Wagalatia 4

Wagalatia 4

Sisi tu wana wa Mungu.

1Nasema: Kibwana siku anapokuwa mchanga bado, hakuna, apitanacho na mtumwa, angawa ni bwana wa vyote,

2ila hana budi kuwatii walezi na watunza mali, mpaka siku zitimie zilizowekwa na baba yake.

3Vivyo hivyo nasi tulipokuwa wachanga tulikuwa tumeyatumikia kitumwa mambo ya kwanza ya humu ulimwenguni.[#Gal. 3:23; 4:8-10; 5:1; Kol. 2:20.]

4Lakini siku zilipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe, akizaliwa na mwanamke, akawa akiyatii Maonyo,[#Ef. 1:10.]

5kusudi awakomboe walioyatii Maonyo, kwamba tupate kuwa wana.[#Gal. 3:13,26.]

6Kwa sababu m wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe, aingie mioyoni mwetu, ndiye anayetuombea na kulia: Ee, Baba yetu![#Rom. 8:15.]

7Kwa hiyo hu mtumwa tena, ila umekuwa mwana. Lakini kama umekuwa mwana, umekuwa hata mrithi wa Mungu kwa kuwa wake Kristo.*[#Gal. 3:29; Rom. 8:16-17.]

Msirudie kuwa wanyonge!

8Lakini hapo kale, mlipokuwa hammjui Mungu, mlitumikia miungu isiyo miungu kwa hivyo, ilivyo.

9Lakini sasa, mnapomtambua Mungu, tena mnapotambulikana kwake Mungu, mwaigeukiaje tena ile miiko ya kale ikosayo nguvu, iletayo ukiwa tu? Mwatakaje, mwanze kuitumikia tena?[#Kol. 2:20-21.]

10Mwaangalia sana siku na miezi na miongo na miaka.[#Rom. 14:5; Kol. 2:16.]

11Naogopa kwa ajili yenu kwamba: Labda nimejisumbua kwenu bure.[#2 Yoh. 8.]

Paulo anawaonya kama watoto wake.

12Ndugu, nawabembeleza, mwe, kama mimi nilivyo! Maana, mimi ni kama ninyi. Hamkunipotoa lo lote.[#2 Kor. 2:5.]

13Lakini mwajua: hapo kwanza nilipowapitia hiyo mbiu njema nilikuwa mnyonge wa mwili;[#Tume. 16:6; 1 Kor. 2:3.]

14nikawapo nikijaribiwa na mambo yale ya mwili wangu, lakini hamkunibeua, wala hamkunifukuza, ila mmenipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu mwenyewe.

15Yale mashangilio yenu sasa yako wapi? Kwani nawashuhudia ninyi kwamba: Kama ingaliwezekana, mngaliyang'oa hata macho yenu, mkanipa.

16Je? Nimegeuka kuwa mchukivu wenu kwa kuwaambia yaliyo ya kweli?[#Amo. 5:10.]

17Wanavyowahimiza, si vizuri, ila wanataka kuwatenganisha na sisi, mpate kujihimiza kuwatumikia wao.[#Gal. 1:7.]

18Ni vizuri kujihimiza kwa ajili ya jambo zuri po pote, msijihimize hapo tu, nikiwako kwenu.

19Watoto wangu, ninao uchungu, kama nitawazaa mara ya pili, mpaka Kristo aonekane kuwa yumo mwenu.[#1 Kor. 4:15.]

20Ingefaa, niwe kwenu sasa, nikaweza kuigeuza sauti yangu, maana ninawahangaikia ninyi.

Sara na Hagari.

21Mniambie ninyi mnaotaka kujitwika Maonyo: Hamyasikii Maonyo?[#Gal. 3:23; 4:9.]

22Kwani imeandikwa: Aburahamu alikuwa na wana wawili waume, mmoja wa kijakazi, mmoja wa mkewe mwenyewe.[#1 Mose 16:15; 21:2.]

23Lakini yule wa Kijakazi alizaliwa kwa tamaa ya mwili, lakini yule wa mwungwana alizaliwa kwa nguvu ya kiagio[#Rom. 9:7-9.]

24Mambo hayo yako na maana: kwani wale wanawake wawili ndio maagano mawili. La kwanza ndilo lililotokea mlimani kwa Sinai, linalozaa watumwa tu; hili ndio Hagari.[#Gal. 5:1; Rom. 8:15.]

25Maana mlima wa Sinai huitwa Hagari kule Arabuni; nao umelingana na Yerusalemu wa sasa, kwani uko utumwani pamoja na watoto wake.

26Lakini ule Yerusalemu wa juu ndio yule mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi.[#Ebr. 12:22.]

27Kwani imeandikwa:

Shangilia, wewe uliye mgumba, usiyezaa!

Jichekelee na kupaza sauti, wewe usiyeona uchungu wa

kuzaa!

Kwani wana wake yule aliye peke yake ni wengi

kuliko wana wake yule aliye na mumewe.

28Lakini ninyi ndugu, mmekuwa wana wa kiagio kama Isaka.

29Lakini kama hapo kale yule aliyezaliwa kwa tamaa ya mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho, ndivyo, vilivyo hata sasa.[#Gal. 4:23; 1 Mose 21:9.]

30Lakini Maandiko yasemaje?

Mfukuze huyu kijakazi pamoja na mwanawe!

Kwani mwana wa kijakazi hatapata urithi

pamoja na mwana wa mwungwana.

31Kwa hiyo, ndugu, sisi hatu watoto wa kijakazi, ila wake mwungwana.[#Gal. 3:29.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania