The chat will start when you send the first message.
1Ni nani huyu anayetoka Edomu
na kuvaa nguo nyekundu za Bosira?
Ni mtukufu katika vazi lake,
anatembea na kuzionyesha nguvu zake nyingi;
anasema: Yuko nani asemaye kwa wongofu?
Ninazo njia nyingi za kuokoa.
2Mbona vazi lako ni jekundu?
Mbona nguo zako zinafanana nazo za mkamua zabibu?
3Kweli nimekamua kamulioni mimi peke yangu,
pasipokuwa na mtu mwingine,
nikawakamua kwa makali yangu,
nikawaponda kwa moto wa machafuko yangu,
damu zao zikazirukia nguo zangu,
nikayachafua mavazi yangu yote,
4kwani ilikuwa siku ya lipizi,
niliyoiweka moyoni mwangu,
tena umetimia mwaka wa kuwakomboa walio wangu.
5Nikatazama, lakini hakuna msaidiaji,
nikachungulia na kushangaa, lakini hakuna ashikizaye;
ndipo, mkono wangu uliponitumikia kuwa wa kuokoa,
nao moto wa machafuko yangu ukanishikiza.
6Basi, nikayoponda makabila ya watu kwa makali yangu,
nikawalevya kwa moto wa machafuko yangu
nilipozimwaga damu zao chini.
7*Nitawakumbusha magawio ya Bwana na kumtukuza Bwana
kwa ajili yao yote, aliyotutendea Bwana;
mema yake ni mengi, aliyoutendea mlango wa Isiraeli
kwa huruma zake aliwagawia mengi.
8Akasema: Kumbe hawa ndio walio ukoo wangu,
ndio wanangu, hawataongopa;
akawa mwokozi wao.
9Katika masongano yao yote naye alikuwa amesongeka;
ndipo, malaika aliyetoka usoni kwake alipowaokoa,
kwa kuwapenda na kwa kuwaonea uchungu
akawakomboa yeye mwenyewe,
akawaokota, akawachukua siku zote za kale.
10Lakini wakaacha kumtii,
wakaisikitisha Roho yake takatifu;
ndipo, alipogeuka kuwa adui yao,
akapigana nao mwenyewe.
11Ndipo, wao walio ukoo wake
walipozikumbka siku za kale, siku za Mose,
wakasema: Yuko wapi aliyewatoa baharini
pamoja na mchungaji wa kundi lake?
12Kwa mkono wake wenye utukufu alimwongoza Mose
alipomshika mkono wake wa kuume,
akayatenga maji mbele yao,
ajipatie Jina la kale na kale.
13Akawapitisha vilindini
kama farasi nyikani, wasijikwae.
14Kama kundi linavyotelemka bondeni,
ndivyo, roho ya Bwana ilivyowapeleka pa kupumzikia.
Hivyo ndivyo, ulivyowaongoza walio ukoo wako,
ujipatie Jina lenye utukufu.
15Chungulia toka mbinguni!
Tazama toka Kao lako takatifu lenye utukufu!
Wivu wako uko wapi?
Matendo yako ya nguvu yako wapi?
Huruma zako zinazovuma moyoni mwako
zimejizuia, zisifike kwangu.
16Kwani wewe ndiwe baba yetu;
kwani Aburahamu hakutujua,
wala Isiraeli hakututambua.
Wewe Bwana ndiwe baba yetu;
Mkombozi wetu ndilo jina lako la kale.*
17Mbona umetupoteza, Bwana, tukaziacha njia zako?
Mbona umeishupaza mioyo yetu, isikuogope?
Rudi kwa ajili ya watumishi wako
walio milango ya fungu lako!
18Ilikuwa kitambo kidogo tu,
watu wako watakatifu walipokuwa wenye mafungu yao,
kisha wao waliotusonga walipaponda Patakatifu pako,
19tukawa watu, usiowatawala tangu kale,
wasiolitambikia Jina lako.