Yesaya 41

Yesaya 41

Mungu anamwita mtumishi wake kuwatuliza wakiwa mioyo na kuwatia wamizimu soni.

1Ninyi visiwa, nyamazeni mbele yangu!

nayo makabila ya watu na yajipatie nguvu mpya,

watu na wakaribie, kisha waseme!

Sote pamoja na tuje kushindana shaurini!

2Yuko nani aliyeamsha mtu maawioni kwa jua?

Naye huyo mtu ndiye, aliyemwita mwongofu,

akampatia pa kuiwekea miguu yake.

Yuko nani aliyemtolea huyu mataifa,

awakanyage wafalme wao,

upanga wake uwaponde, wawe kama mavumbi,

nao upindi wake uwatawanye kama makapi yapeperushwayo?

3Anapowakimbiza mwenyewe hupita salama.

ijapo miguu yake isije kushika njia ya watu.

4Yuko nani aliyevitengeneza na kuvifanya?

Yuko nani aliyeviita vizazi toka mwanzo?

Ni mimi Bwana niliye wa mwanzo na wa mwisho, mimi ndiye.

5Visiwa vimeyaona, vikaogopa,

mapeo ya nchi yakatetemeka:

Wanakuja! Wamekwisha kufika karibu!

6Wakasaidiana kila mtu na mwenziwe,

wakaambiana mtu na ndugu yake: Kaza nguvu!

7Mafundi wa vinyago wakawashupaza wafua dhahabu,

nao wenye kuteleza dhahabu kwa nyundo ndogo

wakawashupaza wapiga fuawe

wakisema: Tindikali ni njema,

kisha wakavipigilia misumari, visitikisike.

8Nawe Isiraeli uliye mtumishi wangu,

nawe Yakobo, niliyekuchagua,

ndiwe uzao wa mpenzi wangu Aburahamu.

9Nilikushika, nikakutoa kwenye mapeo ya nchi,

nikakuita pembeni kwake, nikakuambia:

Wewe u mtumishi wangu, nimekuchagua, sijakukataa.

10Usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe!

Usitupe macho po pote! Kwani mimi ndimi Mungu wako,

ninakutia nguvu, ninakusaidia,

ninakushikiza kwa mkono wangu wa kuume,

nao huyanyosha yaliyopotoka.

11Tazama! Wote waliokutolea ukali

watapatwa na soni, watamalizika,

watakuwa, kama si kitu;

nao waliotaka kukushinda wataangamia.

12Utawatafuta, usiwaone waliokupingia,

waliopigana na wewe watakuwa kama si kitu chenye maana.

13Kwani mimi Bwana ndimi Mungu wako,

ninaushupaza mkono wako wa kuume,

ninakuambia: Usiogope! Mimi ninakusaidia!

14Usiogope, wewe Yakobo uliye kidudu,

nawe Isiraeli uliye kikosi kidogo! Mimi ninakusaidia!

Ndivyo, asemavyo Bwana aliyekukomboa,

aliye Mtakatifu wa Isiraeli.

15Tazama! Nimekuweka kuwa gari jipya la kupuria

lililo lenye meno makali,

uiponde milima na kuibungua,

vilima navyo uvifanye kuwa kama makapi.

16Utaipepeta, nao upepo utaichukua,

nacho kimbunga kitaitawanya;

nawe utampigia Bwana vigelegele,

utamshangilia Mtakatifu wa Isiraeli.

17Wanyonge na wakiwa wako katika kutafuta maji,

lakini kwa kuwa hayako, ndimi zao zimekauka kwa kiu,

lakini mimi Bwana nitawaitikia,

mimi Mungu wa Isiraeli sitawaacha.

18Nitatoa majito kwenye vilima vikavu,

namo mabondeni katikati nitatoa chemchemi,

nyika nitaigeuza kuwa ziwa la maji,

namo jangwani maji yataonekana.

19Nitaotesha nyikani miangati na migunga

na vihagilo na mibono;

huko nyikani nitaweka mivinje

na mitamba na mizambarau,

20kusudi wapate kuyaona na kuyatambua,

wayaweke mioyoni na kujifundisha wote pamoja,

ya kuwa mkono wa Bwana umeyafanya hayo,

ya kuwa Mtakatifu wa Isiraeli ameyaumba.

21Yaleteni mabishano yenu! ndivyo, Bwana anavyosema;

yafikisheni mambo yenu magumu!

ndivyo, mfalme wa Yakobo anavyosema.

22Yafikisheni na kutusimulia yatakayokuwa!

Yale ya mbele tuelezeeni maana yao, tuyaweke mioyoni,

tupate kuyatambua nayo ya nyuma! Nayo yajayo tuambieni!

23Yatangazeni yatakayokuja nyuma,

tujue, ya kuwa ninyi m miungu!

Fanyizeni tu mambo yakiwa mema au mabaya,

tuyastaajabu tutakapoyaona!

24Tazameni! Ninyi m wa bure,

nazo kazi zenu huwa si kitu,

anayewachagua ninyi hutapisha.

25Mimi nimeamsha mtu upande wa kaskazini, akaja;

nimemtoa maawioni kwa jua

atakayelitambikia Jina langu.

Akawajia wakuu na kuwawazia kuwa mchanga,

awaponde, kama mfinyanzi anavyoponda udongo.

26Yuko nani aliyeyaagua tangu mwanzo, tukayajua?

Yuko nani aliyeyasema kale,

tukayaitikia kwamba: Amesema kweli?

Lakini hakuna aliyeyaagua,

kweli hakuna aliyeyatangaza,

wala hakuna aliyeyasikia maneno yenu.

27Wa kwanza mimi nimeuambia Sioni: Yatazameni! Yako!

Namo Yerusalemu nimetuma mjumbe, apige mbiu njema.

28Lakini nilipotazama, hakuwako mtu;

nako kwao hao hakuwako wa kunipa shauri,

nikimwuliza, anipe majibu.

29Tazameni! Wote pamoja ni wa bure,

nazo kazi zao huwa si kitu,

vinyago vyao ni upepo mtupu pasipo maana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania