa Yesua, na Noadia, mwana wa Binui.

34Vyote pia vikahesabiwa, vikapimwa, siku hiyo kikaandikwa kipimo chao vyote pamoja.

35Kisha wao waliorudi kwenye uhamisho, walikopelekwa kwa kutekwa, wakamtolea Mungu wa Isiraeli ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima: ng'ombe dume 12 za Waisiraeli wote, madume ya kondoo 96, wana kondoo 77, tena madume ya kondoo 12 kuwa ng'ombe za tambiko za weuo; hawa wote wakawateketeza kuwa ng'ombe za tambiko za Bwana.

36Nazo zile amri za mfalme wakawapa watawala nchi wa mfalme na wenye amri waliozishika nchi za ng'ambo ya huku ya jito kubwa; kwa hiyo hawa wakawasaidia hawa watu katika kazi za Nyumba ya Mungu.[#Ezr. 7:12-26.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania