Hagai 2

Hagai 2

Utukufu wa Nyumba ya Mungu utakaokuwa.

1Siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba neno la Bwana likaja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba:

2Mwambie mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nao walio masao ya ukoo huu, useme:

3Kwenu ninyi mliosalia yuko nani aliyeiona Nyumba hii, ilivyokuwa yenye utukufu wake wa kwanza? Tena sasa mnaiona kuwaje? Machoni penu siyo kama si kitu?[#Ezr. 3:12.]

4Ndivyo, asemavyo Bwana: Sasa Zerubabeli, jipe moyo! Nawe mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, jipe moyo! Nanyi nyote mlio ukoo wa nchi hii, jipeni mioyo! Ndivyo, asemavyo Bwana: Fanyeni kazi, kwani mimi niko pamoja nanyi! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

5Lile Neno, nililoliagana nanyi, mlipotoka Misri, lingaliko; nayo Roho yangu inakaa bado katikati yenu; kwa hiyo msiogope![#2 Mose 19:5; Zak. 4:6.]

6Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Bado kitambo kidogo ndipo, nitakapozitetemesha mbingu na nchi, hata bahari na pakavu,[#Ebr. 12:26.]

7nao wamizimu wote nitawatetemesha. Ndipo, yatakapotokea yapendezayo wamizimu wote, ndipo, nitakapoijaza Nyumba hii utukufu. Bwana Mwenye vikosi ameyasema.

8Yangu ni fedha, yangu ni dhahabu; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

9Utukufu wa Nyumba hii ya nyuma utakua kuliko ule wa Nyumba ya kwanza; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema; kwani mahali hapa nitawapatia watu utengemano; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

10Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa katika mwaka wa pili wa Dario neno la Bwana likaja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba:

11Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Waulize watambikaji maana ya Maonyo ukisema:

12Kama mtu anachukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha kwa huo upindo anagusa mkate au ugali au mvinyo au mafuta au chakula cho chote, je? Nacho kitakuwa kitakatifu? Watambikaji wakajibu, wakasema: Hapana.

13Hagai akauliza tena: Inakuwaje? Mtu aliyejipatia uchafu kwa kugusa mfu, akigusa kimoja chao vitu hivyo, kitakuwa kichafu? Watambikaji wakajibu, wakasema: Ndio, kitakuwa kichafu.[#3 Mose 5:2; 4 Mose 19:22.]

14Hagai akajibu, akasema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Ndivyo walio ukoo huu walivyo, ndivyo hili taifa lilivyo machoni pangu, ndivyo nazo kazi zote za mikono yao zilivyo, ndivyo navyo vipaji vyote wanavyonitolea vilivyo, vyote ni vichafu.

15Sasa ielekezeni mioyo yenu, mwone yaliyowapata kuanzia siku ya leo na siku zote zilizopita, mlipokuwa hamjaweka jiwe kwa jiwe penye Jumba la Bwana.

16Hapo pote yalikuwa hivyo: mtu alipofika penye chungu ya miganda ya ngano yenye pishi ishirini, zikapatikana kumi tu, au alipofika penye kamulio kuchota ndoo hamsini, zikapatikana ishirini tu.[#Hag. 1:6.]

17Nilikuwa nimewapiga ninyi, nikayaunguza mashamba na kuyakausha kabisa, tena nikayanyeshea mvua ya mawe, kazi zote za mikono yenu zisifae, lakini ninyi hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Hag. 1:11.]

18Sasa ielekezeni mioyo yenu, mwone yatakayokuwa kuanzia siku hii ya leo na siku zote zitakazokuja tangu siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, ni kwamba tangu siku hii, msingi wa Jumba la Bwana ulipowekwa. Basi, ielekezeni mioyo mwone,

19kama mbegu za kupanda zitakaa tena chanjani, kama mizabibu na mikuyu na mikomamanga na michekele itaacha tena kuzaa; kuanzia siku hii ya leo nitakubariki.

20Neno la Bwana likamjia Hagai mara ya pili siku ya ishirini na nne ya mwezi huo la kwamba:

21Mwambie mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli kwamba: Mimi nitazitetemesha mbingu na nchi;[#Hag. 2:6.]

22ndipo, nitakapovifudikiza viti vya kifalme vya wafalme, nazo nguvu za nchi za kifalme za wamizimu nitaziangamiza; tena nitayafudikiza magari nao walioyapanda, farasi waanguke pamoja nao waliowapanda, wauawe kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.

23Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Siku hiyo ndipo, nitakapokuchukua wewe Zerubabeli, mwana wa Saltieli, kwa kuwa u mtumishi wangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitakutunza kama pete yangu yenye muhuri, kwani nimekuchagua; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.[#Zak. 4:6-7.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania