Yesaya 59

Yesaya 59

Makosa huuzuia wokovu.

1Tazameni: Mkono wake Bwana sio mfupi, usiweze kuokoa,

wala masikio yake siyo mazito, yasiweze kusikia.

2Ila manza zenu, mlizozikora, ndizo

zinazowatenga ninyi na Mungu wenu,

nayo makosa yenu ndiyo

yanayowafichia uso wake asiwasikie.

3Kwani mikono yenu imechafuliwa na damu,

hata vidole vyenu vimechafuliwa na mabaya, viliyoyafanya;

midomo yenu husema uwongo,

ndimi zenu hunong'ona mapotovu.

4Hakuna amwitaye mwenziwe shaurini

kwa kuyataka yaongokayo,

wala hakuna ahukumuye kwa kweli,

huyakimbilia yaliyo maovyo tu, hujisemea yasiyo maana,

huchukua mimba ya maumivu, huzaa mapotovu.

5Huangua mayai ya pili, hufuma matandabui;

mtu akiyala mayai yao hufa,

nalo lipasukalo hutoka nyoka.

6Matandabui yao hayatumiki kuwa mavazi,

hawawezi kujifunika kwa hizo kazi zao;

kazi zao ni kazi za upotovu,

matendo ya ukorofi yamo mikononi mwao.

7Miguu yao hukimbilia mabaya,

hupiga mbio kuja kumwaga damu zao wasiokosa,

mawazo yao ni mawazo mapotovu,

maangamizo na mavunjiko huzijulisha njia zao.

8Lakini njia ya utengemano hawaijui,

wala maamuzi yapasayo hayako kwenye mapito yao,

mikondo yao wameipotoa,

wote waifuatao hawajui utengemano.

Kujutia makosa.

9Kwa sababu hii maamuzi yapasayo yametukalia mbali,

nayo yaongokayo hayafiki kwetu.

Tukangojea, kuche, lakini tunaona giza tu,

tukangojea, kupambazuke,

lakini vivyo hivyo tunajiendea na weusi wa usiku.

10Tunapapasa ukutani kama vipofu,

kweli tunapapasa tu kama watu wasio na macho;

tunajikwaa na mchana, kama ni jioni,

tuko kama wafu kwao walio wenye nguvu.

11Sisi sote huvuma kama nyegere,

hulia, kama hua wanavyolia,

tukayangojea yale maamuzi yapasayo, lakini hayako,

tukaungojea wokovu, nao ukawa mbali, usifike kwetu.

12Kwani mapotovu yetu yako mengi mbele yako,

nayo makosa yetu yanatusuta;

kwani mapotovu yetu yako kwetu,

nazo manza zetu tunazijua.

13Tumemtengua Bwana na kumkana,

tukarudi nyuma na kumwacha Mungu wetu,

tukasema maoneo na machokozi,

tukachukua maneno ya uwongo kama mimba,

tukayatoa tena mioyoni.

14Kwa hiyo maamuzi yapasayo yamerudishwa nyuma,

nayo yaongokayo yakasimama mbali;

kwani ya kweli yalijikwaa njiani,

nayo yaliyo sawa hayakuweza kuingia.

15Kwa hiyo kweli ikakosekana,

naye aliyeacha mabaya hunyang'anywa.

Bwana alipoyaona, yakawa mabaya machoni pake,

kwa kuwa hakuna maamuzi yapasayo.

Mapatilizo ya wabaya na wokovu wao wajutao.

16Akaona, ya kuwa hakuna mtu,

akashangaa, ya kuwa hakuna msaidiaji;

ndipo, mkono wake ulipomtumikia kuwa wa kuokoa,

nao wongofu wake ukamshikiza.

17Akajivika wongofu kuwa fulana ya chuma kifuani,

kichwani akavaa wokovu kuwa kofia,

kisha akajivika lipizi kuwa mavazi ya mwili,

akajifunika wivu kuwa nguo za juu.

18Kama matendo yao yalivyo,

ndivyo, nayo malipizi yatakavyokuwa:

makali yatawatokea waliompingia,

nao waliomchukia watafanyiziwa vivyo hivyo,

hata visiwa atavilipisha matendo yao.

19Hapo ndipo, watakapoliogopa Jina la Bwana machweoni kwa jua,

nako maawioni kwa jua watauogopa utukufu wake,

kwani atakuja kama mto unaopita mahali pembamba,

upepo wa Bwana ukiyasukuma maji yake.

20Sioni ataingia atakayewakomboa wa Yakobo

walioyaacha mapotovu;

ndivyo, asemavyo Bwana.

21Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Hili ni agano langu mimi, ninalolifanya nao:

Roho yangu inayokukalia

na maneno yangu, niliyoyatia kinywani mwako,

hayataondoka kinywani mwako,

wala vinywani mwao walio wa uzao wako,

wala mwao walio uzao wa uzao wako,

kuanzia sasa hata kale na kale;

ndivyo, Bwana anavyosema.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania