The chat will start when you send the first message.
1Ninyi mliotoka katika nchi yenye vivuli viwili
iliyoko ng'ambo ya majito ya Nubi!
2Ninyi wajumbe mliokuja mkilifuata lile jito kubwa
katika mitumbwi yenu ya mafunjo ya kwendea juu ya maji,
ninyi wajumbe wepesi, nendeni kwenu
kwenye watu warefu sana wajipakao mafuta.
Ndio watu wanaoogopwa kwao hata kungineko,
kwa kuwa ni wenye nguvu za kuponda watu,
nayo nchi yao inakatwakatwa na mito.
3Nyote mkaao ulimwenguni, nyote mliotua nchini,
bendera itakapotwekwa milimani, itazameni!
Mabaragumu yatakapopigwa, yasikilizeni!
4Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wangu anavyosema:
Nitatulia, nichungulie kwenye kao langu
kama mwangaza mweupe wa jua kali la mchana,
au kama wingu lenye umande siku za mavuno.
5Kwani mavuno yanapokuwa hayajafika bado,
maua yakiisha kupakatika, kole likiivisha zabibu zake,
ndipo, anapoyakata kwa kisu matawi yenye majani tu,
ndipo, anapoiondoa miche, itoke kabisa.
6Wote pamoja wataachiliwa madege wakaao milimani
nao nyama wa porini,
madege makubwa wakae hapo siku za kiangazi,
nao nyama wote wa porini wawe hapo siku za kipupwe.
7Siku zile Bwana Mwenye vikosi ataletewa matunzo nao walio watu warefu sana wajipakao mafuta. Ndio wale watu wanaoogopwa kwao na kungineko, kwa kuwa ni watu wenye nguvu za kuponda watu, nayo nchi yao inakatwakatwa na mito. Hao watatua matunzo yao mahali penye Jina la Bwana Mwenye vikosi, ndipo mlimani kwa Sioni.[#Sh. 68:30,32.]