Ezera 9

Ezera 9

Ezera anajuta kwa ajili ya watu waliooa wanawake wa kimizimu.

1Hayo yalipomalizika, wakuu wakanitokea kwamba: Walio ukoo wa Isiraeli nao watambikaji na Walawi hawakujitenga kabisa na makabila ya nchi hizi walio na mambo mengi ya kutapisha mtu, wao Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori.

2Kwani wamejichukulia wenyewe na wana wao wanawake wa huko; ndivyo, walivyochanganya mazao matakatifu nayo yao ya makabila ya nchi hizi, nao wakuu wa watawalaji ndio walioanza kuinyosha mikono kuyavunja maagano ya Mungu.[#Ezr. 9:11-12; Neh. 13:23.]

3Nilipolisikia neno hili nikazirarua nguo zangu na kanzu yangu, nikang'oa nywele za kichwani na za udevu, nikaja kukaa chini kwa kupigwa na bumbuazi.[#1 Mose 37:34.]

4Ndipo, walipokusanyika kwangu wote walioingiwa na woga wa ajili ya maneno ya Mungu wa Isiraeli, kwa kuwa wao waliorudi kwenye kutekwa waliyavunja maagano yake; mimi nikawa nimekaa chini kwa kupigwa na bumbuazi, mpaka saa ya tambiko ya jioni ilipofika.

5Saa ya tambiko ya jioni ilipofika, nikainuka hapo, nilipojinyenyekeza na kuzirarua nguo zangu na kanzu yangu, nikapiga magoti yangu, nikamkunjulia Bwana Mungu wangu mikono yangu,

6nikasema:

Mungu wantu, kwa kutwezwa nina soni za kukuelekezea uso wangu, Mungu wangu, kwani maovu yetu, tuliyoyafanya, ni mengi sana, yanatupita vichwani petu, nazo manza zetu, tulizozikora, ni kubwa, zinafika hata mbinguni.

7Tangu siku za baba zetu hata siku hii ya leo manza zetu sisi ni kubwa, kwa ajili ya hayo maovu yetu sisi na wafalme wetu na watambikaji wetu tulikuwa tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi hizi, watuue kwa panga, watuteke, watunyang'anye mali zetu, watutukane usoni petu, kama vinavyofanywa hata leo.

8Sasa kitambo kidogo huruma imetutokea iliyotoka kwa Bwana Mungu wetu, akisaza kwetu wengine waliopona, tena akitupa kupigilia mambo mahali pake Patakatifu, Mungu wetu akitaka kuyaangaza macho yetu akitupa kupumua kidogo katika utumwa.[#Yos. 22:23.]

9Kwani sisi tu watumwa, lakini Mungu hakutuacha, ingawa tu watumwa, ila alitupatia upendeleo mbele ya wafalme wa Wapersia, atupe kupumua na kuijenga tena Nyumba ya Mungu wetu na kuyasimamisha tena mabomoko yake na kutupa mahali penye boma, tukae huku Yuda mijini mwa Yerusalemu.[#Yes. 5:5.]

10Na sasa tusemeje, Mungu wetu, hayo yakifanyika kwetu? Kwani tumeyaacha maagizo yako,

11uliyotuagiza vinywani mwao watumishi wako wafumbuaji kwamba: Nchi, mtakayoiingia kuichukua, ni nchi yenye uchafu kwa ajili ya machafu ya makabila ya nchi hizo na kwa ajili ya matapisho yao, waliyoyafurikisha huko toka mpaka hata mpaka kwa machukizo yao ya kimizimu.[#3 Mose 18:24-25.]

12Kwa hiyo msiwaoze wana wao wanawali wenu, wala wana wenu msiwaoze wanawali mwao, wala msiwatafutie kale na kale matengemano na mema yo yote, kusudi ninyi mpate nguvu, myale mema ya nchi hii, mkayaachia wana wenu, yawe fungu lao kale na kale.[#5 Mose 7:2-3.]

13Kweli haya yote yametupata kwa ajili ya matendo yetu mabaya na kwa ajili ya manza zetu zilizo kubwa; lakini wewe, Mungu wetu, umetupunguzia malipizo yaliyoyapasa maovu yetu, tuliyoyafanya, ukatupatia uponya kama huu.

14Kwa hiyo inapasaje kuyavunja maagizo yako kwa kuoana na watu wa makabila haya yatapishayo? Hutatutolea makali, mpaka tuangamie kabisa, pasiwepo masao wala uponya?

15Bwana Mungu wa Isiraeli, wewe u mwongofu; kwani wao waliosalia ni sisi tu tuliopona, kama inavyojulika leo. Tazama, sisi tunasimama mbele yako na kuziungama manza zetu, kwani hakuna awezaye kusimama mbele yako kwa hivyo, alivyo.[#Neh. 9:33.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania