Yesaya 54

Yesaya 54

Maaagano mapya, Mungu anayouwekea Sioni.

1Shangilia, wewe uliye mgumba, usiyezaa!

Jichekelee na kupaza sauti, wewe usiyeona uchungu wa kuzaa!

Kwani wana wake yule aliye peke yake ni wengi

kuliko wana wake yule aliye na mumewe; ndivyo, Bwana anavyosema.

2Papanue mahali pa hema lako!

Nazo nguo za hema za makao yako

na waziwambe na kuzivuta! Usiwazuie!

Kamba za hema ziongeze, ziwe ndefu!

Mambo zake zipigilie, zishike vema!

3Kwani utazieneza pande za kuumeni nazo za kushotoni,

nao wazao wako watatwaa makabila ya watu,

wakae katika mahame ya miji yao.

4Usiogope! Kwani hutapatwa na soni,

wala hutaiva uso, kwani hutadanganyika,

kwa kuwa utazisahau soni, ulizoziona ulpokuwa kijana,

nayo matusi, uliyotukanwa ulipokuwa mjane, hutayakumbuka.

5Kwani mumeo ni yeye aliyekufanya,

Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake,

naye mkombozi wako ni Mtakatifu wa Isiraeli

aitwaye Mungu wa nchi zote.

6Kwani ulipokuwa mwanamke aliyeachwa,

aliyesikitika rohoni, Bwana alikuita.

Naye mke wa ujana anakataliwaje?

Ndivyo, Mungu wako anavyosema.

7Kweli kitambo kidogo nimekuacha,

lakini nitakupokea tena kwa huruma kubwa.

8Makali yalipofurika,

nimeuficha uso wangu punde kidogo, usiuone,

lakini kwa upole ulio wa kale na kale nitakuhurumia;

ndivyo, Bwana aliye mkombozi wako anavyosema.

9Hayo yatakuwa, kama yalivyokuwa katika mafuriko ya Noa,

nikaapa: Mafuriko ya Noa hayataididimiza nchi tena;

vivyo hivyo nimeapa sasa kwamba:

Sitakutolea makali tena, wala sitakukaripia.

10Ijapo milima iondoke,

ijapo navyo vilima vitikisike,

upole wangu hautaondoka kwako,

wala agano la utengemano wangu halitatikisika;

ndivyo, Bwana akuhurumiaye anavyosema.

11Kweli umenyongeka kwa kutikiswa na upepo mkali,

hukutulizwa moyo!

Lakini na uone, mimi ninavyokujenga

na kuyaweka mawe yako katika udongo wenye wanja

na kuitengeneza misingi yako kwa mawe ya safiro.

12Minara yako nitaijenga kwa mawe ya yaspi,

nayo malango yako kwa mawe yamulikayo,

nalo boma lako zima kwa mawe ya vito vizuri.

13Watoto wako wote watakuwa wamefundishwa na Bwana,

hivyo watoto wako watakuwa wametengemana kabisa.

14Wongofu wao utakuwa nguvu zako;

kwa hiyo jitenge na ukorofi!

Kwani hakuna kitakachokuogopesha.

Acha kustuka! Kwani hakuna tisho litakalokufikia.

15Kama wanakujia, si kwa kuagizwa na mimi;

kwa hiyo yuko nani atakayekujia, akupige?

Hapo atakapopigana na wewe ataanguka.

16Tazameni! Mimi nimeumba mafundi

wanaowakisha moto wa makaa,

watengeneze mata ya kufanyia kazi zao;

tena mimi ndiye niliyeumba nao waangamizi wa kuyavunja.

17Hakuna mata yatakayozimaliza kazi zao

yakiwa yametengenezwa ya kukuumiza,

nao kila ulimi utakaokuinukia shaurini

utashinda na kuupatilizia mabaya;

hilo ndilo fungu, watumishi wake Bwana watakalolitwaa,

hilo ndilo pato la wongofu wao, nitakalowapatia;

ndivyo, asemavyo Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania