The chat will start when you send the first message.
1Amka! Amka! Ivae nguvu yako, Sioni!
Zivae nguo zako tukufu, Yerusalemu, ulio mji mtakatifu!
Kwani mwako hatamwingia tena
asiyetahiriwa wala mwenye uchafu.
2Yakung'ute mavumbi, kisha inuka, upate kukaa, Yerusalemu!
Yafungue mafungo yaliyopo shingoni pako,
binti Sioni, uliofungwa!
3Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mliuzwa bure, kwa hiyo hamtakombolewa kwa fedha.[#Yes. 50:1.]
4Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Misri ndiko, walikotelemkia kwanza walio ukoo wangu, wakae huko; lakini Waasuri wamewakorofisha bure.
5Sasa inakuwaje? Ninapata nini hapo? ndivyo, asemavyo Bwana. Walio ukoo wangu wamechukuliwa bure, nao wanaowatawala hulia kwa furaha, tena siku zote Jina langu hutukanwa; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Ez. 36:20.]
6Kwa sababu hii walio ukoo wangu na walijue Jina langu, kweli siku ile watajua, ya kuwa mimi ndimi nisemaye: Nitazameni, nipo!
7*Tazameni, miguu yake mpiga mbiu njema
jinsi inavyopendeza milimani,
anapotangaza utengemano,
anapopiga mbiu ya mambo mema, anapotangaza wokovu,
anapouambia Sioni: Mungu wako ni mfalme!
8Zisikilize sauti za walinzi wako!
Wamepaza sauti pamoja na kupiga shangwe,
kwani wanaona na macho yao, Bwana akirudi Sioni.
9Pigeni shangwe na kupaza sauti,
ninyi mabomoko ya Yerusalemu!
Kwani Bwana amewatuliza mioyo walio ukoo wake,
akaukomboa Yerusalemu.
10Mkono wake mtakatifu Bwana ameuvua nguo
machoni pa makabila yote ya watu,
mapeo yote ya nchi yauone wokovu wa Mungu wetu.*
11Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa! Msiguse yenye uchafu!
Tokeni humu kati! Jitakaseni, ninyi
mnaovichukua vyombo vya Bwana!
12Kwani hamtatoka upesiupesi,
wala hamtakwenda na kukimbia,
kwani atakayewaongoza ni Bwana,
naye atakayewakusanya nyuma ni Mungu wa Isiraeli.
13Mtazameni mtumishi wangu,
jinsi atakavyoendelea kwa welekevu:
atatukuka na kukwezwa, awe mkuu kabisa!
14Kama wengi walivyokustuka, watamstuka naye:
kwa kuwa walipomtazama alikuwa amenyongeka kuliko watu,
nalo umbo lake halikuwa kama la wana wa watu;
15ndivyo, atakavyoshangaza makabila mengi ya watu,
nao wafalme wafumbe vinywa vyao kwa ajili yake yeye;
kwani watakaomwona ndio wasioambiwa Neno lake,
nao wasiolisikia watalijua maana.