Yesaya 2

Yesaya 2

Yerusalemu utakuwa ufalme wa utengemano.

1Hili ni neno, Yesaya, mwana wa Amosi, aliloliona la Yuda na la Yerusalemu:

(2-4: Mika 4:1-3.)

2*Mwisho wa siku utakapotimia,

mlima wenye Nyumba ya Bwana utakuwa umeshikizwa na nguvu,

uwe wa kwanza wa milima, uende juu kuliko vilima vingine,

hata wamizimu wote wataukimbilia.

3Makabila mengi ya watu watakwenda wakisema:

Njoni, tupande mlimani kwa Bwana

kwenye Nyumba ya Mungu wa Yakobo!

Atufundishe, njia zake zilivyo,

tupate kwenda na kuifuata mikondo yake!

Kwani ufundisho utatoka Sioni,

namo Yerusalemu litatoka Neno la Bwana.

4Ndipo, atakapowaamulia wamizimu

na kuyapatiliza makabila mengi ya watu;

nao watazifua panga zao kuwa majembe,

hata mikuki yao kuwa miundu,

kwani halitakuwako tena kabila

litakalochomolea jingine upanga,

wala hawatajifundisha tena mapigano ya vita.

Mapatilizo yao waliomwacha Mungu.

5Mlio wa mlango wa Yakobo, njoni,

tuendelee pamoja katika mwanga wa Bwana!*

6Kwani umewatupa wao waliokuwa ukoo wako,

wale wa mlango wa Yakobo,

kwani wamejaa mambo yatokayo maawioni kwa jua,

huagulia mawingu kama Wafilisti,

hufanya maagano nao vijana wa nchi ngeni.

7Nchi yao ikajaa fedha na dhahabu, malimbuko yao hayana mwisho;

nchi yao ikajaa farasi, magari yao hayana mwisho.

8Nchi yao ikajazwa vinyago;

huziangukia kazi za mikono yao, walizozitengeneza kwa vidole vyao.

9Watu wakavinyenyekea, mabwana nao wakaviinamia;

hivi hatawaondolea kabisa.

10Nenda magengeni! Jifiche uvumbini!

Usiuone uso wake ukutishao wala utukufu wa ukuu wake!

11Macho ya watu wajivunao yatanyenyekezwa,

nao waume wajikwezao watainamishwa,

kwa maana atakayetukuka siku ile ni Bwana peke yake.

12Kwani siku ya Bwana Mwenye vikosi itawajia watu,

wanyenyekezwe wenye majivuno na ukuu, nao wajitukuzao;

13nayo miangati ya Libanoni iliyo mikubwa na mirefu,

nayo mikwaju yote ya Basani inyenyekezwe,

14nayo milima mirefu yote,

hata vilima vyote vinavyokwenda juu sana;

15nayo minara mirefu yote,

hata maboma yote yenye nguvu;

16nazo merikebu zote za Tarsisi ziletazo mali

na vitu vizuri vyote pia, watu wanavyovitamani.

17Nao watu wajivunao watainamishwa,

hata waume wajikwezao watanyenyekezwa,

kwa maana atakayetukuka siku ile ni Bwana peke yake,

18navyo vinyago vitatoweka vyote pia.

19Ndipo, watakapokwenda mapangoni kwenye magenge

namo mashimoni kwenye nchi kavu,

wasiuone uso wa Bwana uwatishao wala utukufu wa ukuu wake,

atakapoinuka kuistusha nchi.

20Siku ile watu watavikupa vinyago vyao,

ijapo viwe vya fedha na vya dhahabu;

hivyo, walivyojifanyizia vya kuvitambikia,

watavitupa kwenye panya na mapopo,

21wapate kujiendea kwenye nyufa za magenge

na kwenye mapango ya miamba,

wasiuone uso wa Bwana uwatishao wala utukufu wa ukuu wake,

atakapoinuka kuistusha nchi.

22Sasa waacheni wale watu! Nao puani mwao ni pumzi tu;

huwaziwa kuwa nini?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania