Yesaya 23

Yesaya 23

Mapatilizo ya Tiro.

1Pigeni vilio, ninyi merikebu za Tarsisi!

Kwani mji wenu umetoweshwa, hamna nyumba wala kituo;

ndivyo, walivyoambiwa katika nchi ya Wakiti.

2Nyamazeni, ninyi mkaao pwani!

Wachuuzi wa Sidoni waliopita baharini waliwaletea yote.

3Kwenye maji mengi uliletewa yaliyopandwa Sihori

nayo yaliyovunwa mtoni kwa Nili,

ukawa mahali, mataifa yalipochuuzia.

4Ona soni, Sidoni! Kwani baharini kwenye ngome ya baharini wako

waliolia kwamba: Sikushikwa na uchungu, sikuzaa,

wala sikulea vijana, wala sikukuza wanawali.

5Wamisri watakapoyasikia, watashikwa na uchungu

kwa kuzisikia hizo habari za Tiro.

6Vukeni kuja Tarsisi! Pigeni vilio, mkaao pwani!

7Je? Huo ndio mji wenu uliopiga vigelegele?

uliojengwa siku za kale kabisa?

ulioiendesha miguu yenu,

mwende katika nchi za mbali kutua kulekule?

8Ni nani aliyeukatia Tiro shauri hili?

Ulikuwa umegawia wengine taji za kifalme,

wachuuzi wake walikuwa wakuu wa nchi,

nao waliokuwa wenye maduka

walitukuzwa kuliko wengine katika nchi.

9Bwana Mwenye vikosi ndiye aliyelikata shauri lake,

auchafue urembo wote, waliojivunia,

awanyenyekeze wote waliotukuka katika nchi.

10Furikieni katika nchi yenu kama mto wa Nili,

ninyi wana wa Tarsisi! Hakuna ukingo tena.

11Bwana ameikunjulia bahari mkono wake,

akazitetemesha nchi zenye wafalme,

akaagiza, miji ya Kanaani yenye maboma ibomolewe.

12Akasema: Hutashangilia tena, binti Sidoni,

kwa kuwa mwanamwali aliyetiwa soni.

Ondoka, uvuke kwenda kwao Wakiti!

Lakini nako kule hutapata kutulia.

13Itazameni nchi ya Wakasidi! Ndio watu wasiokuwa kabila;

kwa hiyo Waasuri walitaka kuigeuza nchi yao,

iwe kao la nyama wa porini.

Lakini sasa wanaisimamisha minara yao ya kulindia,

wakayabomoa majumba ya nchi hii

na kuyageuza kuwa mabomoko.

14Pigeni vilio, ninyi merikebu za Tarsisi!

Kwani mji wenu uliokuwa na nguvu umetoweshwa.

15Siku zile mji wa Tiro utakuwa umesahauliwa miaka 70, kama siku za mfalme mmoja zilivyo. Miaka 70 itakapokwisha, Tiro utapata yaliyoandikwa katika wimbo wa mwanamke mgoni ya kwamba:

16Chukua zeze, utembee mjini, wewe mwanamke mgoni uliyesahauliwa! Kalipige zeze vizuri, uliimbie nyimbo nyingi, ukumbukwe tena!

17Miaka 70 itakapokwisha, Bwana ataukagua mji wa Tiro, uyarudie mapato ya uasherati wake, ukiufuata ugoni katika nchi zote zenye wafalme zilizoko ulimwenguni.

18Lakini mapato yake ya uchuuzi na ya uasherati yatakuwa mali za Bwana, hazitalimbikwa, wala hazitawekwa za akiba, ila atakayoyapata kwa uchuuzi wake, watagawiwa wakaao machoni pa Bwana, wapate kula na kushiba, tena wapate kuvaa na kujifunika vema.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania