Yesaya 53

Yesaya 53

Mateso yake mtumishi wa Bwana.

1*Yuko nani anayeutegemea utume wetu?

Yuko nani aliyefumbuliwa,

mkono wake Bwana unayoyafanya?

2Alikua machoni pake kama mche,

kama chipuko la shina lililoko katika nchi kavu,

hakuwa mwenye uzuri wala mwenye utukufu wa mwili,

tulipomtazama, hakuna umbo lililotupendeza.

3Akabezwa, akaachwa na watu,

akajulikana kuwa mwenye maumivu,

akabezwa kama mtu, watu wanayemfichia nyuso zao,

tukamwazia kuwa si kitu.

4Kumbe ameyachukua manyonge yetu,

akajitwisha maumivu yetu,

nasi tukamwazia kwamba:

Ameteswa na Mungu, akapigwa naye, anyongeke.

5Kumbe ilikuwa kwa ajili ya mapotovu yetu, akichomwa,

akaumizwa kwa ajili ya manza zetu, tulizozikora sisi;

akapatilizwa, sisi tupate kutengemana,

namo katika mavilio yake ndimo, tulimoponea.

6Sote tulikuwa tumepotea kama kondoo,

kila mtu akiishika njia yake,

naye Bwana akampigia manza, tulizozikora sisi wote.

7Alipoonewa yeye amevumilia tu, hakukifumbua kinywa chake

kama kondoo, akipelekwa kuchinjwa;

au kama mwana kondoo anavyowanyamazia wenye kumkata manyoya,

hakukifumbua kinywa chake.

8Ameuawa kwa kusongwa na kwa kunyimwa uamuzi mnyofu,

lakini kwao wa kizazi chake yuko nani ayawazaye kwamba:

Ameondolewa katika nchi yao walio hai,

alipopigwa kwa ajili ya upotovu wao walio ukoo wake?

9Wakampa kaburi lake pamoja nao wasiomcha Mungu,

alipokwisha kufa akazikwa pake mwenye mali,

naye hakufanya ukorofi,

uwongo tu haukuonekana kinywani mwake.

10Lakini Bwana alipendezwa na kumwumiza, asipone, kwamba:

Atakapojitoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi

kwa ajili ya makosa ya watu,

ndipo, atakapopata mazao,

ndipo, siku zake zitakapoanzia kuwa nyingi,

nayo yampendezayo Bwana yatatimizwa na mkono wake.

11Kwa kuwa roho yake imesumbuliwa,

na aone mapato ya kumshibisha;

naye alivyo mtumishi wangu mwongofu,

ndivyo, atakavyopatia wengi wongofu kwa ujuzi wake,

kwani amejitwisha manza zao, walizozikora.

12Kwa hiyo nitamgawia wengi, wawe fungu lake,

naye atawagawia wanguvu mateka yao, yawe mafungu yao,

kwa kuwa ameimwaga roho yake, ife,

akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu.

Naye ameyachukua makosa ya watu wengi,

akawaombea nao wapotovu.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania