Yesaya 15

Yesaya 15

Mapatilizo ya Wamoabu.

(Taz. Yer. 48.)

1Kumbe Ari wa Moabu umebomolewa usiku, ukaangamia!

Kumbe Kiri wa Moabu nao umebomolewa usiku!

2Wabeti na Wadiboni wanapanda vilimani kupiga vilio;

kule Nebo na Medeba Wamoabu wanaomboleza,

vichwa vyao vyote viko na vipara,

nazo ndevu zote zimekatwa.

3Wakitoka nje huwa wamejivika magunia,

wao wote, kama wamo vipaani au kama wamo mawanjani,

wanapiga vilio na kutoa machozi.

4Wahesiboni na Waelale wanapiga makelele,

sauti zao zinasikilika mpaka Yasa.

Kwa hiyo nao wapiga vita wa Moabu wanapiga yowe,

maana mioyo yao imekwisha kuwa mibaya.

5Moyo wangu unawalilia Wamoabu,

kwa kukimbizwa wamefika Soari na Eglati wa tatu,

hata njia za Luhiti watu wanazipanda na kulia,

vilevile njiani kwenda Horonemu

wanapiga makelele ya kuyalilia maangamizo.

6Kwani maji ya Nimurimu yamekupwa, pakawa nyika,

majani ya hapo yamenyauka, malisho yamekauka,

hakuna kitakachoota hapo tena.

7Kwa sababu hii wanayapeleka masao ya mali zao,

hata malimbiko yao, wayavushe mtoni huko nyikani.

8Vilio vimezunguka kwenye mipaka yote ya Moabu,

maombolezo yao yanasikilika mpaka Eglemu,

hata Beri-Elimu yamefika maombolezo yao.

9Kwani maji ya Rimoni yamejaa damu;

nao Wamoabu waliokimbilia Dimoni

nitawaletea kibaya kingine:

ni simba atakayewamaliza

pamoja nao waliosalia katika nchi yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania