Yesaya 7

Yesaya 7

Mahangaiko ya Yerusalemu.

1Siku za Ahazi, mwana wa Yotamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, ndipo, Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Isiraeli, walipokuja kupiga vita nao waliomo Yersalemu, lakini hawakuweza kuwashinda vitani.[#2 Fal. 15:37; 16:5.]

2Walio wa mlango wa Dawidi walipopashwa habari, ya kwamba vikosi vya Washami vimeingia katika nchi ya Efuraimu, vikapiga makambi, mioyo yao ikatikisika nayo mioyo ya watu wao, kama miti ya mwituni inavyotikiswa na upepo.

3Lakini Bwana akamwambia Yesaya: Toka wewe na mwanao Seari-Yasubu (Sao litarudi), uje kukutana na Ahazi, mwishoni pa mfereji wa maji ya ziwa la juu, kule barabarani panapokwenda kwenye shamba la Mfua nguo.

4Mwambie: Jiangalie, utulie, usiogope! Jipe moyo kwa ajili ya moshi wa hivyo vijinga viwili vilivyomo katika kuzimika, ijapo makali ya Resini na ya Washami na ya mwana wa Remalia yawakishe moto.[#Yes. 30:15.]

5Kweli Washami, Waefuraimu na mwana wa Remalia wamekulia njama mbaya ya kwamba:

6Na tupande kwenda Yuda, tuwastushe tukiwashambulia na kuwashinda, kisha tumweke mwana wa Tabeli kuwa mfalme kwao katikati!

7Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema: Hayatatimia! Hayatakuwa!

8Kwani kichwa cha Ushami ni Damasko, nacho kichwa cha Damasko ni Resini, tena miaka 65 itakapopita, Efuraimu atakuwa amepondwa kabisa, wasiwe ukoo tena.

9Kichwa cha Efuraimu ni Samaria, nacho kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Ikiwa mnakosa wa kumtegemea, kweli hamtategemezwa.[#2 Mambo 20:20.]

Kiagio cha Imanueli.

10Bwana akaendelea, akamwambia Ahazi kwamba:

11Jiombee kielekezo kwake Bwana Mungu wako! Omba kilicho mbali kuzimuni au kilicho mbali mbinguni!

12Ahazi akajibu: Sinacho nitakachokiomba, nisimjaribu Bwana.

13Ndipo, (Yesaya) aliposema: Sikilizeni, ninyi mlio wa mlango wa Dawidi! Je? Havijawatoshea kuwachokoza watu, mkimchokoza naye Mungu wangu?

14Kwa hiyo Bwana atawapa mwenyewe kielekezo, ni hiki: Tazama, mwanamwali atapata mimba, atazaa mtoto mwanamume, nalo jina lake atamwita Imanueli (Mungu yuko nasi).[#Yes. 8:8,10; 9:6; Mika 5:2; Mat. 1:23.]

15Atakula maziwa yenye mafuta na asali, mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema.[#Yes. 7:21-22.]

16Yule kijana atakapokuwa hajajua bado kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ile itakuwa imeachwa, sasa unawastukiaje wafalme wake wawili?[#Yes. 8:4.]

Mapatilizo yatakayokuja na Waasuri.

17Bwana atawaletea ninyi, wewe nao wa ukoo wako nao wa mlango wa baba yako, siku zisizokuja bado kuanzia siku ile, Waefuraimu walipojitenga kwao Wayuda; itakuwa hapo, mfalme wa Asuri atakapokuja.

18Siku ile mbung'o walioko mwishoni kwenye mito ya Misri nao nyuki walioko katika nchi ya Asuri Bwana atawapigia miluzi, waje.

19Watakuja kutua wote pamoja katika mabonde na makorongo, katika nyufa za magenge, hata katika maboma yote ya miti yenye miiba na malishoni po pote.

20Siku ile Bwana atamtumia mfalme wa Asuri kuwa kama wembe uliokopwa ng'ambo ya lile jito kubwa, awanyoe nywele za vichwa na za miguu, hata za ndevu zitamalizwa zote pia.

21Siku ileile mtu atafuga king'ombe kimoja na vibuzi viwili tu.

22Lakini kwa kupata maziwa mengi kwao hao atakula mafuta; wote watakaosalia katika nchi hiyo watakula mafuta na asali.

23Tena siku ile kila mahali penye mizabibu elfu iletayo sasa fedha elfu patakuwa penye mikunju na mibigili.

24Watu wakienda mahali kama hapo watashika mishale na pindi, kwani nchi nzima itakuwa mapori yenye mikunju na mibigili.

25Nako kwenye milima kote kunakolimwa sasa na majembe, watu hawatakwenda tena huko kwa kuiogopa mikunju na mibigili, watakutumia tu kwa kuchungia ng'ombe na kondoo na mbuzi, wachezeechezee kuko huko.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania