Yesaya 31

Yesaya 31

Wamisri hawaokoi, ila Bwana peke yake.

1Yatawapata washukao kwenda Misri kutafuta msaada,

wakijishikiza kwa farasi,

wakaegemea magari, kwamba ni mengi,

hata wapanda farasi, kwamba ni wenye nguvu sana,

lakini hawakumtazamia Mtakatifu wa Isiraeli,

Bwana hawakumtafuta.

2Naye ni mwenye werevu wa kweli; kwa hiyo analeta kibaya,

nayo maneno yake hayaondoi:

nyumba zao wafanyao mabaya ataziinukia,

vilevile msaada wao wafanyao maovu.

3Misri ndio watu tu, sio Mungu;

farasi wao ndio nyama, sio roho.

Bwana akiukunjua mkono wake,

ndipo, huyo mwenye kusaidia anapojikwaa,

ndipo, naye mwenye kusaidiwa anapoanguka,

wakaanguka wote pamoja.

4Kwani hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia:

Itakuwa kama simba au mwana wa simba,

akikamata kondoo na kunguruma;

kisha wachungaji wakiitana wengi, wamnyang'anye,

hazistukii sauti zao, wala hatishiki kwa makelele yao;

ndivyo, Bwana Mwenye vikosi atakavyoshuka kupiga vita,

mlimani kwa Sioni nako kwenye kilima chake.

5Bwana Mwenye vikosi ataukingia Yerusalemu

kama ndege warukao,

kwa kukinga atawaponya, kwa kuwapita atawakomboa.

6Rudini kwake yeye, mliyemwacha kabisa,

ninyi wana wa Isiraeli!

7Kwani siku ile kila mtu atavikataa

vinyago vyake vya fedha na vinyago vyake vya dhahabu,

mlivyojitengenezea kwa mikono yenu, vikawakosesha.

8Ndipo, Waasuri watakapouawa kwa panga zisizo za waume,

kweli panga zitawala, lakini sizo za watu;

hizo panga watazikimbia,

nao vijana wao watakuwa watumwa.

9Naye aliyekuwa mwamba wao atakimbia kwa woga,

nao walio wakuu wao watazimia kwa kuona bendera.

Ndivyo, asemavyo Bwana alioko Sioni na moto wake

alioko na jiko lake huko Yerusalemu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania