Waebureo 12

Waebureo 12

Maana ya kuonywa.

1*Kwa sababu tuna mashahidi walio wengi hivyo, wanaotuzunguka, kama ni wingu, na tuyatue yote yatulemeayo, tujitenge na makosa yanayoshikamana nasi! Tena katika mashindano, tuliyo nayo, na tukikimbilie kikomo na kuvumilia[#Ebr. 10:36; Rom. 7:21; 1 Kor. 9:24.]

2tukiyaelekeza macho kwake Yesu, maana ndiye aliyetuanzisha kumtegemea, tena ndiye anayetaka kukutimiliza. Yeye akayaacha yaliyoufurahisha moyo wake, akajitwika msalaba, pasipo kuona soni. Kisha akaketi kuumeni penye kiti cha kifalme cha Mungu.[#Ebr. 5:8-9; Fil. 2:8,10.]

3Mkumbukeni aliyevumilia alipobishiwa hivyo na wakosaji, msipate kuchoka mioyoni mwenu wala kulegea![#Luk. 2:34.]

4Hapo, mnapopigania kushinda makosa, hamjajifikisha kwenye kuuawa na kumwagwa damu.

5Nanyi mmeyasahau matulizo ya mioyo, aliyotuambia, ya kama tu wana wake kwamba:

Mwanangu, usiseme: Si kitu, ukichapwa na Bwana,

wala usilegee, unapokanywa naye!

6Kwani Bwana humchapa anayempenda,

naye humpiga kila mwana, anayempokea.*

7Vumilieni, mwonyeke! Mungu huwatunza kama wanawe. Kwani ni mwana gani, baba yake asiyempiga?

8Lakini mkiwa hampigwi, kama wote walivyopigwa, basi, ninyi m wana wa kitumwa, ham wana wa kiungwana.[#Sh. 73:14-15.]

9Tena, tukiwa tumepigwa na baba zetu waliotuzaa, tukaonyeka, je? Hatutajikaza sana kumtii Baba aliyezizaa roho zetu, tupate kuishi?[#4 Mose 16:22.]

10Kwani wale waliotupiga siku chache, kama walivyowaza wenyewe kuwa vema. Lakini huyo hutupigia yafaayo, tugawiwe naye utakatifu wake.

11Mapigo yote, yanapokuwapo, hatuyawazii kuwa furaha, ila masikitiko. Lakini siku za nyuma wale waliofundishwa nayo huona, yanavyowazalia matunda yenye utengemano na wongofu.[#2 Kor. 4:17-18.]

12*Kwa hiyo

mikono iliyolegea nayo magoti yaliyopooza yatieni nguvu tena!

13Nayo miguu yenu ishikisheni mapito yaliyo malinganifu!

Maana wachechemeao wasipotezwe, ila wapate kupona vema!

Sikitiko la Esau. Tafuteni kutakaswa!

14Kukimbilieni kupatana nao watu wote! Tena ukimbilieni utakaso! Kwani hata mmoja hatammwona Bwana asipokuwa ametakaswa.[#Rom. 12:18; 2 Tim. 2:22.]

15Angalieni, mtu asiyakose mema, Mungu ayagawiayo! Wala pasichipuke shina lenye uchungu, likiwasumbua na kuchafua wengi![#5 Mose 29:18.]

16Wala kusionekane mwenye ugoni wala mwenye kumbeza Mungu kama Esau aliyeuuza ukubwa wake kwa chakula kimoja![#1 Mose 25:33-34.]

17Kwani mnajua, hapo nyuma, alipotaka kuirithi mbaraka, alitupwa. Kwani hakupata tena penye kujutia, angawa alipatafuta sana kwa machozi.*[#1 Mose 27:30-41.]

18*Kwani hamkufika penye mlima uliogusika, ukiwaka moto, wala penye wingu jeusi na giza na upepo mkali,[#2 Mose 19:12,16,18; 5 Mose 4:11.]

19wala penye mlio wa baragumu na uvumi wa maneno yaliyowashinda wenye kuyasikia, wakaomba, wasiambiwe tena neno.[#2 Mose 20:19.]

20Kwani hawakuweza kulipokea lile agizo la kwamba: Hata nyama atakayeugusa mlima auawe kwa kupigwa mawe au kwa kuchomwa mikuki.[#2 Mose 19:13.]

21Nayo yaliyoonekana yalikuwa yamewatia woga mkubwa sana, hata Mose akasema, nimeingiwa na kituko, nikatetemeka.

22Ila mmefika penye mlima wa Sioni, ndipo penye mji wa Mungu Mwenye uzima, ni Yerusalemu ulioko mbinguni, panapo malaika maelfu na maelfu wanaowashangilia[#Gal. 4:26; Ufu. 5:11; 14:1; 21:2.]

23wateule waliozaliwa wa kwanza, ndio walioandikwa majina mbinguni. Kisha mmefika penye Mungu aliye mhukumu wa watu wote; ndipo, nazo roho za wenye wongofu waliotimilika zilipo,[#Luk. 10:20.]

24ndipo, alipo naye Yesu aliyetuletea Agano Jipya, hata damu ya kunyunyizia inayosema na nguvu kuipita ile ya Abeli ipo papo hapo.*[#Ebr. 9:15; 11:4; 1 Mose 4:10.]

Ufalme usiowezekana kutingishwa.

25Angalieni, msimkataye yeye anayesema! Kwani kama wale waliomkataa, aliposema nao nchini, hawakuweza kukimbia, sisi tutawezaje kukimbia tukijitenga naye, anaposema nasi toka mbinguni?[#Ebr. 2:2; 10:28-29.]

26Sauti yake ndiyo iliyoitingisha nchi siku ile; lakini sasa kiko kiagio cha kwamba: Mimi nitatetemesha tena mara moja, si nchi tu, ila hata mbingu.[#Hag. 2:6.]

27Lakini neno hili la kwamba: Tena mara moja linaeleza, ya kuwa vinavyotingishika hugeuka, kwa kuwa viliumbwa hivyo, kusudi vile visivyotengishika vikae vivyo hivyo.

28Kwa sababu tumepewa ufalme usiotingishika, na tuyavumishe hayo mema, tuliyogawiwa! Hivyo tutamtambikia Mungu, kama inavyompendeza, tukimcha na kumwogopa.

29Kwani Mungu wetu ni moto ulao kwa kuteketeza.[#5 Mose 4:24; 9:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania