Waamuzi 17

Waamuzi 17

Mika anatengeneza kinyago.

1Milimani kwa Efuraimu kulikuwa na mtu, jina lake Mika.[#3 Mose 5:1.]

2Huyu akamwambia mama yake: Hizo fedha 1100, ulizochukuliwa, umemwapizia mwenye kuzichukua namo masikioni mwangu, basi, hizo fedha mimi ninazo, nimezichukua mimi. Ndipo, mama yake aliposema: Ubarikiwe na Bwana, mwanangu!

3Akamrudishia mama yake hizo fedha 1100 naye mama yake akasema: Hizi fedha nimezitoa kabisa kuwa mali za Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, atengeneze kinyago cha kuchongwa, nacho kivikwe mabati ya fedha. Kwa hiyo sasa nazirudisha kwako.

4Alipomrudishia mama yake hizo fedha, huyu mama yake akachukua fedha 200, akampa mfua fedha, akazitumia kutengeneza kinyago cha kuchongwa kilichovikwa mabati ya fedha, kikawekwa nyumbani mwa Mika.[#Yes. 40:19.]

5Ndivyo, Mika alivyopata nyumba ya mungu, akatengeneza nacho kisibau cha mtambikaji kuwa kinyago cha nyumbani, kisha mmoja wao wanawe Mika akamjaza gao, akawa mtambikaji wake.[#Amu. 8:27.]

6Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, kwa hiyo kila mtu huyafanya yanyokayo machoni pake yeye.[#Amu. 18:1; 19:1; 21:25.]

7Kulikuwa na kijana wa Beti-Lehemu wa Yuda uliokuwa wa ukoo wa Yuda, naye alikuwa Mlawi, lakini alikuwa mgeni huko.[#Amu. 18:3.]

8Kisha huyu mtu akaondoka katika mji wa Beti-Lehemu wa Yuda kwenda kukaa ugenini mahali, atakapopaona; naye akafika milimani kwa Efuraimu nyumbani kwa Mika alipokuwa anajiendea tu.

9Mika akamwuliza: Umetoka wapi? Naye akamwambia: Mimi ni Mlawi wa Beti-Lehemu wa Yuda, nimekwenda kukaa ugenini mahali, nitakapopaona.

10Mika akamwambia: Kaa kwangu, uniwie baba na mtambikaji! Nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, hata nguo za kuvaa na vyakula vya kukutunza nitakupatia. Huyu Mlawi kwanza alitaka kwenda zake,

11halafu ikampendeza huyu Mlawi kukaa kwa huyu mtu, kisha huyu kijana akawa kwake kama mwanawe mmoja.

12Mika akamjaza gao huyu Mlawi, ndipo, huyu kijana alipokuwa mtambikiaji wake, akakaa nyumbani mwa Mika.

13Naye Mika akasema: Sasa najua, ya kuwa Bwana atanifanyizia mema, kwa kuwa huyu Mlawi ni mtambikaji wangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania