The chat will start when you send the first message.
1Na mwone, mji wa Damasko ukiondolewa, usiwe mji,
utakuwa chungu la mawe yatawanyikayo.
2Miji ya Aroeri itakuwa imeachwa nayo, itakuwa malisho,
makundi yatapumzikia hapo pasipo kuona atakayeyastusha.
3Hivyo ngome ya Efuraimu itapotea,
ufalme utakapoondoka Damasko,
nalo sao la Ushami litakuwa kama utukufu wa Waisiraeli;
ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.
4Siku ile ndipo, utukufu wa Yakobo utakapopunguka sana,
nao mwili wake mnene utakuwa gofu la mtu tu.
5Itakuwa kama mvunaji akishika manyasi,
mkono wake ukate masuke,
au itakuwa kama mtu akitaka kuokota masuke
katika bonde la Refaimu.
6Watakaosalia watakuwa wa kuokoteza,
itakuwa kama penye mavuno ya matunda ya mchekele:
mawili matatu yatasalia kileleni juu kabisa,
manne matano yatasalia katika matawi ya mti, ulioyazaa;
ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wa Isiraeli.
7Siku ile watu watamtazamia tena aliyewaumba,
macho yao yatamwelekea Mtakatifu wa Isiraeli;
8hawatapatazamia tena mahali pao pa kutambikia,
mikono yao ilipopatengeneza,
wala hawatataka kuiona tena mifano ya mwezi wala ya jua,
waliyoifanya kwa vidole vyao.
9Siku ile miji yenu yenye maboma itageuka
kuwa kama mahame ya mwituni au ya milimani,
waliyoyaacha walipowakimbia Waisiraeli,
maana itakuwa peke yao tu pasipo watu.
10Kwani umemsahau Mungu aliye wokovu wako,
hukuukumbuka mwamba ulio nguvu yako.
Kwa hiyo panda tu mashamba ya kupendeza
na kumwaga mle mbegu za miti migeni!
11Siku ya kupandia uzichipuze, kesho zipate kuchanua!
Lakini mavuno yatakuwa yamekimbia siku ile,
utakapougua kwa kupatwa na maumivu yasiyopona.
12Je? Uvumi gani huu wa makabila mengi ya watu?
Wanavuma, kama maji yanavyovuma yakiwa mengi.
Ni ngurumo gani ya makabila ya watu?
Wananguruma kama ni ngurumo ya maji yenye nguvu.
13Lakini ijapo makabila ya watu yangurume,
kama maji mengi yanavyonguruma,
yeye atakapowakaripia, watakimbia mbali sana,
watafukuzwa, waruke kama makapi,
yakipeperushwa na upepo vilimani juu,
au kama mavumbi, yakichukuliwa na kimbunga.
14Ilipokuwa jioni, mastuko yakawa yangaliko bado,
lakini kulipotaka kupambazuka, yalikuwa yametoweka.
Hilo ndilo fungu lao waliotaka kututeka,
hilo ndilo gawio, kura lililowapatia wao
waliotaka kuzipokonya mali zetu.