Yesaya 60

Yesaya 60

Utukufu wa Sioni.

1*Inuka uangazike!

Kwani mwanga wako unakuja,

nao utukufu wa Bwana umekuzukia.

2Kwani tunapotazama, giza linaifunika nchi,

mawingu meusi yanayafunika makabila ya watu,

lakini wewe, Bwana anakuzukia,

nao utukufu wake unaonekana juu yako.

3Wamizimu wataujia mwanga wako,

nao wafalme wataujia mmuliko uliozuka kwako.

4Yainue macho yako, utazame po pote!

Hao wote wamekusanyika, waje kwako;

wanao wa kiume watakuja, wakitoka mbali,

wanao wa kike wataletwa na kubebwa.

5Utakapowaona utachangamka,

nao moyo wako utapigapiga, upanuke,

kwani mafuriko ya bahari yatageuka, yaje kwako,

nayo mapato ya wamizimu yataingia kwako.

6Makundi ya ngamia yatakufunika,

hata vijana wa ngamia wa Midiani na wa Efa,

wote watatoka Saba, waje kwako,

wakichukua dhahabu na uvumba,

nao watamtangaza Bwana na kumshangilia.*

7Makundi yote ya Kedari,

yale ya mbuzi na ya kondoo yatakusanyika kwako,

madume ya Nebayoti utayatumia ya tambiko,

yatanipendeza juu ya meza ya kunitambikia;

ndivyo, nitakavyoitukuza Nyumba ya utukufu wangu.

8Hao ni wa nani wanaoruka kama mawingu

au kama hua wanaoyarukia matundu yao?

9Kwani visiwa vinaningojea,

nazo merikebu za Tarsisi zitakuwa za kwanza

za kuwaleta wanao toka nchi za mbali;

fedha zao na dhahabu zao wanazo

za kulitolea Jina la Bwana Mungu wako,

kwa kuwa yeye aliye Mtakatifu wa Isiraeli amekupa utukufu.

10Wana wa nchi ngeni watalijenga boma lako,

nao wafalme wao watakutumikia,

kwani nilipokuchafukia nilikupiga,

tena nilipopendezwa nawe nimekuhurumia.

11Malango yako yatakuwa wazi siku zote,

hayatafungwa mchana wala usiku,

wakuletee mapato ya wamizimu,

nao wafalme wao watajitia mumo humo.

12Kwani kila taifa na kila nchi ya kifalme

itakayokataa kukutumikia itaangamia,

nao watu wao watatoweka kabisa.

13Utukufu wa Libanoni utakuja kwako,

mivinje na mitamba na mizambarau yote pamoja

iwe mapambo ya mahali pangu patakatifu,

maana mahali, miguu yangu itakapopakanyaga,

nitapapatia marembo.

14Nao wana wao waliokutesa

watakuja kwako na kuinama chini,

nao wote waliokutukana

watakuangukia penye nyayo za miguu yako,

watakuita mji wa Bwana,

Sioni wa Mtakatifu wa Isiraeli.

15Kwa sababu ulikuwa umeachwa, ukachukizwa,

watu wakakataa kupitia kwako,

kwa hiyo nitakuweka kuwa mahali

pa kujivunia kale na kale,

tena kuwa wa kufurahisha vizazi na vizazi.

16Utanyonya maziwa ya mataifa mengine,

kweli vifuani kwa wafalme utanyonya,

kwani mimi Bwana ni mwokozi wako,

mkombozi wako ni yeye amtawalaye Yakobo.

17Penye shaba nitaleta dhahabu,

penye vyuma nitaleta fedha,

penye miti nitaleta shaba,

penye mawe nitaleta vyuma.

Nitaweka utengemano kuwa ukuu wako

nao wongofu kuwa ubwana wako.

18Hayatasikiwa tena makorofi katika nchi yako,

wala hayatasikilika maangamizo na mavunjiko

katika mipaka yako.

Boma lako utaliita Wokovu,

nayo malango yako utayaita Mashangilio.

Bwana mi mwanga wao walio ukoo wake.

19Halitawaka tena jua kwako kuwa mwanga wa mchana,

wala mwezi hautakumulikia tena, upate kuona,

kwani Bwana atakuwa mwanga wako kale na kale,

Mungu wako atakuwa utukufu wako.

20Jua lako halitakuchwa tena,

wala mwezi wako hautakufa tena,

kwani Bwana atakuwa mwanga wako wa kale na kale,

nazo siku zako za kusikitika zitakuwa zimekwisha.

21Walio wa ukoo wako wote watakuwa waongofu,

watakuwa wenye nchi kale na kale,

kwa kuwa ni shamba, nililolipanda,

ni kazi ya mikono yangu, nijipatie matukuzo.

22Aliye mdogo atageuka kuwa elfu,

naye aliye mnyonge atageuka kuwa taifa lenye nguvu.

Mimi Bwana nitayafanyiza upesi,

siku zake zitakapotimia.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania