Yesaya 27

Yesaya 27

Mapatilizo ya wakuu wa ulimwengu.

1Siku ile Bwana atatokea akishika upanga

ulio mgumu na mkubwa na wenye nguvu,

amlipishe Lewiatani, ni lile joka limkimbialo;

yeye Lewiatani, lile joka la kujizinga kabisa,

atamwua pamoja na yule nondo alioko baharini.

2Siku ile watasema: Mzabibu mzuri! Uimbieni![#Yes. 5:1.]

3Mimi Bwana ni mlinzi wake; mara kwa mara ninaunywesha;

kusudi mtu asiuharibu, ninaulinda usiku na mchana.

4Ukali sinao tena; kama ningeona mikunju na mibigili,

ningeipelekea vita mara moja, niichome moto yote pamoja;

5nao watanishika, niwalinde kwa nguvu zangu,

wataniomba, watulie kwangu,

kweli wataniomba, watulie kwangu.

6Siku zitakazokuja Yakobo atatia mizizi,

Isiraeli atachanua na kuzaa matunda,

waueneze ulimwengu wote hayo matunda.

7Je? Amewapiga, kama alivyowapiga waliowapiga?

Au wameuawa, kama walivyouawa waliowaua?

8Amewagombeza tu na kuwafukuza na kuwatuma, wajiendee,

akawakimbiza kwa upepo mgumu siku za kimbunga

kilichotoka maawioni kwa jua.

9Hivyo manza zao, wa Yakobo walizozikora,

zimefunikwa kweli,

nalo hili ndilo pato la kuwaondolea makosa yao:

mawe yote ya mahali pa kutambikia miungu wameyaponda

kuwa mavumbi kama ya mawe ya chokaa yaliyobunguliwa,

nayo mifano ya mwezi na ya jua haikusimikwa tena.

10Kwani mji uliokuwa wenye nguvu peke yake tu,

ni mahame tu pasipo watu; yalipoachwa, pakawa nyika:

ng'ombe wanalisha huko,

wanapumzika huko na kuvimaliza vijiti vyake.

11Matawi yao yakiisha kukauka, huvunjwa;

wanawake wanakuja, wanayatumia kuwa kuni,

kwani sio watu wanaotambua maana.

Kwa hiyo yeye aliyewafanya hawahurumii,

muumba wao hawaonei uchungu.

12Siku ile Bwana atayapura masuke yote,

kuanzia kwenye lile jito kubwa kufikisha mpaka mtoni kwa Misri.

Nanyi wana wa Isiraeli, mtakusanywa mmoja kwa mmoja.

13Tena siku ile, baragumu kubwa litakapopigwa,

ndipo, wote waliopotelea katika nchi ya Asuri

watakapokuja pamoja nao waliotawanyika katika nchi ya Misri,

wamtambikie Bwana kwenye mlima mtakatifu wa Yerusalemu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania