Yesaya 3

Yesaya 3

Wakuu wabaya wataondolewa.

1Mtaona, Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi

akiondoa katika Yerusalemu na katika Yuda

yote yatumikayo kuwa shikizo:

kila shikizo la vilaji na kila shikizo la maji;

2wenye nguvu nao wajuao kazi za vita,

waamuzi na wafumbuaji, waaguaji na wazee,

3wakuu wa askari na wenye macheo makubwa,

wakata mashauri na mafundi wa kazi na mafundi wa uganga.

4Kisha nitawapa vijana, wawe wakuu wao,

nao wenye ukorofi watawatawala;

5nao wenyewe watatesana waume na waume wenzao,

kila mtu na ndugu yake,

vijana watajivuna na kuwabeza wazee,

nao wanyonge watawabeza wenye utukufu.

6Hapo itakuwa, mtu amkamate ndugu yake,

ambaye alizaliwa naye nyumbani mwa baba yake,

amwambie: Unazo nguo bado, sharti uwe mwamuzi wetu!

Hame hili liwe mkononi mwako!

7Naye atajibu siku ileile na kupaza sauti: Mimi si mganga!

Humu nyumbani mwangu hamna mkate wala nguo,

msiniweke kuwa mwamuzi wenu!

8Kwani Yerusalemu utakuwa umejikwaa,

nayo Yuda itakuwa imeanguka,

kwa kuwa ndimi zao na kazi zao zilimpinga Bwana

na kuyachafua macho yake yenye utukufu,

9ukorofi wa nyuso zao ukawaumbua,

nao huyasimulia makosa yao pasipo kuyaficha

kwa hivyo, wanavyofanana nao Wasodomu.

Roho zao zitalipizwa vibaya,

walivyojifanyizia wenyewe.

10Yawazeni, ya kuwa waongofu huona mema,

kwani huyala mapato ya kazi zao!

11Lakini wasiomcha Mungu huona mabaya,

kwani mikono yao iliyoyafanya, watafanyiziwa nao.

12Wanaowasonga walio ukoo wangu ni watoto,

nao wanawake ndio wanaowatawala.

Ninyi mlio ukoo wangu, viongozi wenu huwapoteza,

nazo njia zenu zilizowapasa kuzishika huzifisha.

13Bwana ameinuka kupigana,

Bwana amesimama kuyapatiliza makabila ya watu.

14Bwana atakuja kuwahukumu wazee na wakuu wao walio ukoo wake,

kwamba: Ninyi mmeilisha mizabibu yangu!

Mliyoyanyang'anya wanyonge, yamo nyumbani mwenu.

15Imekuwaje, mkiwaponda hivyo walio ukoo wangu?

Mkizirarua nyuso za wanyonge hivyo?

Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi.

Nao wanawake wabaya watapatilizwa.

16Bwana amesema: Kwa kuwa wanawake wa Sioni wamejikuza,

wakatembea na kunyosha shingo

na kutupia wengine macho yenye utongozi,

wakienda na kuchezacheza

na kuipigapiga mikufu ya miguu yao:

17Bwana atawauguza wanawali wa Sioni upele wa vichwani,

yeye Bwana atawavua nazo nguo za kujifunika shungi.

18Siku ile Bwana atayaondoa mapambo kwao:

vikuku na mifano ya jua vipajini nayo manyamwezi shingoni,

19mapete masikioni na mikufu mikononi na mabuibui nyusoni;

20hata miharuma vichwani na mikufu miguuni na mikanda viunoni

na vichupa vya marashi vifuani na hirizi zote miilini po pote,

21nazo pete vidoleni na vipini puani,

22tena nguo za sikukuu, kama marinda na kanga na vijamanda,

23hata vioo na fulana za hariri na vilemba na kaya.

24Hivyo penye manukato mazuri utakuwa mnuko wa kuoza,

penye mikanda watapata kamba tu,

penye misuko ya nywele patakuwa na vipara,

penye zile nguo za urembo watajivika magunia,

maumbufu matupu yatapashika mahali pa uzuri.

25Waume wenu watauana kwa panga,

vijana wenu wenye nguvu watamalizika vitani.

26Kwa hiyo malango yake yatapiga kite kwa kusikitika,

nao wenyewe watakaa uvumbini kwa kuwa peke yao tu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania