The chat will start when you send the first message.
1Ita kwa kinywa kikuu! Usijizuie!
Paza sauti yako, kama ni baragumu!
Walio ukoo wangu watangazie mapotovu yao!
Walio mlango wa Yakobo watangazie makosa yao!
2Kweli siku kwa siku hunitafuta,
hutaka kuzijua njia zangu,
kama ni watu wafanyao yaongokayo,
kama ni watu wasioyaacha yampasayo Mungu wao;
wakaniuliza mashauri yaongokayo
wakinitaka mimi Mungu, niwafikie karibu.
3Husema: Mbona huoni, tukifunga mifungo?
Mbona hujui, tukizisumbua roho zetu?
Lakini tazameni: Siku mnapofunga
hufuata mambo, myapendayo,
nao wakazi wenu huwashurutisha kuja kazini.
4Tazameni: Mnapofunga hugombana na kutetena,
mkapigana makonde, kwani hammchi Mungu,
hamfungi kwamba: Ni siku ya kumlilia Alioko huko juu.
5Je? Huo ndio mfungo, nilioupenda,
uwe siku, mtu anapojinyima yamfaayo?
Mtu akikiinamisha kichwa chake kama unyasi,
tena akilalia gunia na majivu,,
huo utauita mfungo na siku ya kumpendeza Bwana?
6Je? Mfungo, nilioupenda sio huu:
kufungua mafungo ya ukorofi,
kulegeza kamba za utumwa,
kuwapa ruhusa waliopondeka, wajiendee,
kuvunja utumwa wo wote?
7Sivyo hivyo? Ukimgawia mwenye njaa mkate wako.
ukiingiza nyumbni mwako wakiwa waliofukuzwa,
unapoona mwenye uchi ukimpa nguo,
usipowakataa walio wa mlango wako?
8Ukifanya hivyo, ndipo, mwanga wako utakapopambazuka
kama mionzi ya jua,
ndipo, vidonda vyako vitakapopona upesi,
ndipo, wongofu wako utakapokutangulia,
nao utukufu wa Bwana utakufuata nyuma.
9Ndipo, itakapokuwa hivyo: utakapoita, Bwana atakuitikia;
utakapolia, atakuambia: Mimi hapa!
Lakini kwanza sharti uondoe utumwa katikati yako,
uache kunyoshea watu vidole na kusema maovu.
10Mwenye njaa utakapompa, roho yako iyatakayo nayo,
utakapoishibisha roho ya mkiwa,
ndipo, mwanga wako utakapotokea gizani,
ndipo, weusi wa usiku utakapokuwa kwako kama jua la mchana.
11Naye Bwana atakuongoza siku zote,
aishikize roho yako katika nchi kavu;
nayo mifupa yako ataishupaza,
uwe kama shamba lililonyweshwa
au kama kisima cha maji kisichodanganya
kwa kuwa na maji yasiyokauka.
12Nao watakaotoka kwako
watayajenga mabomoko yako ya kale,
nayo misingi ya vizazi na vizazi
utaitengeneza tena;
kwa hiyo watakuita:
Mjenga nyufa na Mfufua njia, watu wakae.
13Kama utaikataza miguu yako siku za mapumziko,
isifanye penye siku yangu takatifu yakupendezayo,
kama siku ya mapumziko utaiita ya kupendezwa,
kwa kuwa ni siku ya Bwana mtakatifu ipasayo kutukuzwa,
ukaitukuza na kuacha kuzishika njia zako,
usipoyafuata uyapendayo, usipojisemea maneno tu:
14ndipo, utakapopendezwa na Bwana,
nami nitakupitisha kwenye vilima vya nchi,
kisha nitakupa nalo fungu la baba yako Yakobo, ulile,
kwani kinywa chake Bwana kimeyasema.