The chat will start when you send the first message.
1Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akawatia mikononi mwa Wafilisti miaka 40.
2Hapo palikuwa na mtu mmoja wa Sora wa ukoo wao Wadani, jina lake Manoa, mkewe huyu mtu alikuwa mgumba, hakuzaa.
3Huyu mwanamke akatokewa na malaika wa Bwana, akamwambia: Tazama, wewe u mgumba, hujazaa; lakini utapata mimba, uzae mtoto mwanamume.
4Sasa jiangalie, usinywe mvinyo wala kileo cho chote, wala usile chakula cho chote chenye mwiko.[#4 Mose 6:3; 3 Mose 11.]
5Kwani utajiona kuwa nwenye mimba, kisha utazaa mtoto mwanamume; nacho kinyoleo kisifike kichwani pake, kwani kijana huyo atakuwa ametengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, atakapozaliwa. Naye ndiye atakayeanza kuwaokoa Waisiraeli mikononi mwa Wafilisti.[#4 Mose 6:2-5; 1 Sam. 1:11.]
6Ndipo, yule mwanamke alipokwenda kumwambia mumewe kwamba: Mtu wa Mungu amekuja kwangu, nayo sura yake ilionekana kabisa kuwa kama sura ya malaika wa Mungu, naye alikuwa wa kutisha sana, kwa hiyo sikumwuliza, anakotoka, naye hakuniambia jina lake.
7Akaniambia: Utajiona kuwa mweye mimba, kisha utazaa mtoto mwanamume. Toka sasa usinywe mvinyo wala kileo cho chote, wala usile chakula cho chote chenye mwiko, kwani kijana huyo atakuwa ametengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, atakapozaliwa hata siku ya kufa kwake.
8Ndipo, Manoa alipomlalamikia Bwana kwamba: E Bwana, yule mtu wa Mungu, uliyemtuma, na aje tena kwetu, atufundishe vema, tutakayomfanyizia huyo kijana atakayezaliwa.
9Mungu akaisikia sauti ya Manoa, yule malaika wa Mungu akaja mara ya pili kwa yule mwanamke, alipokuwa anakaa shambani, lakini mumewe Manoa alikuwa hayuko kwake.
10Ndipo, yule mwanamke alipopiga mbio na kukimbia sana, akampasha mumewe hiyo habari akimwambia: Tazama, amenitokea yule mtu aliyekuja kwangu siku hiyo.
11Ndipo, Manoa alipoondoka, akamfuata mkewe, akafika kwa yule mtu, akamwuliza: Wewe ndiwe yule mtu aliyesema na huyu mwanamke? Akasema: Ni mimi.
12Manoa akauliza: Sasa neno lako litakapotimia, yatakayompasa huyo kijana ndio nini? Tena kazi yake itakuwa nini?
13Malaika wa Bwana akamwambia Manoa: Huyu mwanamke sharti ayaangalie yote, niliyomwambia, ayafanye!
14Yote yatokayo katika mzabibu asiyale, wala asinywe mvinyo wala kileo cho chote! Wala asile chakula cho chote chenye mwiko! Yote, niliyomwagiza, sharti ayaangalie.[#Amu. 13:4.]
15Kisha Manoa akamwambia malaika wa Bwana: Tunataka kukushika, tukuandalie mwana mbuzi.[#Amu. 6:18.]
16Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa: Ijapo unishike, sitakila chakula chako; lakini ukitaka kutoa ng'ombe ya tambiko, mtolee Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kwani Manoa hakujua, ya kuwa yeye ni malaika wa Bwana.
17Ndipo, Manoa alipomwuliza malaika wa Bwana: Jina lako nani, tupate kukuheshimu, neno lako litakapotimia?[#1 Mose 32:29.]
18Malaika wa Bwana akamwambia: Unaniuliziaje jina langu? nalo ni la kustaajabu.
19Ndipo, Manoa alipochukua mwana mbuzi na kilaji cha tambiko, akamtolea Bwana juu ya mwamba hivyo vipaji vya tambiko; naye akafanya jambo la kustaajabu, nao Manoa na mkewe wakawa wanalitazama:[#Amu. 6:21.]
20Ikawa hapo pa kutambikia, miali ya moto ilipopanda mbinguni, ndipo, malaika wa Bwana naye alipopaa katika miali ya moto uliokuwapo hapo pa kutambikia; nao Manoa na mkewe walipoviona, ndipo, walipoanguka kifudifudi chini.
21Kisha malaika wa Bwana hakumtokea tena Manoa wala mkewe; ndipo, Manoa alipojua, ya kuwa ndiye malaika wa Bwana.
22Naye Manoa aakamwambia mkewe: Hatuna budi kufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.[#2 Mose 33:20; Amu. 6:22-23.]
23Lakini mkewe akamwambia: Kama Mungu angependa kutuua, asingalipokea mikononi mwetu ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na kilaji cha tambiko, wala asingalituonyesha hayo yote, wala asingalitupasha habari hizo zote wakati huo.
24Yule mwanamke alipozaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samusoni; huyu kijana alipokua, Bwana akambariki.
25Roho ya Bwana ilipoanza kumhimiza, alikuwa kambini kwao Wadani katikati ya Sora na Estaoli.[#Amu. 6:34; 14:6,19; 15:14.]