Yesaya 43

Yesaya 43

Mungu anawaokoa walio ukoo wake.

1Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyekuumba, Yakobo,

aliyekutengeneza, Isiraeli:

Sasa usiogope! Kwani nimekukomboa,

nimekuita kwa jina lako, ndiwe wangu!

2Utakapopita majini, mimi niko pamoja na wewe;

utakapopita katika majito, hayatakutosa;

utakapopita motoni hutachomwa,

wala ndimi za moto hazitakuunguza.

3Kwani mimi Bwana Mungu wako, Mtakatifu wa Isiraeli,

mimi mwokozi wako,

nimetoa Misri kuwa makombozi yako,

nikatoa Nubi na Seba mahali pako.

4Kwa kuwa uliwaziwa machoni pangu kuwa mali,

umepata utukufu, nikakupenda.

Kwa hiyo nimetoa watu, nikukomboe,

hata makabila mazima, niikomboe roho yako.

5Usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe;

walio uzao wako nitawaleta na kuwatoa maawioni kwa jua,

nitawakusanya na kuwatoa nako machweoni kwa jua.

6Nitauambia upepo wa kaskazini: Watoe!

nao upepo wa kusini: Usiwazuie!

Walete wanangu wa kiume na kuwatoa mbali

nao wanangu wa kike na kuwatoa mapeoni kwa nchi,

7wao wote waitwao kwa Jina langu!

Ndio, niliowaumba, nijipatie utukufu,

ndio, niliowatengeneza na kuwafanya.

8Watokezeni watu walio vipofu! Tena macho wanayo.

Nao walio viziwi! Tena masikio wanayo.

9Wamizimu wote na wakusanyike pamoja,

makabila ya watu na yakutane;

kwao yuko nani aliyetangaza kama hayo?

Yuko nani aliyetuambia yale ya mbele?

Na watoe mashahidi, wapate kushinda shaurini,

watu wayasikie, kisha waseme: Ni kweli!

10Ninyi m mashahidi wangu! ndivyo, asemavyo Bwana,

u mtumishi wangu, niliyekuchagua kwamba:

Mjue, mpate kunitegemea, tena mtambue, ya kuwa mimi ndiye!

Mbele yangu hakufanyika Mungu,

hata nyuma yangu hatakuwa.

11Mimi ndimi Bwana, pasipo mimi hakuna mwokozi.[#Yes. 44:6; 5 Mose 32:39.]

12Mimi nimeyatangaza, nikatengeneza wokovu,

nikaujulisha, mkingali hamna mungu mgeni kwenu;

nanyi m mashahidi wangu, nami ndimi Mungu!

ndivyo, asemavyo Bwana.

13Tena tangu leo nitakuwa yeye niliyekuwa,

hakuna aopoaye mkononi mwangu;

nikitaka kufanya kitu, yuko nani atakayekizuia?

14Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mkombozi wenu,

aliye Mtakatifu wa Isiraeli:

Kwa ajili yenu nilituma watu kwenda Babeli,

niwakimbize wote pia, washuke mtoni,

nao Wakasidi na wakimbie katika vyombo vyao,

walivyovipigia shangwe.

15Mimi Bwana ndimi Mtakatifu wenu,

mimi niliyemwumba Isiraeli ndimi mfalme wenu.

16Hivi ndivyo, anavyosema Bwana awekaye njia baharini,

hata mapito katika maji yenye nguvu,

17atokezaye magari na farasi, vikosi na wakuu pamoja:

Mara wataanguka, wasiinuke tena,

watazimia, kama utambi unavyozimika.

18Msiyakumbuke yaliyoko mbele,

wala msiyatambue yaliyopita kale!

19Tazameni! Ninafanya mapya, nayo yameanza kuchipuka!

Nanyi hamjayaona bado?

Hata nyikani ninatoa njia, nako jangwani majito.

20Nyama wa porini watanitukuza, mbwa wa mwitu na mbuni,

kwa kuwa nimetoa maji nyikani na majito jangwani,

niwanyweshe wao, niliowachagua, wawe ukoo wangu.

21Hao watu, niliojitengenezea, watayasimulia na kushangilia.[#1 Petr. 2:9.]

22Nawe Yakobo, hukuniita mimi,

nawe Isiraeli, hukujichokesha kwa ajili yangu.

23Hukuniletea wana kondoo wako kuwa wa kunitambikia,

wala hukuniheshimu na kunitolea vipaji vya tambiko.

Nami sikukusumbua, unipatie matunzo,

wala sikukuchokesha na kutaka uvumba kwako.

24Hukuninunulia vipande vya kichiri na kutoa fedha zako,

wala hukuninywesha mafuta ya ng'ombe zako za tambiko.

Ila ulinisumbua kwa makosa yako,

ukanichokesha kwa manza zako, ulizozikora.

25Mimi ninayafuta mapotovu yako

kwa ajili yangu mimi,

nayo makosa yako sitayakumbuka tena.

26Nikumbushe, tubishane!

Nawe yaseme yako, upate kushinda humu shaurini!

27Baba yako wa kwanza alikosa naye,

nao wasemaji wako walinitengua.

28Ndipo, nilipowatia mwiko wakuu wa Patakatifu,

nikamtoa Yakobo kuwa wa kuapizwa

naye Isiraeli kuwa wa kufyozwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania