The chat will start when you send the first message.
1Watumeni wana kondoo wapasao mtawala nchi,
watoke magengeni, wapite nyikani,
wafike mlimani kwa Binti Sioni!
2Kama ndege wanavyohangaika na kurukaruka
wakistushwa matunduni mwao,
ndivyo, wana wa Moabu watakavyokuwa
na kuvikimbilia vivuko vya Arnoni.
3Tupatieni mzungu! Tupatanisheni!
Vikuzeni vivuli vyenu vya mchana,
viwe virefu kama vya jioni,
viwe maficho yao wafukuzwao! Msiwachongee waliokimbia!
4Acha, wafukuzwao Moabu wafikie kwako!
Wawie ficho machoni pao wanaowakimbiza,
sharti siku zao wawasongao ziishe, maangamizo yamalizike,
nao waliowaponda watoweke katika nchi yao!
5Hapo kiti cha kifalme kitasimikwa kwa upole,
naye atakayekikalia kwa welekevu hemani mwa Dawidi
atakuwa mwamuzi atafutaye yanyokayo kwa kujua wongofu.
6Tuliyasikia majivuno ya Wamoabu kuwa makuu sana,
lakini hayo matukuzo na majivuno na machafuko yao ni maneno makuu tu.
7Kwa hiyo Wamoabu wote pamoja
na waipigie kilio nchi yao ya Moabu,
na wayalilie maandazi ya zabibu ya Kiri-Hereseti
kwa kupondeka rohoni.
8Kwani mashamba ya Hesiboni yamenyauka,
hata mizabibu ya Sibuma
iliyoleta zabibu zenye mvinyo kali
za kulevya nao wakuu wa wamizimu;
matawi yao yaliendelea sana,
yakafika Yazeri, mengine yakapotea nyikani,
miche yao ikaenea po pote mpaka kwenye bahari.
9Kwa hiyo nami ninaililia mizabibu ya Sibuma
pamoja na watu wa Yazeri,
machozi yangu yazinyeshee nchi za Hesiboni na za Elale,
kwani mazomeo yamewaangukia siku hizi za kiangazi
zilizo siku zenu za mavuno yenu.
10Shangwe za furaha zikatoweka mashambani,
nako mizabibuni hawapigi vigelegele wala mashangilio,
wala hakuna anayekamulia mvinyo makamulioni,
nyimbo za wakamuliaji nimezinyamazisha.
11Kwa hiyo nasikia ndani yangu mlio
kama wa zeze wa kuwalilia Wamoabu,
namo kufuani umo mlio
wa kuwalilia watu wa Kiri-Heresi.
12Napo hapo, Wamoabu watakapotokea vilimani juu
na kujisumbulia hapohapo,
napo, watakapoingia patakatifu pao kuomba,
hakuna watakachojipatia.
13Hilo ndilo tamko zito, Bwana alilolisema kale la kuwaambia Wamoabu;
14lakini sasa Bwana anasema hivi:
Itakapotimia miaka mitatu
iliyo kama miaka ya kibarua,
ndipo, utukufu wa Moabu utakapokuwa umebezeka,
nao ulikuwa haukupimika kwa wingi wa watu,
nalo sao lao litakuwa limepunguka,
liwe dogo sana pasipo nguvu zo zote.