Yesaya 9

Yesaya 9

1Lakini huko kuliko na masongano kama hayo giza haitakaa kabisa. Siku za mbele nchi ya Zebuluni na nchi ya Nafutali alizitia soni, lakini huko nyuma atazipatia utukufu kwenye njia ya baharini na ng'ambo ya Yordani, Galilea ya wamizimu iliko.[#Mat. 4:12-16.]

Kuzaliwa kwake Masiya.

2Watu waliofanya mwendo gizani wameona mwanga mkuu, waliokaa penye kivuli kiuacho mwanga umemulika juu yao.[#Yes. 60:2; Luk. 1:79.]

3Wewe umekuza watu, wawe wengi, ukawapatia furaha kuu;

wanakufurahia, kama watu wanavyofurahi penye mavuno,

kama wanavyoshangilia wakigawanya mateka.

4Kwani umeivunja miti ya kuchukulia mizigo

pamoja na magongo yaliyowapiga migongoni,

nazo fimbo za wasimamizi,

kama ulivyofanya siku ya kuwapatiliza Wamidiani.

5Kwani mata yote, waliyoyashika kwenye mapigano,

nazo nguo zilizofuliwa katika damu

zitateketezwa kwa ukali wa moto.

6*Kwani tumezaliwa mtoto,

tumepewa mwana wa kiume,

nao ufalme uko begani pake.

Jina lake wanamwita:

Ajabu la mizungu, Mungu mwenye nguvu,

Baba wa kale na kale,

Mfalme wa utengemano.

7Ufalme wake ni mkubwa,

nao utengemano hauna mwisho

kwenye kiti cha Dawidi

na katika nchi zote, azitawalazo;

atazitengeneza na kuzishikiza

akiziamua kwa wongofu

kuanzia sasa na kuendelea vivyo hivyo kale na kale.

Bwana Mwenye vikosi atajihimiza kuyafanya hayo.*

Mapatilizo ya Waisiraeli.

8Bwana alituma neno la kuwatisha wa Yakobo,

linawapasa Waisiraeli nao.

9Watu wote watalitambua, kama Waefuraimu nao wakaao Samaria

wasemao kwa majivuno na kwa mawazo makuu ya mioyo yao kwamba:

10Majengo ya matofali yalipoanguka, tutapajenga kwa mawe ya kuchonga;

mitamba ilipokatwa, tutapanda miangati mahali pao.

11Kwa hiyo Bwana alipandisha kwao vikosi vya Resini, viwasonge,

nao adui zao akawachochea, wawajie:

12upande wa mbele wakaja Waasuri upande wa nyuma Wafilisti,

wakawala Waisiraeli na kuasama vinywa kabisa.

Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado,

nao mkono wake ungaliko umekunjuka.

13Nao walio ukoo wake hawakurudi kwake aliyewapiga,

Bwana Mwenye vikosi hawakumtafuta.

14Basi, siku moja Bwana alikata kwao Waisiraeli

kichwa na mkia, hata makuti na majani.

15Kichwa ndio wazee na wenye macheo,

mkia ndio wafumbuaji wafundishao mambo ya uwongo.

16Kwani viongozi wa ukoo huu walikuwa wapotevu,

nao walioongozwa nao wakaangamizwa.

17Kwa sababu hii Bwana hakupendezwa na vijana wao,

hakuwahurumia wala waliofiwa na wazazi wala wajane wao,

kwani hao wote humbeza Mungu kwa kufanya mabaya,

kila kinywa husema mapumbavu.

Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado,

nao mkono wake ungaliko umekunjuka.

18Kwani kule kumbeza Mungu kuliendelea kama moto uwakao.

unakula miiba na mibigili mikavu, unachoma vichaka vya msituni

na kupandisha mawingu mazima ya moshi.

19Nchi ikateketea kwa moto wa makali ya Bwana Mwenye vikosi,

watu wakawa kama chakula cha moto,

kwa hiyo hakuwako aliyemwonea ndugu yake uchungu.

20Wakajikatia kuumeni, lakini njaa haikuondoka;

wakala nako kushotoni, lakini hawakushiba;

kisha wakala kila mtu nyama ya mkono wake:

21Manase akamla Efuraimu, naye Efuraimu akamla Manase,

kisha wote wawili pamoja wakamgeukia Yuda.

Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado,

nao mkono wake ungaliko umekunjuka.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania