The chat will start when you send the first message.
1Tamko zito la kuwaambia Wababeli, Yesaya, mwana wa Amosi, aliloliona:[#Yer. 50—51.]
2Twekeni bendera mlimani juu kileleni palipokatwa miti!
Walioko karibu wapalizieni sauti na kuwapungia mikono,
waje kuingia malangoni mwenye wakuu wa nchi!
3Wao waliojitakasia mimi nimewaagiza kuja huku,
nikawaita nao walio mafundi wangu wa kupiga vita,
wapige yowe na kujikuza wakiyatimiza makali yangu.
4Makelele mengi mno yako milimani kama ni ya watu wengi,
sauti za uvumi ziko za wafalme wanaokusanya watu wao.
Bwana Mwenye vikosi anavitazama
vikosi vyake vya kwenda vitani.
5Wamekuja na kutoka nchi za mbali mapeoni kwa mbingu,
yeye Bwana na vyombo vya machafuko yake
vitakavyoziangamiza nchi zote.
6Pigeni vilio! Kwani siku ya Bwana iko karibu;
itakuja kama pigo la umeme, likitoka kwake Mwenyezi.
7Kwa hiyo mikono yote italegea,
nayo mioyo yote ya watu itayeyuka.
8Vituko na masongano na maumivu yatawashika,
wajipinde kama mzazi,
watatumbulizana macho kwa kushangaa,
nyuso zao zitawaiva kama ni zenye moto.
9Tazameni: Siku ya Bwana inakuja,
inaleta mastuko na makali na machafuko yenye moto,
yaziangamize nchi, ziwe jangwa,
kwa kuwamaliza wakosaji, wasikae.
10Kwani nyota za mbinguni kama kilimia na wenziwe
hazitaangaza mwanga wao,
jua nalo litakapokucha litakuwa jeusi lenye giza,
nao mwezi hautaumulikisha mwanga wake.
11Nitayaumbua mabaya kwao wakaao nchini,
nayo mapotovu yao kwao wasionicha,
niyanyamazishe majivuno yao wajitutumuao,
niwanyenyekeze wakorofi wajiwaziao kuwa wakuu.
12Nitafanya, watu wawe wachache kuliko dhahabu,
kweli wenye kufa watakuwa haba kuliko dhahabu ya Ofiri.
13Kwa sababu hii nitazitikisa mbingu,
nayo nchi itatenguliwa mahali pake kwa kutetemeka,
makali ya Bwana Mwenye vikosi yatakapotokea,
siku ya kuyaleta machafuko yake yenye moto itakapotimia.
14Watakuwa kama paa akimbiaye kwa kustushwa
au kama kondoo wakosao mchungaji;
ndivyo, watakavyowageukia kila mtu wenziwe wa kwao,
ndivyo, watakavyokimbilia kila mtu shamba lake.
15Kwani kila atakayeonekana atachomwa,
kila atakayekamatwa atauawa kwa upanga.
16Nao watoto wao wachanga watapondwa machoni pao,
nyumba zao zitatekwa, wanawake wao watatiwa soni.
17Jueni, nitawaletea Wamedi wasiotaka fedha,
wasiopendezwa na dhahabu.
18Lakini pindi zao hupiga vijana, wafe;
hata wenye mimba hawawaonei huruma,
wala macho yao hayatazami watoto, waache kuwaua.
19Kweli Babeli umekuwa urembo wa wafalme
nao utukufu, Wakasidi waliojivunia,
lakini Mungu atauangamiza,
kama alivyoiangamiza miji ya Sodomu na ya Gomora.
20Hautakaa kale na kale, wala havitatua humo vizazi na vizazi,
Waarabu tu hawatapiga mle mahema yao,
wala wachungaji hawatawapumzisha kondoo wao hapohapo.
21Ila nyama wa porini watalala hapo,
nyumba zao zitajaa mabundi,
nao mbuni watalala huko,
hata mashetani watachezacheza hapo.
22Mbwa wa mwitu watalia majumbani mwao,
nao mbweha katika nyumba zao zilizokuwa na furaha tu.
Kweli mwisho wa mji huo uko karibu kutimia,
siku zake hazitakawilia.