The chat will start when you send the first message.
1Mmeona nini mkipanda wote vipaani?[#Yes. 15:3.]
2Wewe mji uliojaa makelele ya machafuko,
mliomo na wapiga vigelegele,
watu wako waliouawa hawakuuawa kwa panga,
wala hawakufa vitani.
3Wakuu wako wamekimbia wote pamoja,
wakatekwa pasipo upindi,
nao watu wako waliopatikana wametekwa wote,
nao waliokimbia mbali.
4Kwa hiyo nimesema: Msinitumbulie macho,
nilie kwa uchungu!
Wala msinibembeleze na kunituliza moyo
kwa ajili ya kuangamia kwao walio wazaliwa wa ukoo wangu!
5Kwani siku ya mastuko na ya maangamizo na ya machafuko
imetoka kwake Bwana Mungu Mwenye vikosi,
ikaja Bondeni kwenye Maono,
ni siku iliyobomoa maboma,
vilio vyake vikasikilika mlimani.
6Waelamu wameshika mapodo, wakapanda magari na farasi,
Wakiri nao wakazifunua ngao.
7Ndipo, mabonde yako mazuri yalipojaa magari,
nao wapanda farasi wakajisimamisha
upande wa lango la maji.
8Hivyo akayafunua, ambayo Wayuda walijifunika nayo,
siku ile wakayatazamia mata
yaliyowekwa katika nyumba ya mwituni.
9Mkapaona, mji wa Dawidi ulipobomokabomoka,
ya kuwa ni pengi,
mkayakusanya maji ya ziwa la chini.
10Mkazihesabu nazo nyumba za Yerusalemu,
mkabomoa nyingine, mpate ya kuujengajenga ukuta wa boma.
11Katikati ya kuta mbili za boma mkatengeneza mahali,
pawe pa kukusanyia maji ya ziwa la kale.
Lakini yeye aliyeyafanya mambo hayo hamkumtazama,
hamkumwona aliyeyalinganya, yalipokuwa yangaliko mbali.
12Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi aliwaita siku ile,
mlie na kuomboleza, mnyoe vichwa na kuvaa magunia.
13Kumbe mkacheza na kufurahi,
mkaua ng'ombe, mkachinja nao kondoo,
mkala nyama, mkanywa mvinyo, mkasema:
Na tule, na tunywe! Kwani kesho tutakufa!
14Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi ameyafumbua masikioni mwangu:
Mpaka mtakapokufa, hamtaondolewa kabisa
manza hizi, mlizozikora.
Ndivyo, anavyosema Bwana Mungu Mwenye vikosi.
15Ndivyo, anavyosema Bwana Mungu Mwenye vikosi:
Nenda, uje kwake huyo mtunza mali,
huyo Sebuna aliye mkuu wa nyumba ya mfalme.
16Unafanya nini hapa? Kuna nani wa kwenu huku?
Kumbe unajichimbia kaburi hapa!
Kweli unajichimbia hapa juu kaburi lako,
unajichongea magengeni kao lako!
17Tazama, Bwana atakutupa na kukubwaga kwa nguvu!
Wewe mtu wa kiume atakukunja kabisa.
18Atakuzinga, uviringane kama mpira,
akutupe katika nchi iliyopanuka pande mbili;
ndiko, utakakokufa,
ndiko, magari yako mazuri yatakakokufuata
wewe uliyeitweza Nyumba ya Bwana wako.
19Nitakutangua katika utunzaji wako,
nitakuondoa katika usimamizi wako.
20Siku ile ndipo, nitakapomwita
mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia.
21Nitamvika kanzu yako, nitamfunga nao mshipi wako,
utunzaji wako nitampa, uwe mkononi mwake,
atakuwa baba yao wakaao Yerusalemu,
hata baba yao walio wa mlango wa Yuda.
22Nitampa ufunguo wa nyumba ya Dawidi, uwe begani pake;
atakapofungua, hatakuwako awezaye kupafunga,
atakapofunga, hatakuwako awezaye kupafungua.
23Nitampigilia kama msumari mahali pagumu,
atauwia lango wa baba yake kiti chenye utukufu.
24Kwake utatundikwa utukufu wote wa mlango wa baba yake;
miche na machipukizi na vyombo vyote vidogo,
kuanzia vikombekombe kufikisha mitungitungi yote.
25Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi:
Msumari uliokuwa umepigiliwa mahali pagumu
siku ile uvunjike, utajipinda,
uanguke chini, nao mzigo ulioangikwa kwake utaanguka,
kwani Bwana amevisema.