Yesaya 50

Yesaya 50

Makosa yao ndiyo yaliyowaponza Waisiraeli.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kiko wapi cheti cha kuachana,

nilichompa mama yenu nilipomtuma kujiendea?

Au yuko nani aliyenidai, nikawauza ninyi kwake?

Tazameni: Mmeuzwa kwa ajili ya manza zenu, mlizozikora;

tena ni kwa ajili ya mapotovu yenu,

mama yenu akitumwa kujiendea.

2Ilikuwaje, nisione mtu nilipofika? Au nilipoita, asijibu mtu?

Je, Mokono wangu ulikuwa mfupi, usiweze kukomboa?

Au je? Sinazo nguvu za kuponya?

Tazameni! Kwa nguvu za makemeo yangu naikausha bahari,

nayo mito naigeuza kuwa jangwa,

samaki wao wanuke kwa kukosa maji wanapokufa kwa kiu.

3Mbingu nazivika weusi, ninapozifunika kama kwa gunia.

Mtumishi wa Bwana aleta wokovu.

4Bwana Mungu amenipa ulimi uliojifunza,

mpaka ukijua kuegemeza mchovu kwa kusema naye,

huniamsha kunapokucha, huliamsha sikio langu,

lisikilize, kama wenye kujifunza wanavyosikiliza.

5Bwana Mungu amenizibua sikio,

nami sikukataaa, wala sikurudi nyuma.

6Mgongo wangu nimeuelekezea wao walionipiga,

nayo mashavu yangu wao walioning'oa ndevu,

uso wangu sikuufichia wao walionitweza,

ndio wao walionitemea mate.

7Bwana Mungu akanisaidia, kwa hiyo sikutwezeka,

kwa hiyo nikaushupaza uso wangu kuwa kama jiwe la moto,

nikajua, ya kuwa sitaiva uso.

8Yuko karibu atakayenishindisha;

yuko nani atakayenigombeza? Na tutokee kusimama pamoja!

Yuko nani atakayenipeleka shaurini? Na aje, twende!

9Na mwone, ya kuwa Bwana Mungu ananisaidia!

Yuko nani atakayenishinda?

Na mwone, ya kuwa hawa wote watachakaa

kama nguo, ikiliwa na nondo!

10Yuko nani kwenu anayemwogopa Bwana?

Yuko nani kwenu anayeisikiliza sauti ya mtumishi wake?

Akienda gizani pasipo kumulikiwa

na aliegemee Jina la Bwana! Na ajikongojee Mungu wake!

11Sasa ninyi nyote mnaowasha moto,

mwikoleze mishale ya moto,

nendeni kuunguzwa na moto wenu,

mishale, mliyoiwasha, iwachome moto!

Hayo yatatokea mkononi mwangu,

yawajie, mlazwe mahali panapoumiza.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania