Yesaya 45

Yesaya 45

Mfalme Kiro ni chombo cha Bwana.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyomwambia Kiro, aliyempaka mafuta:

Nimemshika mkono wake wa kuume,

nikanyage mbele yake mataifa mazima,

nikafungua mishipi viunoni kwa wafalme,

nikafungua mbele yake milango na malango,

yasifungike tena.

2Mimi nitakwenda mbele yako, nipalinganye pasipopitika,

nivunje milango ya shaba, nikate makomeo ya chuma.

3Nitakupa malimbiko yaliyomo gizani

nazo tunu zilizofichwa,

kusudi upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana,

Mungu wa Isiraeli ndiye aliyekuita kwa jina lako.

4Ni kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo

na kwa ajili ya mteule wangu Isiraeli,

nikikuita kwa jina lako na kukupa jina la macheo,

nawe ulikuwa hukunijua.

5Mimi ni Bwana, hakuna mwingine tena;

pasipo mimi hakuna Mungu;

nimekuvika, nawe ulikuwa hukunijua.

6Kwani walioko maawioni nao walioko machweoni kwa jua

ninawataka wote, wajue,

ya kuwa hakuna aliye Mungu, isipokuwa mimi,

mimi ni Bwana, hakuna mwingine tena.

7Natengeneza mwanga, naumba giza nayo,

nafanya utengemano, naumba ubaya nao,

mimi Bwana ndiye ayafanyaye hayo yote.

8Ninyi mbingu, nyesheni huko juu,

nanyi mawingu umimineni wongofu,

nchi ifunguliwe, ijae wokovu, ioteshe wongofu nao;

mimi Bwana ndiye aliyeiumba.

9Yatampata ambishiaye mfinyanzi wake,

naye ni kigae tu kwenye vigae wenziwe vya udongo!

Je? Udongo unaweza kumwambia mfinyanzi: Unafanya nini?

Au kiko kiumbe chako kiwezacho kukuambia: Hana mikono?

10Yatampata amwambiaye baba yake:

Watoto unawazalia nini?

au amwambiaye mama yake: Mimba unazipatia nini?

11Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, Mtakatifu wa Isiraeli,

yeye aliyemtengeneza asema: Niulizeni yatakayokuja!

Niagizieni nayo mambo ya watoto wangu!

Kwani ndio kazi za mikono yangu.

12Mimi nilifanya nchi, nikawaumba watu waikaao;

mikono yangu mimi iliziwamba mbingu,

navyo vikosi vyao vyote niliviagiza, vitokee.

13Mimi nimemwamsha naye yeye (Kiro) kwa hivyo, nilivyo mwongofu,

nazo njia zake zote na nizinyoshe.

Yeye ndiye atakayeujenga mji wangu,

nao watu wangu waliotekwa atawafungua, wajiendee;

lakini havitakuwa kwa makombozi

wala kwa fedha za kupenyezewa.

Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.

14Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Wamisri na mali zao, walizozisumbukia,

nao Wanubi na mapato yao, waliyoyachuuzia,

nao Waseba, wale watu warefu, watakufikia, wawe wako;

wakikuangukia na kukulalamikia,

watakwenda nyuma yako wakiwa wamejifunga mapingu,

kwani kwako yuko Mungu,

hakuna mwingine tena awaye yote aliye Mungu.

15Wewe ndiwe Mungu kweli, ijapo uwe mwenye mafumbo,

u Mungu wa Isiraeli, u mwokozi.

16Wao wote pamoja watakuwa wameona soni kwa kutwezwa,

mafundi wa vinyago watakuwa wamejiendea kwa kutwezwa.

17Isiraeli atakuwa ameokolewa na Bwana,

atapata wokovu wa kale na kale,

hamtaona soni, wala hamtatwezeka

siku za kale na kale zitakazokuwa zote.

18Kwani hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyeziumba mbingu,

yeye Mungu, aliyeifanya nchi na kuitengeneza vema,

yeye aliyeishikiza, kwa kuwa hakuiumba, iwe tupu,

yeye aliyeitengeneza, watu waikae, yeye anasema:

Mimi ndimi Bwana, hakuna mwingine tena.

19Sikusema fichoni mahali penye giza ya nchi,

wala sikuwaambia walio uzao wa Yakobo: Nitafuteni bure!

Mimi Bwana husema yenye wongofu, hutangaza yanyokayo!

20Njoni, kusanyikeni, mfike karibu,

ninyi masao ya wamizimu mliopona!

Hawajui kitu wajitwikao vinyago vya miti

kulalamikia mungu usioweza kuokoa.

21Semeni, leteni mashahidi! Na wapige shauri pamoja!

Yuko nani aliyeambia watu haya, wakiyasikia huko kale?

Yuko nani aliyeyatangaza tangu mwanzo?

Si mimi Bwana? Hakuna tena aliye Mungu, isipokuwa mimi.

Mungu aliye mwongofu na mwokozi hayuko pasipo mimi.

22Nigeukieni, mwokoke, ninyi mapeo yote ya nchi!

Kwani mimi ndimi Mungu, hakuna mwingine tena.

23Nimeapa na kujitaja mwenyewe,

neno lenye wongofu likatoka kinywani mwangu,

nalo halitarudi bure, hilo la kwamba:

Mimi wote watanipigia magoti,

ndimi zao zote zikisema kwa kuapa:

24Kwake Bwana peke yake ndiko,

nilikopata wongofu na nguvu.

Sharti waje kwake na kuona soni wote waliomkasirikia.

25Kwake Bwana watapata wongofu,

kisha watamshangilia wote walio wa uzao wake Isiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania