Yesaya 62

Yesaya 62

Utukufu wa Sioni utakaokuwa.

1Kwa ajili ya Sioni sitanyamaza,

kwa ajili ya Yerusalemu sitapumzika,

mpaka yaupasayo yatokee kama mwangaza,

mpaka wokovu wake uwe kama mwenge uwakao.

2Ndipo, wamizimu watakapoona yaliyokupasa,

nao wafalme wote watauona utukufu wako,

nawe utaitwa kwa jina jipya,

kinywa cha Bwana kitakalolitaja.

3Ndipo, utakapokuwa urembo wa kichwa

wenye utukufu mkononi mwa Bwana,

na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.

4Hutaambiwa tena: Umeachwa!

Wala nchi yako haitaambiwa tena: Ni pori tupu,

ila utaitwa: Hunipendeza,

nayo nchi yako itaitwa: Ameolewa,

kwani Bwana atapendezwa na wewe,

nayo nchi yako itaolewa.

5Kwani kama mchumba mume anavyomchukua mwali,

ndivyo, wanao watakavyokuchukua wewe,

kama mwenye ndoa anavyomfurahia mchumba wake,

ndivyo, Mungu wako atakavyokufurahia.

6*Bomani kwako, Yerusalemu, nimeweka walinzi juu,

mchana kutwa na usiku kucha wasinyamaze kamwe.

Ninyi mnaolitangaza Jina la Bwana, msiwe kimya!

7Wala msimwache Bwana kuwa kimya,

mpaka aushikize Yerusalemu tena

na kuuweka, utukuzwe katika nchi!

8Bwana ameapa na kuutaja mkono wake wa kuume

ulio na nguvu kwamba:

Sitazitoa tena ngano zako,

ziliwe na adui zako,

wala wana wa nchi ngeni

wasinywe tena pombe zako, ulizozisumbukia.

9Ila watakaozivuna ndio watakaozila, wamshukuru Bwana,

nao watakaozichuma ndio watakaozinywa

nyuani penye Patakatifu pangu.

10Piteni mlangoni, mwitengeneze njia yao

walio ukoo wetu!

Chimbeni! Ichimbeni barabara na kuyaondoa mawe!

Twekeni bendera, makabila ya watu yaione!

11Angalieni! Bwana anatangaza mapeoni kwa nchi kwamba:

Mwambieni binti Sioni:

Tazama, wokovu wako unakuja!

Tazama, mshahara wake wa kulipa anao,

nayo mapato yake yako mbele yake.

12Nao watawaita: Ukoo mtakatifu

ulio wao waliokombolewa na Bwana,

nawe utaitwa Mji uliotafutwa, usioachwa tena.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania