The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwaka wa 14 wa mfalme Hizikia, ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoipandia miji yote ya Wayuda iliyokuwa na maboma, akaiteka.
2Kisha mfalme wa Asuri akamtuma mkuu wa askari, atoke Lakisi kwenda Yerusalemu na kikosi kikubwa kwake mfalme Hizikia. Akaja kusimama kwenye mfereji wa ziwa la juu katika barabara iendayo Shambani kwa Dobi.
3Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa wakamtokea.[#Yes. 22:20.]
4Mkuu wa askari akawaambia: Mwambieni Hizikia: Hivi ndivyo, mfalme mkuu, mfalme wa Asuri, anavyosema: Hilo egemeo, unaloliegemea, ndio nini?[#Yes. 36:13.]
5Nasema: Ni maneno ya midomo tu, ukisema: Nimekata shauri na kujipa moyo wa kupiga vita. Sasa unamwegemea nani, ukinikataa na kuacha kunitii?
6Tazama! Egemeo lako, unaloliegemea, ni Misri, hilo fimbo la utete unyongekao! Mtu akilikongojea, litamwingia kiganjani, limchome. Ndivyo, Farao, mfalme wa Misri, anavyowawia wote waliomwegemea.
7Ukiniambia: Tunamwegemea Bwana Mungu wetu, basi, yeye siye, ambaye Hizikia aliwakataza watu kumtambikia vilimani pake napo penye meza zake za kutambikia, alipowaambia Wayuda na Wayerusalemu: Sharti mmwangukie mbele ya meza hii tu ya kumtambikia?
8Sasa na upinge na bwana wangu, mfalme wa Asuri: Nitakupa farasi 2000, kama wewe unaweza kujipatia watu wa kuwapanda.
9Usipowapata utawezaje kuuelekeza nyuma uso wa mwenye amri mmoja tu, ijapo awe mdogo katika watumishi wa bwana wangu? Tena unawaegemea Wamisri, kwa kuwa wako na magari na wapanda farasi.
10Bwana alikuwa hayuko, nilipoipandia sasa nchi hii, niiangamize? Bwana ndiye aliyeniambia: Ipandie nchi hii, uiangamize!
11Ndipo, Eliakimu na Sebuna na Yoa walipomwambia mkuu wa askari: Sema Kishami na watumishi wako! Kwani tunakisikia; usiseme na sisi Kiyuda masikioni pa watu hawa walioko ukutani!
12Mkuu wa askari akawajibu: Je? Bwana wangu amenituma kwa bwana wako na kwako kuyasema haya maneno? Sio kwa watu hawa wanaokaa ukutani watakaokula pamoja nanyi mavi yao na kunywa mikojo yao?
13Kisha mkuu wa askari akatokea, akapaza sauti sana na kusema Kiyuda kwamba: Yasikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Asuri![#Yes. 36:4.]
14Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Hizikia asiwadanganye! Kwani hataweza kuwaponya ninyi.
15Wala Hizikia asiwaegemeze Bwana kwamba: Bwana ndiye atakayetuponya, mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Asuri.
16Msimwitikie Hizikia! Kwani hivi ndivyo, mfalme wa Asuri anavyosema: Fanyeni na mimi maagano ya mbaraka, mje kunitokea, mpate kula kila mtu mazao ya mzabibu wake na ya mkuyu wake, mpate kunywa kila mtu maji ya shimo lake mwenyewe,[#1 Fal. 4:25; Mika 4:4.]
17mpaka nitakapokuja, miwachukue kuwapeleka katika nchi iliyo kama nchi yenu. Nayo ni nchi inayojaa ngano na pombe, ni nchi yenye vyakula na mizabibu.
18Hizikia asiwapoteze na kusema: Bwana atatuponya! Je? Miungu ya wamizimu iliweza mmoja tu kuiponya nchi yake, isichukuliwe na mfalme wa Asuri?[#Yes. 10:10; 37:12.]
19Ilikuwa wapi miungu ya Hamati na ya Arpadi? Ilikuwa wapi miungu ya Sefarwaimu? Hata Samaria haikuweza kuiponya, nisiichukue!
20Katika miungu yote ya nchi hizi ni ipi iliyoweza kuziponya nchi zao, nisizichukue? Basi, Bwana atawezaje kuuponya Yerusalemu, nisiuchukue?
21Wakanyamaza, hawakumjibu neno, kwani mfalme alikuwa amewaagiza kwamba: Msimjibu!
22Kisha Eliakimu, mwana wa Hilikia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa wakaja kwa Hizikia wenye nguo zilizoraluliwa, wakamsimulia maneno ya mkuu wa askari.