The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, wana wote wa Isiraeli walipotoka, mkutano wao ukamkusanyikia Bwana huko Misipa kuwa kama mtu mmoja toka Dani mpaka Beri-Seba, hata nchi ya Gileadi.[#Amu. 11:11; 1 Sam. 7:5.]
2Wote waliokuwa pembeni kwa watu wa mashina yote ya Waisiraeli wakatokea katika mkutano wao walio ukoo wa Mungu, watu 400000 waliokwenda kwa miguu waliojua kuchomoa panga.
3Nao wana wa Benyamini wakasikia, ya kuwa wana wa Isiraeli wamepanda kwenda Misipa. Ndipo, wana wa Isiraeli waliposema: Semeni, jinsi jambo hilo baya lilivyofanyika!
4Yule mtu wa Kilawi mwenye mwanamke aliyeuawa akajibu akisema: Naliingia Gibea wa Benyamini, mimi na suria yangu, tulale humo.[#Amu. 19:15.]
5Lakini wenyeji wa Gibea wakaniinukia; ulipokuwa usiku, wakaizunguka hiyo nyumba, nilimokuwa, wakataka kuniua mimi, naye suria yangu wakamkorofisha, mpaka akifa.
6Ndipo, nilipomshika suria yangu, nikamkata vipande, navyo nikavituma kufika mashambani po pote kwenye fungu la Waisiraeli, kwani walifanya mambo, Waisiraeli wanayoyawaza kuwa maovu na mapumbavu.
7Ninyi nyote wana wa Isiraeli mko hapa, sasa toeni maneno na mashauri yenu hapa!
8Ndipo, watu wote walipoinuka kama mtu mmoja kwamba: Hatutakwenda hata mmoja hemani kwake, wala hatutaondoka hata mmoja kwenda nyumbani kwake.
9Tutakalowafanyizia Wagibea hi hili: Tutawajia kwa kujipigia kura.
10Na tuchukue watu kumi wa kila mia ya mashina yote ya Waisiraeli, tena mia wa kila elfu na elfu wa kila elfu kumi, waende kuwachukulia watu pamba; watakaporudi, tutawafanyizia wao wa Gibea wa Benyamini yaupasayo huo upumbavu wote, waliowafanyia Waisiraeli.
11Ndivyo, watu wote wa Waisiraeli walivyokusanyikia huo mji wakiwa wameungwa kuwa kama mtu mmoja.
12Kisha mashina ya Waisiraeli wakatuma watu kwenda kwao mashina yote ya Benyamini kuwaambia: Hilo ni tendo baya gani lililofanyike kwenu?
13Sasa watoeni wale watu wasiofaa kitu waliomo Gibea, tuwaue, tuuondoe ubaya huo kwetu Waisiraeli! Lakini wana wa Benyamini wakakataa kuzisikia sauti za ndugu zao wana wa Isiraeli.
14Kisha wana wa Benyamini nao wakakusanyika Gibea na kutoka mijini mwao, waende vitani kupigana na wana wa Isiraeli.
15Wana wa Benyamini waliotoka mijini walipojikagua siku hiyo wlikuwa watu 26000 waliojua kuchomoa panga pasipo wenyeji wa Gibea waliokaguliwa kuwa watu wateule 700.
16Katika watu hawa wote walikuwa watu 700 waliochaguliwa kwa kuwa wenye shoto; kila mmoja wao alijua kutupa mawe kwa kombeo, asikose, ijapo uwe unywele tu, aliotaka kuupiga.
17Waisiraeli nao walipojikagua walikuwa watu 400000 waliojua kuchomoa panga pasipo Wabenyamini; hao wote walikuwa watu wa vita.
18Kisha Waisiraeli wakaondoka, wakapanda kwenda Beteli, wakamwuliza Mungu, wana wa Isiraeli wakisema: Ni wa nani wa kwetu, ndio waanze kupigana na wana wa Benyamini? Bwana akasema: Wayuda na waanze![#Amu. 1:1-2; 20:26-27; 21:2.]
19Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka asubuhi, wakapiga makambi yao kuelekea Gibea.
20Waisiraeli walipotoka kupigana wa Wabenyamini, Waisiraeli wakajipanga kupigana nao hapo Gibea.
21Wana wa Benyamini walipotoka Gibea, wakawafanyizia Waisiraeli vibaya siku hiyo na kulaza chini watu 22000.
22Lakini watu wa Waisiraeli wakajishupaza, wakajipanga tena kupigana papo hapo, walipojipanga siku ya kwanza.
23Lakini tena walikuwako wana wa Isiraeli waliopanda na kumlilia Bwana mchana kutwa, wakamwuliza Bwana kwamba: Tuendelee kujisogeza, tupigane na wana wa Benyamini walio ndugu zetu? Bwana akawaambia: Haya! Wapandieni!
24Wana wa Isiraeli walipowakaribia wana wa Benyamini siku ya pili,
25wana wa Benyamini wakatoka Gibea kukutana nao hiyo siku ya pili, wakawafanyizia wana wa Isiraeli vibaya na kulaza chini tena watu 18000, nao wote walikuwa watu waliojua kuchomoa panga.[#1 Mose 49:27.]
26Ndipo, wana wote wa Isiraeli nao watu wote walipopanda kwenda Beteli, wakamlilia Bwana huko pasipo kukoma, wakafunga siku hiyo mchana kutwa wakimtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani.[#Amu. 20:18.]
27Kisha wana wa Isiraeli wakamwuliza Bwana; nazo siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwako huko.
28Naye Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa Haroni, alitumikia huko siku hizo. Wakauliza: Tuendelee kutoka kupigana na wana wa Benyamini walio ndugu zetu, au tuache? Bwana akasema: Pandeni! Kwani kesho nitawatia mikononi mwenu.[#Yos. 22:13.]
29Kwa hiyo Waisiraeli wakaweka wenye kuvizia po pote pande zote za Gibea.
30Wana wa Isiraeli walipowapandia wana wa Benyamini hiyo siku ya tatu wakajipanga kuelekea Gibea kama jana na juzi.
31Wana wa Benyamini nao wakatoka kukutana nao, wakatengekana na mji wa kwao; walipoanza kupiga watu wengine kama jana na juzi na kuwaumiza hapo barabarani watu wa Waisiraeli 30, palikuwa hapo, barabara moja inapokwenda kupanda Beteli, ya pili inakwenda Gibea na kupita mashambani.
32Basi, wana wa Benyamini wakasema: Hawa wanapigwa na sisi kama hapo kwanza. Lakini wana wa Isiraeli walisema: Na tukimbie, tuwatenge na mji wa kwao tukiwapeleka barabarani.
33Kwa hiyo Waisiraeli wote wakaondoka mahali pao kwenda kujipanga tena Baali-Tamari; papo hapo Waisiraeli waliovizia wakatoka upesi hapo, walipokuwa, upande wa machweoni kwa jua wa huko Geba.
34Ndivyo, watu 10000 waliochaguliwa katika Waisiraeli wote walivyoujia Gibea toka ng'ambo ya huko; ndipo, mapigano yalipokuwa makali, nao walikuwa hawajajua bado, ya kuwa mambo mabaya yamewapata.
35Ndivyo, Bwana alivyowapiga Wabenyamini mbele ya Waisiraeli, nao wana wa Isiraeli wakawafanyizia Wabenyamini mabaya siku hiyo kwa kuangamiza watu 25100, nao hao wote walijua kuchomoa panga.
36Ndipo, wana wa Benyamini walipoona, ya kuwa wamekwisha kupigwa. Lakini Waisiraeli waliendelea kuwaachia Wabenyamini mahali pao, walipokuwa, kwani waliwaegemea wao waviziao, waliowaweka ng'ambo ya huko ya Gibea.
37Nao waviziao wakajihimiza, waushambulie mji wa Gibea; wao waviziao walipouteka wakawaua wote waliokuwamo mjini kwa ukali wa panga.
38Nao Waisiraeli walikuwa wameagana nao waviziao kielekezo, kwamba wapandishe moshi mwingi kama wingu mle mjini.
39Ikawa, Waisiraeli walipogeuka hapo penye mapigano, Wabenyamini walipoanza kuwapiga Waisiraeli na kuumiza kama watu 30 wakasema: Kweli wanapigwa mbele yetu kama katika mapigano ya kwanza.
40Mara kile kielekezo cha moto kikaanza kupanda juu, lile wingu la moshi; nao Wabenyamini walipogeuka nyuma yao, wakaona, mji wote mzima ulivyoteketea na kupandisha moshi mbinguni.
41Ndipo, Waisiraeli walipogeuka, nao Wabenyamini wakastushwa, kwani waliona, ya kuwa mabaya yamekwisha kuwapata.
42Ndipo, walipogeuka na kuwaonyesha Waisiraeli migongo yao, wakashika njia ya kwenda nyikani; lakini mapigano yakaandamana nao, nao waliotoka mijini wakawaangamiza katikati yao.
43Wakawazunguka Wabenyamini kwa kuwafukuza, walipopumzika, wakawakimbiza mpaka ng'ambo ya Gibea ya upande wa maawioni kwa jua.
44Wakauawa kwao Wabenyamini 18000, nao hao wote walikuwa watu wenye nguvu.
45Ndipo, walipogeuka kukimbilia nyikani kwenye mwamba wa Rimoni; lakini wale wakawaokoteza barabarani na kuua tena 5000, wakagandamana nao kwa kuwafuata hata Gidomu, huko nako wakaua wengine wao 2000.
46Ndivyo, hesabu ya Wabenyamini wote walioangushwa ilivyokuwa siku hiyo watu 25000 waliojua kuchomoa panga, nao hao wote walikuwa watu wenye nguvu.
47Lakini watu 600 waliogeuka wakakimbilia nyikani, wakakaa kwenye mwamba wa Rimoni miezi minne.[#Amu. 21:13.]
48Kisha Waisiraeli wakawarudia wana wa Benyamini, wakawapiga kwa ukali wa panga wote walioonekana, watu wa mijini pia hata nyama; nayo miji yote iliyopatikana wakaiteketeza kwa moto.