Yesaya 24

Yesaya 24

Mapatilizo ya dunia yote nzima.

1Tazameni, Bwana anaondoa watu katika nchi, iwe peke yake!

Anaiumbua umbo lake na kuwatawanya wanaokaa huku.

2Wote watakuwa sawa: watu na mtambikaji,

mtumwa na mabwana wake, kijakazi na bibi yake,

anunuaye na auzaye, akopeshaye na akopaye,

mwenye kudai na mwenye kudaiwa.

3Kweli nchi itaondolewa watu kabisa,

nazo mali zitapokonywa,

kwani Bwana amelisema neno hilo.

4Nchi imesikitika, maana imenyauka,

ulimwengu wote umefifia, maana umenyauka,

nao walio wakuu wa watu katika nchi wamefifia.

5Chini yao wakaao huku nchi imechafuliwa,

kwani wameyapita Maonyo, hawakuyafuata maongozi,

wakalivunja Agano la kale na kale.

6Kwa sababu hii apizo limeila nchi;

nao wakaao huku wanalipishwa manza, walizozikora;

kwa sababu hii waikaao nchi wameunguzwa,

watu waliosalia ni wachache tu.

7Mvinyo mbichi zimesikitika, mizabibu imefifia,

wote waliokuwa na furaha mioyoni hupiga kite.

8Patu zilizofurahisha hunyamaza,

makelele yao wapigao vigelegele yamekoma,

nayo mazeze yaliyofurahisha hunyamaza.

9Hawanywi tena mvinyo na kuiimbia,

kileo cha sasa ni chenye uchungu kwao wanaokinywa.

10Mji umebomolewa, uko peke yake tu,

kila nyumba imefungwa, hakuna anayekuja.

11Makelele ya kulilia mvinyo yanasikilika huko nje,

furaha yote imeguiwa na giza,

maana yote yaliyoifurahisha nchi yamehama.

12Yaliosalia mjini ni mahame tu,

nalo lango lake limevunjwavunjwa kuwa vipandepande tu.

13Kwani hivyo ndivyo, mambo yatakavyokuwa

katika nchi katikati ya watu,

kama yalivyo penye mavuno ya matunda ya mchekele

au penye kuokoteza, mavuno ya zabibu yakiisha.

14Hawa wanapaza sauti zao kwa kupiga vigelegele

wakiushangilia utukufu wa Bwana kuanzia baharini.

15Kwa hiyo mtukuzeni Bwana nako maawioni kwa jua,

nako kwenye visiwa vilivyoko baharini

litukuzeni Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli!

16Toka mapeoni kwa nchi tulisikia nyimbo kwamba:

Mwongofu na apambwe!

Nikajibu kwamba: Ni mnyonge! Ni mnyonge! Nimekufa!

Wakorofi wanakorofisha,

kweli wakorofi wanakorofisha kwa ukorofi.

17Mastuko na miina na matanzi yanawangoja

ninyi mkaao katika nchi!

18Itakuwa hivi:

Atakayeyakimbia makelele ya kustusha ataanguka mwinani,

naye atakayepanda na kutoka mwinani atanaswa na tanzi,

kwani madirisha ya huko juu yatakuwa yamefunguliwa,

nayo misingi ya nchi itatetemeka.

19Nchi itavunjikavunjika,

nchi itaatukaatuka, nchi itayumbayumba.

20Nchi itapepesukapepesuka kama mlevi,

itachukuliwa huko na huko kama machela,

italemewa na mapotovu yake,

itaanguka, isiweze kuinuka tena.

Utukufu wa Mungu utakaotokea Sioni.

21Siku ile itakuwa hivi:

Bwana atavijilia vikosi vya juu huko juu,

nao wafalme wa nchi atawajilia huku chini.

22Watakusanywa, kama wafungwa wanavyokusanywa,

wapelekwe shimoni, wafungwe kifungoni,

tena wafunguliwe, siku nyingi zitakapopita.

23Hapo ndipo, mwezi utakapojifunika,

ndipo, nalo jua litakapoona soni,

kwa kuwa Bwana Mwenye vikosi atakuwa yuko mfalme

mlimani kwa Sioni namo Yerusalemu,

nako mbele ya wazee wake utakuwako utukufu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania