The chat will start when you send the first message.
1Shuka, ukae mavumbini, binti Babeli uliye mwanamwali!
Kaa chini! Hakuna kiti kitukufu, mwana wa Wakasidi!
Hutaitwa tena mwanana mwenye mwili mzuri.
2Chukua jiwe la kusagia, jike na dume,
usage unga mwenyewe ukiisha kuuvua ukaya wako!
Pandisha nguo, mapaja yaoneke, ukipita mito!
3Uchi wako na ufunuliwe, nayo yakutiayo soni yaoneke!
Nitakulipisha hivyo, hakuna nitakayemhurumia.
4Mkombozi wetu ni Bwana Mwenye vikosi,
Jina lake ni Mtakatifu wa Isiraeli.
5Nyamaza kimya, uende zako gizani,
mwana wa kike wa Wakasidi!
Kwani hawatakuita tena bibi mwenye nchi za kifalme.
6Nilipowakasirikia walio ukoo wangu,
ndipo, nilipowachafua walio fungu langu,
nikawatia mikononi mwako,
lakini wewe hukuwahurumia,
ukawatwika nao wazee mizigo yako iliyowalemea sana.
7Ukasema kwamba: Kale na kale nitakuwa mfalme!
Kwa hiyo hukuyawaza hayo moyoni,
wala hukukumbuka, ya kuwa yako na mwisho.
8Sasa yasikie haya, wewe mcheshi uliyekaa salama,
uliyesema moyoni mwako: Ni mimi, hakuna mwingine tena!
Sitakaa ujane, wala sitakujua kuwa pasipo watoto.
9Tena yatakujia siku moja na kukugundua hayo mambo mawili:
kuwa pasipo watoto na kukaa ujane;
haya yatakujia yote pamoja,
ijapo mazindiko yako yawe mengi,
ijapo kugangua kwako kuwe kwenye nguvu sana.
10Ulijiegemeza kwa ubaya wako ukisema: Hakuna anayeniona.
Werevu wako na ujuzi wako ukakuponza,
ukasema moyoni mwako:
Ni mimi, hakuna mwingine tena!
11Basi, mabaya yatakujia, usiyojua kuyalogoa;
teso litakuangukia, usiloweza kujizindikia.
Mara angamizo litakujia, usilolijua.
12Jisimamie hapo, unapogangua, panapo mazindiko yako mengi,
ambayo ulijisumbua nayo tangu ujana wako;
labda utaweza kujipatia mafaa, labda utastusha watu.
13Umechokeshwa na mashauri yako mengi;
sasa na watokee, wakuokoe,
wao waaguliao ya mbinguni nao wachunguzao nyota,
wao waliolinganya kila mwandamo wa mwezi upande,
yatakakotokea mabaya yatakayokujia.
14Watazameni! Wako kama makapi yaliyounguzwa na moto,
hawawezi kujiokoa wenyewe katika moto uwashikao,
hakuna makaa ya kuyaotea,
wala hakuna jiko lenye moto la kukaa hapohapo.
15Ndivyo, walivyokufanyia nao wachuuzi wako,
uliowasumbukia tangu ujana wako,
wametawanyika, kila mmoja upande wake, hakuna akuokoaye.