Hosea 13

Hosea 13

Mabaya yatakayowapata Waisiraeli hayawezi kuutangua wokovu.

1Efuraimu aliposema, watu walitetemeka;

kwani alikuwa mkuu kwao Waisiraeli.

kisha akakora manza kwa kumtumikia Baali, basi akafa.

2Na sasa wanaendelea kukosa

wakijifanyizia vinyago kwa fedha zao,

vingine wanavichonga, kama wanavyojua;

vyote pia ni kazi za mafundi.

Kwa ajili yao wenyewe husema:

Watoao watu kuwa ng'ombe zao za tambiko sharti wanonee

ndama!

3Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi

na kama umande ukaukao upesi,

au kama makapi yanayopeperushwa penye kupuria

au kama moshi utokao katika bomba.

4Lakini mimi Bwana ni Mungu wako

tangu hapo, nilipokutoa katika nchi ya Misri;

nawe usijue mungu mwingine ila mimi,

hakuna mwokozi, nisipokuwa mimi.

5Mimi nilikujua ulipokuwa nyikani

katika nchi kavu yenye kiu.

6Lakini walipoona malisho mema wakashiba;

napo waliposhiba, mioyo yao ikajikuza, kwa hiyo

wamenisahau.

7Ndipo, nilipowageukia kuwa kama simba,

nikawavizia kama chui njiani,

8niwarukie kama nyegere aliyenyang'anywa watoto,

niwapasue vifua vifunikavyo mioyo yao,

niwale hapo hapo kama simba jike,

kisha nyama wa porini wawanyafuenyafue,

9Haya ndiyo yanayokuangamiza, Isiraeli,

ya kuwa unanikataa mimi niliye msaada wako

10Mfalme wako yuko wapi,

akuokoe katika miji yako yote?

Wako wapi waamuzi wako, uliowaambia:

Nipeni mfalme na wakuu!

11Mimi nilikupa mfalme kwa kukasirika kwangu,

tena nikamwondoa kwa makali yangu yenye moto.

12Manza zake Efuraimu zimefungwa pamoja,

makosa yake yakawekwa fichoni.

13Uchungu wa mzazi utamjia,

lakini yeye ni mwana asiyejua kitu;

saa yake itakapofika, haji kusimama hapo,

wana wanapotokea tumboni mwa mama.

14Nitawakomboa katika nguvu za kuzimuni

na kuwaokoa kufani.

Wewe Kifo, magonjwa yako yauayo yako wapi?

Wewe Kuzimu, uchungu wako uko wapi?

Ndipo, yawezayo kujutisha yatakapokuwa yamefichwa,

macho yangu yasiyaone.

15Lakini ijapo awe mwenye kuzaa miongoni mwa ndugu zake,

pumzi ya Bwana itamjia

kuwa upepo utokao maawioni kwa jua upande wa nyikani,

kisima chake kikauke, nacho kijito chake kipwe.

Yule ndiye atakayeviteka

vilimbiko vyote vya vyombo vyote pia vipendezavyo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania