The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa pili wa mfalme Dario katika mwezi wa sita siku ya kwanza ya mwezi kwa msaada wa mfumbuaji Hagai neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Saltieli, aliyekuwa mtawala nchi ya Yuda, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, kwamba:[#Ezr. 4:24; 5:1.]
2Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Wao wa ukoo huu husema: Siku ya kujengwa kwake Nyumba ya Bwana, siku hizo hazijaja bado.
3Kwa hiyo neno la Bwana lilikuja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba:
4Je? Siku hizi inawapasa ninyi kukaa katika nyumba zilizopambwa kwa mbao, Nyumba hii ikikaa kuwa kama hame?[#2 Sam. 7:2.]
5Hivi ndivyo, Bwana mwenye vikosi anavyosema sasa: Ielekezeni mioyo yenu, izitazame njia zenu!
6Mmepanda mengi, mkavuna machache; mnapokula hamshibi, mnapokunywa, kiu haiishi; mnapovaa, baridi haiondoki miilini; afanyaye kazi ya mshahara huutia mshahara katika mfuko wenye matundu.[#Hag. 2:16; 5 Mose 28:38.]
7Hivi ndivyo, Bwana mwenye vikosi anavyosema: Ielekezeni mioyo yenu, izitazame njia zenu!
8Pandeni milimani, kaleteni miti, mwijenge hiyo Nyumba! Ndipo, nitakapopendezwa nayo, nitokeze humo utukufu wangu; ndivyo, Bwana anavyosema.
9Mliwaza kupata mengi, lakini mlipoyatazama, yalikuwa machache, nayo mliyoyapeleka nyumbani, nikayapeperusha; hivyo ni kwa sababu gani? ndivyo, aulizavyo Bwana Mwenye vikosi. Ni kwa ajili ya Nyumba yangu iliyo hame tu, nanyi mnajihimiza kila mtu kuijenga nyumba yake.
10Kwa sababu hii mbingu zimewanyima umande, nayo nchi ikawanyima mazao.[#1 Fal. 17:1.]
11Nikauita ukavu, uzijie nchi na milima hii na ngano na pombe mbichi na mafuta nayo yote pia, nchi iyazaayo, uwajie nao watu na nyama na mapato yote ya mikono.[#Hag. 2:17; Amo. 4:9.]
12Ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nayo masao yote ya huo ukoo walipoisikia sauti ya Bwana Mungu wao nayo maneno ya mfumbuaji Hagai, Bwana Mungu aliyemtuma kuwaambia hayo, nao wa ukoo huu wakamwogopa Bwana.
13Ndipo, Hagai aliyetumwa na Bwana alipowaambia wao wa ukoo huu kwa kuagiziwa huo utume na Bwana, akasema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi niko pamoja nanyi.[#Mal. 2:7.]
14Kisha Bwana akaiamsha roho ya mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli, mwana wa Saltieli, nayo roho ya mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nazo roho zao masao yote ya ukoo huu, wakaenda kufanya kazi ya kuijenga Nyumba ya Bwana Mwenye vikosi aliyekuwa Mungu wao.
15Ikawa siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita katika mwaka wa pili wa mfalme Dario.