The chat will start when you send the first message.
1Nimetafutwa nao wasioniuliza;
nimeonwa nao wasioninyatia.
Nimewaambia watu wasiolitambikia Jina langu:
Mimi hapa! Mimi hapa!
2Mchana kutwa naliikunjua mikono yangu
kuwaita watu wabishi
washikao njia isiyo nzuri, wayafuatao mawazo yao.
3Ndio watu wanaonikasirisha pasipo kukoma,
ijapo niwatazame,
hutambika shambani, huvukiza kwenye matofali.
4Hukaa makaburini, hulala usiku penye mwiko,
hula nyama za nguruwe,
namo vyomboni mwao mna mchuzi wa kibudu.
5Husema: Jikalie kwako, usinifikie karibu!
kwani mimi ni mwiko kwako;
hawa ndio wanaotoa moshi puani mwangu,
ndio moto uwakao mchana kutwa.
6Tazameni! Yameandikwa mbele yangu;
sitanyamaza, ila nitayalipiza,
kweli nitayalipiza vifuani mwao.
7Manza zenu, mlizozikora,
pamoja nazo za baba zenu na mzilipe,
ndivyo, Bwana anavyosema;
maana wamevukiza milimani juu,
nako vilimani juu wamenibeua.
Nami kwanza nitawapimia malipo ya matendo yao,
wayachukue vifuani mwao.
8Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:
Kama watu wanavyosema fumbo la zabibu,
maji yao yakingali yamo,
kwamba: Usiziangamize! Kwani mbaraka imo,
ndivyo, nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu,
nisiwaangamize wote.
9Nitatokeza mzao kwake Yakobo,
nako kwake Yuda atakayekuwa mwenye milima yangu,
kusudi wao, niliowachagua, waitwae,
watumishi wangu wapate kukaa huko.
10Nako Saroni kutakuwa na malisho[#Yos. 7:26.]
ya makundi ya mbuzi na ya kondoo;
nalo bonde la Akori litakuwa pa kukalia ng'ombe
kwao walio ukoo wangu, kwa kuwa wamenitafuta.
11Lakini ninyi mliomwacha Bwana,
mkausahau mlima wangu mtakatifu,
mkamtandikia meza Mwenye kura,
naye Mwenye maaguo mkammiminia vinyweo
vilivyojaa mvinyo za tambiko,
12basi, ninyi nimewaagulia kuuawa kwa panga,[#Yes. 65:2; 66:4.]
nyote mpige magoti, mchinjwe,
kwa kuwa nilipowaita, hamkujibu,
niliposema, hamkusikia,
mkayafanya yaliyokuwa mabaya machoni pangu,
mkayachagua, ambayo nilikuwa sipendezwi nayo.
13Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema:
Kwa hiyo na mwone:
Watumwa wangu watakapokula,
ninyi mtaumwa na njaa;
watumwa wangu watakapokunywa,
ninyi mtaumwa na kiu;
watumwa wangu watakapofurahi,
ninyi mtaona soni.
14Watumwa wangu watakapopiga shangwe
kwa kuwa na mema mioyoni,
ndipo, ninyi mtakapolia kwa kuumia mioyoni,
tena mtapiga makelele kwa kupondeka rohoni.
15Nayo majina yenu mtayaachilia wao, niliowachagua,
watayatumia wakitaka kuapiza na kusema:
Bwana Mungu na akuue hivyo!
Lakini watumishi wangu atawaita kwa majina mengine.
16Atakayejiombea mema katika nchi
atajiombea kwake Mungu mwenye welekevu,
atakayeapa katika nchi
ataapa na kumtaja Mungu mwenye welekevu,
kwani masongano ya kwanza yatakuwa yamesahauliwa,
kwani yatakuwa yametoweka machoni pangu.
17*Tazameni! Mimi nitaumba
mbingu mpya na nchi mpya,
nazo za kwanza hazitakumbukwa tena,
hazitaingia mioyoni tena.
18Yafurahieni na kuyashangilia kale na kale,
nitakayoyaumba mimi!
Kwani na mwone, nikiumba Yerusalemu kuwa pa kushangilia
nao watu wake kuwa wenye furaha.
19Nami nitaushangilia Yerusalemu,
nitawafurahia walio ukoo wangu.
Mwake hamtasikilika tena sauti za vilio
wala sauti za maombolezo.*
20Hatakuwamo tena mnyonyaji wa siku chache,
wala mzee asiyezimaliza siku zake;
kwani watakaokufa wakingali vijana
watakuwa wa miaka mia,
nao watakaokufa wenye miaka mia
watawaziwa kuwa wakosaji walioapizwa.
21Watakaojenga nyumba wataikaa,
watakaopanda mizabibu wataila matunda yao.
22Hawatajenga, mwingine akae humo,
wala hawatapanda, mwingine ayale,
kwani siku za miti zilivyo,
ndivyo, siku zao walio ukoo wangu zitakavyokuwa,
nayo, wao niliowachagua watakayoyafanya kwa mikono yao,
watayatumia wenyewe.
23Hawatasumbuka bure,
wala hawatazaa watoto watakaogunduliwa na kifo,
kwani watakuwa mazao yaliyobarikiwa na Bwana,
wao wenyewe nao watakaotoka miilini mwao.
24*Itakuwa hivyo: Watakapokuwa hawajanililia bado,
mimi nitawaitikia;
watakapokuwa wanasema bado,
mimi nitakuwa nimesikia.
25Mbwa wa mwitu na mwana kondoo watalisha pamoja,
naye simba atakula majani kama ng'ombe,
naye nyoka mavumbi yatakuwa chakula chake.
Hawatafanya mabaya, wala hawataangamizana
katika mlima wangu mtakatifu wote.*
Ndivyo, Bwana anavosema.