Yesaya 14

Yesaya 14

Shangilio lao Waisiraeli waliookoka Babeli.

1Kwani Bwana atawahurumia wa Yakobo,

atawachagua Waisiraeli tena,

awarudishe katika nchi yao, watue kuko huko,

hata wageni wataandamana nao,

wajitie katika mlango wa Yakobo.

2Watu wengine watawachukua, wawapeleke kwao,

kisha mlango wa Isiraeli utawatumia katika nchi ya Bwana

kuwa watumishi wao wa kiume na wa kike.

Hivyo watawateka waliowateka, wawatawale waliowasonga.

3Hapo Bwana atakapokupatia pa kutulia na kuyapumzikia masumbufu na mahangaiko na matumishi yako magumu, waliyokutumikisha,

4utamwimbia mfalme wa Babeli wimbo huu wa kumfyoza kwamba:

Kumbe mwenye kusonga ametulia!

Kumbe napo tulipoumizwa pametulia!

5Bwana amezivunja fimbo zao wasiomcha,

fimbo zao waliotutawala!

6Ni zile fimbo zao walioyapiga

makabila ya watu kwa ukali pasipo kukoma.

Ni fimbo zao walioponda mataifa mazima

wakiyakanyaga kwa ukali tu pasipo huruma.

7Nchi yote nzima imetulia kimya, wote pia wanapiga shangwe.[#Hab. 2:20.]

8Hata mivinje imefurahi pamoja na miangati ya Libanoni kwamba:

Tangu hapo ulipotulizwa hakuna aliyepanda kutukata.

9Kule chini kuzimuni kumevurugika kwa ajili yako:

kwa kungoja, uje, kukawaamsha wazimu wote,

waliokuwa wenye nguvu katika nchi,

kukawainua wafalme wote, wao wa kimizimu,

waondoke katika viti vyao vilivyo vya kifalme.

10Wote pamoja wanakuzomea kwamba:

Kumbe nawe umegeuzwa kuwa mnyonge kama sisi!

Ukafananishwa kuwa sawasawa kama sisi!

11Kumbe nao utukufu wako umekumbwa kushuka kuzimuni

pamoja na milio ya mapango yako!

Chini umetandikiwa funyo kuwa kilalio chako,

nalo blanketi lako la kujifunika ni vidudu.

12Kumbe umeanguka toka mbinguni,

ulimokuwa nyota yenye mwanga

uliokuwa kama mwanga wa macheche ya jua!

Kumbe umepondwa, ukaanguka chini

uliyeyalaza mataifa chini yako!

13Nawe ulijiwazia moyoni mwako kwamba:

Na nipande mbinguni kwenye nyota za Mungu,

nikisimike kiti changu cha kifalme huko juu,

nikae mlimani kwa miungu mapeoni kwa kaskazini!

14Na nipande kupita mawingu yaliyoko mbinguni juu,

nijifananishe kuwa sawasawa naye Mwenyezi!

15Kumbe umeshushwa kuzimuni mapeoni kwenye mashimo!

16Wakuonao watakutumbulia macho, wakutambue kwamba:

Je? Huyu siye aliyeitetemesha nchi,

aliyewatikisa nao wafalme?

17Je? Siye aliyezigeuza nchi kuwa mapori tu?

Je? Siye aliyebomoa miji mizima?

Je? Siye aliyewakataza wafungwa wake, wasirudi kwao?

18Wafalme wote wa kimizimu hulala kwenye utukufu,

kila mtu chumbani mwake;

19lakini wewe umetupwa mbali, usifike kaburini mwako,

ukawa kama tawi litapishalo watu,

ukafunikwa na mizoga yao waliochomwa kwa panga,

waliotupwa mashimoni kwenye majiwe,

ukawa kama kibudu kinachokanyagwa.

20Wewe hutafika kaburini pamoja nao wale,

kwani nchi yako umeiangamiza, nao walio ukoo wako umewaua.

Uzao wao wasiomcha hautatajwa kale na kale.

21Watu husema: Na tuwatengenezee wana wao pa kuwachinjia

kwa ajili ya manza, baba zao walizozikora,

wasije kuinuka tena na kutwaa nchi

na kupajaza hapa juu nchini miji yao!

22Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi:

Nitawainukia, niling'oe jina la Babeli nalo sao lake,

wanawe na wajukuu; ndivyo, asemavyo Bwana.

23Nitaiweka nchi yao kuwa kao lao nungu,

iwe yenye mabwawa ya matopetope tu;

nitapazoa kabisa na kutumia kizoleo kiangamizacho!

Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.

Kuangamia kwao Waasuri.

24Bwana Mwenye vikosi ameapa kwamba:

Kama nilivyoyawaza moyoni, yatakuwa vivyo hivyo;

kama nilivyokata shauri, yatatimia vivyo hivyo.

25Nitawaponda Waasuri katika nchi yangu,

nitawamaliza na kuwakanyagakanyaga mlimani kwangu.

Mizigo yao iondoke kwao wanaokaa kule,

hata miti ya kuchukulia mizigo iondoke kwao mabegani.

26Hili ndilo shauri, alilozipigia nchi zote;

kwa hiyo mkono wake uko umewakunjukia wamizimu wote.

27Kwani Bwana Mwenye vikosi akikata shauri,

yuko nani atakayelitangua?

Yuko nani atakayeukunja mkono wake uliokunjuka?

Kuangamia kwao Wafilisti.

29Ninyi wa nchi nzima ya Ufilisti, msifurahie kwamba:

Fimbo iliyotupiga imevunjika!

Kwani kooni mwa nyoka atatoka pili,

naye atazaa nondo mwenye mabawa.

30Hapo ndipo, wanyonge waliosongeka sana watakapolisha,

nao wakiwa watalala hapohapo na kutulia vizuri;

lakini mizizi yako nitaifisha kwa njaa,

nao watakaosalia atawaua yule nondo.

31Piga kilio, wewe lango! Omboleza, wewe mji!

Zimia, nchi nzima ya Ufilisti!

Kwani uko moshi utakaotoka kaskazini,

kwao asiwe atakayeachwa peke yake kambini.

32Nao majumbe wa taifa la kimizimu watapata jibu gani?

Ni hili: Bwana ameushikiza Sioni!

Wanyonge wao walio ukoo wake watapakimbilia!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania