Yesaya 57

Yesaya 57

1Mwongofu akiangamia,

hakuna aumiaye moyoni;

wapole wakiondolewa,

hakuna ayatambuaye,

ya kuwa mwongofu huondolewa, ubaya ulipo.

2Nao huingia kwenye utengemano,

hupumzika hapo, wanapolala wao

waliozifuata njia zao zinyokazo.

Kuhangaika kwao wasiomcha Mungu.

3Nanyi karibuni hapa, mlio wana wa mwaguaji wa kike!

Mlio uzao wa mvunja unyumba na mwanamke mgoni!

4Yuko nani, mnayemcheka?

Yuko nani, mnayemwasamia vinywa na kutoa ndimi?

Je? Ninyi ham wana wa upotovu na mazao ya uwongo?

5Mnaingiwa na tamaa chini ya mitamba

napo chini ya kila mti wenye majani meusi,

mnachinja watoto mitoni kwenye mapango ya miamba.

6Mawe ya mtoni yatelezayo na fungu lako,

hayo ndiyo, unayoyatumia kuwa kura yako;

nayo huyamwagia vinywaji vya tambiko,

ukayatolea hata vilaji vya tambiko.

Sasa je? Hayo niyanyamazie tu?

7Kwenye mlima mrefu juu kileleni

hujitandikia pako pa kulalia,

ukipanda huko kuchinja ng'ombe za tambiko.

8Kwa kuniacha mimi unakiweka kinyago chako cha nyumbani

nyuma ya mlango kwenye miimo;

kisha ukakifunua kilalo chako, ukakipanda,

ukakipanua, ukajichagulia mmoja wao,

ukapenda kulala nao, ulipoona mkono uliokupungia.

9Ukasafiri kumwendea mfalme

ukichukua mafuta ya kukipaka na manukato yako mengi,

ukatuma wajumbe wako kwenda katika nchi za mbali,

ukawaendesha hata kushuka kuzimuni.

10Ukachoka kwa njia zako nyingi,

lakini hukusema: Tamaa zimekatika;

ulipoona mkononi mwako, ya kuwa nguvu zimo bado,

basi, hukulegea.

11Ni kwa ajili ya nani ukitishika,

ukamwogopa, ukafanya ya uwongo?

Lakini mimi hukunikumbuka, hukuniweka moyoni mwako.

Imekuwaje? Sivyo hivyo:

kwa kuwa mimi nimenyamaza tangu kale, hukuniogopa?

12Nami na nitangaze, wongofu wako ulivyo,

lakini viumbe vyako havitakufalia kitu.

13Utakapolia, na vikuponye vile vyote, ulivyovikusanya!

Lakini hivyo upepo utavichukua, pumzi tu itaviondoa.

Naye anikimbiliaye ataitwaa nchi,

nao mlima wangu mtakatifu ataupata kuwa wake.

Wajutao wataokoka.

14Amesema: Chimbeni! Chimbeni! Itengenezeni njia!

Yaondoeni makwazo njiani kwao walio ukoo wangu!

15Kwani hivi ndivyo, anavyosema atukukaye, Alioko huko juu,

akaaye kale na kale,

aitwaye jina lake Mtakatifu:

Ninakaa hapa juu patakatifu,

tena kwao wapondekao na kunyenyekea rohoni,

nizirudishe uzimani roho zao wanyenyekevu,

niirudishe uzimani nayo mioyo yao wapondekao.

16Kwani sitagomba kale na kale,

wala sitakasirika siku zote,

roho zao zisizimie mbele yangu

pamoja nao wenye pumzi, niliowafanya mimi.

17Ubaya wa choyo chao niliukasirikia,

nikawapiga nikijificha kwa kuwa na makali,

nao wakajiendea na kuniacha,

wakashika njia za kuipendeza mioyo yao.

18Nikaziona hizo njia zao,

kwa hiyo nitawaponya na kuwaongoza,

niwalipe na kuwatuliza mioyo

wao na wenzao, waliowasikitikia.

19Na niumbe mazao ya midomo

itakayotangaza utengemano kwamba:

Utengemano utawajia walioko mbali nao walioko karibu!

Ndivyo, anavyosema Bwana: Kweli nitawaponya.

20Lakini wasiomcha Mungu hufanana na bahari ichafukayo,

isiyoweza kutulia kamwe,

mawimbi yake hayakomi kutoa machafu na takataka.

21Hakuna utengemano kwao wasiomcha Mungu;

ndivyo, anavyosema Mungu wangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania