Yesaya 56

Yesaya 56

Watakaoyapata magawio ya Agano Jipya.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Yaangalieni yapasayo, myafanye yaongokayo!

Kwani wokovu wangu uko karibu, utokee,

nao wongofu wangu na ufunuliwe.

2Mwenye shangwe ni mtu atakayeyafanya

naye mwana wa mtu atakayeyashika,

anayeziangalia siku za mapumziko, asizichafue,

anayeiangalia mikono yake, isifanye kibaya cho chote.

3Naye mwana wa nchi ngeni aliyeandamana na Bwana asiseme:

Bwana atanitenga kabisa kwao walio ukoo wake!

Wala aliyekatazwa kuzaa asiseme: Nitazameni, mimi ni mti mkavu!

4Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Waume wasiozaa kama wanazingalia siku zangu za mapumziko,

kama wanayachagua yanipendezayo,

walishike sana Agano langu,

5nitawapa nyumbani mwangu na bomani kwangu mahali,

ndipo majina yao yakae,

napo patakuwa pema kuliko pengine

penye wana wa kiume na wa kike;

kweli nitawapa majina ya kale na kale yasiyong'oleka.

6Nao wana wa nchi ngeni walioandama na Bwana, wamtumikie,

walipende Jina lake Bwana, wawe watumishi wake,

wote waziangaliao siku zake za mapumziko,

wasizichafue, walishike Agano lake,

7hawa nitawapeleka kwenye mlima wangu mtakatifu,

niwafurahishe Nyumbani mwangu mwa kuombea,

nazo ng'ombe zao za tambiko

na vipaji vyao vingine vya tambiko vitanipendeza

vitakapotolewa mezani pangu pa kunitambikia,

kwani Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea

kwao makabila yote ya watu.

8Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu

anayewakusanya Waisiraeli waliotawanyika:

Wako wengine wa kwao, nitakaowakusanya,

niwatie kwao waliokusanywa.

Mapatilizo ya wachungaji wabaya.

9Ninyi nyama wa porini nyote,

nanyi nyama wa mwituni, nyote njoni, mle!

10Walinzi wa watu wangu ni vipofu wote, hawajui kitu;

wote ni mbwa mabubu wasioweza kulia,

hulala na kuota ndoto, hupenda kupumzika tu.

11Tena ni mbwa walafi wasiojua kushiba;

hawa walio wachungaji hawajui kitu,

wala hawatambui maana,

wote wamezishika njia zao,

kila hutaka kupata tu, hakuna asiye hivyo.

12Husema; Njoni, nichukue mvinyo,

tunywe, hata tutakapolewa!

Vivyo hivyo itakuwa nayo siku ya kesho,

iwe sikukuu kabisa kupita cheo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania