Yesaya 28

Yesaya 28

Mapatilizo ya Efuraimu.

1Yatakupata wewe,

uliye kilemba chenye majivuno ya walevi wa Efuraimu!

Uliye hata sasa urembo wenye utukufu,

utakuwa kama ua lililonyauka,

kwa maana umejengwa kilimani juu

kwenye bonde lioteshalo sana,

likaalo watu waangushwao na mvinyo.

2Tazameni! Mwenye nguvu na ukorofi yuko tayari kwa Bwana,

anafanana na mvua ya mawe

inayokuja na upepo unaovunjavunja,

ni mvua inyeshayo maji mengi yenye nguvu

ya kufurikia nchini,

nayo yatawabwaga chini na kuwadidimiza

kwa kuwavuta kwa nguvu zilizo kama za mkono.

3Kisha utakanyagwa na miguu,

wewe uliye kilemba chenye majivuno ya Efuraimu.

4Lile ua litakalonyauka lingaliko,

nao urembo wenye utukufu wake linao,

kwa maana liko kilimani juu

kwenye bonde lioteshalo sana,

lakini litakuwa kama kuyu inayoiva upesi,

siku za mavuno zinapokuwa hazijatimia bado;

mtu akiiona anaichuma hapohapo,

tena ikiwa ingalimo mkononi mwake, amekwisha kuimeza.

5Siku ile Bwana Mwenye vikosi

atakuwa kilemba chenye urembo

na pambo la kipajini lenye utukufu

kwao waliosalia wa ukoo wake.

6Naye atakayekaa kitini penye uamuzi

atampa roho yenye unyofu

nao wapiga vita watakaowakimbiza adui malangoni

atawapa nguvu za kushinda.

Mapatilizo ya Yuda.

7Kumbe hao nao wanapepesuka kwa mvinyo

na kuyumbayumba kwa vileo!

Watambikaji na wafumbuaji wanapepesuka kwa vileo:

wameshikwa na kizunguzungu kwa kunywa mvinyo,

wanayumbayumba kwa vileo,

wanapepesuka wakifumbua, wanatukutika wakiamua.

8Kwani meza zote zimejaa matapiko,

hakuna mahali pasipo machafu.

9Nao husema: Yuko nani, Bwana atakayemfundisha kujua maana?

Yuko nani, atakayemtambulisha waliyoyasikia?

Ni wao waliozoezwa, waache kunyonya,

walioondolewa sasa hivi kwenye maziwa ya wamama?

10Agizo hufuata agizo, kweli agizo hufuata agizo;

kingojeo huita kingojeo, kweli kingojeo huita kingojeo

kwamba: Hapa bado kidogo napo hapo bado kidogo!

11Ni kweli, midomo, watu wasiyoitambua,

nazo ndimi zilizo ngeni kwao

ndizo, atakazozitumia atakaposema nao walio wa ukoo huu.

12Maana aliwaambia: Hapo ni penye kupumzikia,

waacheni wachovu, wapumzike!

Hapa ni penye kutulia! Lakini hawakutaka kusikia.

13Kwa hiyo lile neno lao litakuwa kwao neno la Bwana:

Agizo hufuata agizo, kweli agizo hufuata agizo,

kingojeo huita kingojeo, kweli kingojeo huita kingojeo

kwamba: Hapa bado kidogo napo hapo bado kidogo!

Kusudi waende na kujikwaa na kuanguka kichalichali,

wapondeke, wanaswe, watekwe.

14Kwa hiyo lisikieni neno la Bwana, ninyi waume mfyozao,

nanyi mnaowatawala wa Yerusalemu walio wa ukoo huu!

15Kwani mlisema: Tumekwisha kuagana na kufa,

nako kuzimu tumekwisha kupatana nako kwamba:

Pigo la kudidimiza litakapokutia, lisitufikie!

Kwani uwongo tumeutumia kuwa kimbilio letu,

tukajificha kwenye madanganyifu.

Jiwe la pembeni.

16Lakini hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema:

Nitazameni! Mimi ndimi niliyeweka jiwe,

liwe msingi wa Sioni,

nalo ni jiwe lililojulika,

ya kuwa litafaa la pembeni kwa utukufu wake,

likawekwa la msingi

kuwa kama mwamba,

ni hili la kwamba:

Alitegemeaye hatakimbia.

17Nayo yaliyo sawa nikayatumia kuwa kamba ya kupimia,

nayo yaongokayo kuwa kipimo chenyewe,

mvua ya mawe italiondoa kimbilio lenu la uwongo,

nalo ficho lenu maji yatalididimiza.

18Nayo mliyoyaagana na kufa yatatanguliwa,

yasisimamike mliyoyapatana na kuzimu;

pigo la kudidimiza litakapotukia,

ndipo, watakapopokonywa nalo.

19Kila mara litakapopita litawashika,

kila kunapokucha litapita, hata mchana na usiku;

nako kustushwa ndiko peke yake

kutakakowatambulisha mliyoyasikia.

20Kwani: Kitanda kifupi, hutaweza kujinyosha;

nalo: Blanketi dogo, hutaweza kujifunika.

21Kwani Bwana atainuka kama kwenye mlima wa Perasimu,

achafuke kama kule bondeni karibu ya Gibeoni,

aifanye kazi yake, nayo hiyo kazi yake ni ngeni,

atumike katika matumishi yake,

nayo hayo matumishi yake hayajasikiwa bado.

22Sasa acheni kufyoza, vifungo vyenu visikazwe,

kwani nchi zote zimekwisha kukatiwa shauri la angamizo,

kama nilivyosikia kwa Bwana Mungu aliye Mwenye vikosi.

Bwana huyatengeneza yote vizuri.

23Sikilizeni, mwisikie sauti yangu!

Angalieni, mlisikie neno langu!

24Inakuwaje? Mlima hulima siku zote, apate kumwaga mbegu?

Au huponda siku zote madongo na kupalinganya?

25Au sivyo: alipokwisha kuusawasawisha mchanga wa juu,

humwaga mbegu za maboga na za pilipili, nazo huzitupatupa,

kisha hupanda nazo ngano nzuri mistarimistari,

hata mtama na mahindi, nao uwele kandokando?

26Hivyo Mungu wake alimfundisha yafaayo na kumwonyesha.

27Kwani mbegu za maboga hazipurwi kwa magogo,

mbegu za pilipili hazipitwi juu na magurudumu ya magari,

ila mbegu za maboga zinafikichwa kwa vijiti,

pilipili vilevile zinapigwapigwa kwa fimbo.

28Je? Ngano zinapondwa? Hapana, hawazipuri pasipo kukoma;

hata wakipitisha magari na farasi wao, hawazipondi.

29Hayo nayo yalitoka kwake Bwana Mwenye vikosi,

mizungu yake hustaajabisha,

utambuzi wake ni mkuu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania