The chat will start when you send the first message.
1Tazameni: Bwana amepanda wingu jepesi, aje Misri!
Vinyago vya Misri vinatikisika usoni pake,
mioyo yao Wamisri imeyeyuka vifuani mwao.
2Nitawachochea Wamisri, wapigane na Wamisri wenzao,
wagombane mtu na ndugu yake, hata mtu na mwenziwe,
hata mji upigane na mji mwingine,
vilevile ufalme ugombane na ufalme mwingine.
3Hapo ndipo, roho zao Wamisri zitakapozimia vifuani mwao,
nikiitengua mizungu yao; nao watatafuta msaada
kwa vinyago na kwa waganga, kwa wachawi na kwa waaguaji.
4Nitawafungia Wamisri mikononi mwa bwana mgumu,
mfalme, mwenye ukorofi, awatawale!
Ndivyo, asemavyo Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi.
5Kisha maji yatakupwa baharini,
nao mto mkubwa utakauka, pawe pakavu tu.
6Mifereji mikubwa ya maji itanuka vibaya,
nayo mito ya Misri ya chini itakuwa minyonge,
kisha itakauka nayo,
hata matete na manyasi yatanyauka.
7Viwanda vilivyoko kando ya mto kwenye kingo za mto,
nayo mashamba yote ya mtoni yatanyauka,
yatakauka kabisa yatoweke.
8Wavuvi watalia, pamoja nao wote
waliokamata samaki mtoni kwa ndoana watasikitika,
nao waliotanda nyavu majini watafifia.
9Hata wafanyao kazi za pamba wataangamia
pamoja nao wafumao nguo nyeupe.
10Hivyo misingi yao itakuwa imepondeka,
wote wafanyao kazi za kibarua wataumia rohoni.
11Wakuu wa Soani watakuwa wamepumbaa kabisa;
nao wajuzi wa Farao wasiokosa mizungu,
hapo mizungu yao itakuwa ujinga tu.
Mtawezaje kumwambia Farao: Mimi ni mwana wao watambuzi?
au: Mimi ni mwana wao wafalme wa kale?
12Sasa watambuzi wako wako wapi?
Kama wanalitambua, na wakufumbulie shauri,
Bwana Mwenye vikosi aliloikatia nchi ya Misri!
13Wakuu wa Soani ni wajinga kweli,
nao wakuu wa Nofu wamedanganyika,
waliokuwa vichwa vya milango wameiangamiza Misri.
14Bwana amemwaga mioyoni mwao roho za kizunguzungu,
wawapoteze Wamisri katika matendo yao yote,
wapepesuke kama mlevi kwenye matapiko yake.
15Hakuna tendo tena, Wamisri, watakalolitenda,
kama ni kichwa au mkia, kama ni makuti au majani.
16Siku zile Wamisri watakuwa kama wanawake, watetemeke kwa kuyastukia matisho ya mkono wa Bwana Mwenye vikosi, atakaowakunjulia.
17Hapo nchi ya Yuda itawawia Wamisri kitisho, kila mtu aingiwe na kituko atakaposikia, ikitajwa, kwa ajili ya shauri la Bwana Mwenye vikosi, alilowakatia.
18Siku ile miji mitano itakuwako katika nchi ya Misri itakayosema msemo wa Kanaani, itakayoapa na kulitaja Jina la Bwana Mwenye vikosi, mmoja wao utaitwa Mji wa Mabomoko.[#Yes. 65:16; Yer. 12:16.]
19Siku zile patakuwako pa kumtambikia Bwana katika nchi ya Misri katikati na nguzo ya Bwana iliyojengwa kwa mawe mpakani kwake.
20Hivyo Bwana Mwenye vikosi atakuwa na kielekezo cha kumshuhudia katika nchi ya Misri; napo, watakapomlilia Bwana kwa ajili yao wawasongao, atatuma mwokozi, awagombee, awaponye.
21Ndivyo, Bwana atakavyojulikana kwa Wamisri, kweli Wamisri watamjua Bwana siku zile, watamtumikia na kumtolea ng'ombe za tambiko na vipaji vingine vya tambiko, nayo waliyomwagia Bwana kumpa, watayalipa.
22Itakuwa hivyo: Bwana akiwapiga Wamisri na kuwaponya, nao wakimrudia Bwana, atawaitikia, wakimwomba, awaponye kabisa.
23Siku zile itakuwako barabara toka Misri kwenda Asuri, nao Waasuri watakuja Misri, nao Wamisri watakuja Asuri kuamkiana, hivyo Wamisri na Waasuri watatumikiana.
24Siku zile Isiraeli atakuwa wa tatu wa kupatana na Misri na Asuri, hawa watakuwa mbaraka katika nchi katikati.
25Naye Bwana Mwenye vikosi atawabariki na kusema: Wabarkiwe Wamisri walio ukoo wangu! Wabarikiwe Waasuri walio kazi ya mikono yangu! Wabarikiwe Waisiraeli walio fungu langu, nililojipatia![#Rom. 15:10.]