The chat will start when you send the first message.
1Kama upepo wenye nguvu unavyovuma upande wa kusini,
ndivyo, mambo yanavyotoka nyikani katika nchi inayoogopwa.
2Nimefumbuliwa na kuonyeshwa yenye ugumu:
mdanganyifu hudanganya, naye mwangamizaji huangamiza.
Pandeni, Waelamu! Shambulieni, Wamedi!
Hivyo nitawanyamazisha wote waliowapigia kite.
3Kwa hiyo viuno vyangu vimeenea kukauka,
uchungu ukanishika kama uchungu wa mwanamke azaaye,
kizunguzungu kikanipata, nisisikie, nikastushwa, nisione.
4Roho yangu ikazimia, mastuko yakanigundua;
saa za jioni, nilizozipenda, zikawa za kunitetemesha.
5Wao hutandika meza, huweka wangoja zamu, hula, hunywa.
Mara wanaambiwa: Inukeni, wakuu! Zipakeni ngao mafuta!
6Kwani ndivyo, Bwana alivyoniambia:
Nenda, uweke mlinzi, akuambie, atakayoyaona!
7Atakapoona kikosi cha watu waliopanda farasi,
wakienda wawiliwawili,
hata kikosi cha punda na kikosi cha ngamia,
na aangalie sana kwa uangalifu mwingi.
8Akaita na kupaza sauti kama simba kwamba:
Bwana, hapa kilindoni mimi ninasimama mchana kutwa,
nao usiku kucha nimewekwa mimi kungoja hapa kidunguni.
9Sasa tazameni! Panakuja kikosi cha watu
waliopanda farasi wakienda wawiliwawili!
Kisha akasema: Umeanguka! Umeanguka mji wa Babeli!
Navyo vinyago vyake vyote vya miungu yao
amevivunja na kuvitupa chini.
10Ninyi wenzangu mliopigwa,
kama mpunga unavyopigwa penye kuupuria,
niliyoyasikia kwa Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli,
nimewatangazia ninyi.
11Toka Seiri wananiita kwamba:
Mlinzi, saa ngapi sasa za usiku?
Mlinzi, saa ngapi sasa za usiku?
12Mlinzi akajibu: Ijapo mapema yaje,
usiku utakuwa ungalipo.
Kama mnataka kuuliza mengine, haya! Ulizeni!
13Sharti mlale kwenye mapori nyikani,
ninyi watembezi wa Dedani!
14Waliokufa kiu wapelekeeni maji,
ninyi mkaao katika nchi ya Tema!
Waliokimbia wagawieni vilaji vya kuwatunza!
15Kwani wamezikimbia panga,
zile panga walizochomolewa wao,
wamezikimbia nazo pindi, walizovutiwa,
hata uzito wote wa vita.
16Kwani ndivyo, Bwana alivyoniambia:
Ungaliko bado mwaka, kama miaka ya kibarua ilivyo,
ndipo, utukufu wote wa Kedari utakapokuwa umekwisha.
17Watakaosalia kwa wana wa Kedari walio wenye nguvu
katika hesabu yao ya wavuta pindi watakuwa wachache,
kwani Bwana Mungu wa Isiraeli amevisema.