The chat will start when you send the first message.
1Waisiraeli walikuwa wameapa huko Misipa kwamba: Mtu wa kwetu asimpe mtu wa Benyamini mwanamke wa kike kuwa mkewe!
2Watu walipofike Beteli na kukaa huko mchana kutwa mbele ya Mungu, wakapaza sauti zao, wakalia kilio kikubwa
3na kusema: Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa sababu gani hili limefanyika kwa Waisiraeli, shina moja likiwa limepotea leo kwetu Waisiraeli?
4Ikawa kesho yake, watu walipoamka na mapema, wakajenga hapo pa kutambikia, kisha wakatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani.
5Ndipo, wana wa Isiraeli walipoulizana: Je? Katika mashina yote ya Waisiraeli wako wasiopanda kumtokea Bwana penye mkutano huu hapa Misipa? Kwani walikuwa wameapiana kiapo kikuu cha kwamba: Wao watakaokaa, wasipande kumtokea Bwana, hawana budi kuuawa.
6Tena wana wa Isiraeli wakawaonea uchungu ndugu zao Wabenyamini, wakasema: Leo hivi shina moja limekatwa kwetu Waisiraeli.
7Tufanyeje, wao waliosalia tuwapatie wanawake? Kwani sisi tumeapa na kumtaja Bwana, tusiwape wana wetu wa kike kuwa wake zao.
8Wakaulizana tena: Je? Miongoni mwa mashina ya Waisiraeli liko moja lisilopanda kumtokea Bwana hapa Misipa? Ndipo, ilipoonekana, ya kuwa watu wa Yabesi wa Gileadi hawakuja makambini kwenye mkutano huu.
9Watu walipojikagua wakaona: Kweli kwao wenyeji wa Yabesi wa Gileadi hakuja hata mmoja.
10Ndipo, watu wa mkutano walipochagua kwao walio wenye nguvu watu 12000, wakawatuma kwenda huko wakiwaagiza kwamba: Nendeni, mwapige wenyeji wa Yabesi wa Gileadi kwa ukali wa panga, hata wanawake na watoto!
11Tena hivi ndivyo mfanye: kila mume mtamtia mwiko wa kuwapo, vilevile kile mwanamke aliyekwisha kutambua mtu mume.
12Lakini kwao wenyeji wa Yabesi wa Gileadi wakaonekana wanawali 400 wasiotambua bado mtu mume kwa kulala naye; hao wakawapeleka katika makambi ya Silo ulioko katika nchi ya Kanaani.
13Kisha watu wote wa mkutano wakatuma wengine kwenda kwa wana wa Benyamini huko mwambani kwa Rimoni, wawaambie, ya kuwa vita vimekwisha.
14Ndipo, Wabenyamini waliporudi kwao wakati huo, nao wale wakawapa wale wanawake wa Yabesi wa Gileadi, walioacha kuwaua, lakini hawakuwatoshea.
15Nao watu wakawaonea Wabenyamini uchungu, kwa kuwa Bwana amewatenga Waisiraeli, patokee ufa.
16Wazee wa mkutano wakasema: Tufanyeje, tuwapatie wanawake nao wale waliosalia? Kwani kwa Wabenyamini wanawake walikuwa wameangamizwa.
17Wakasema: Fungu zima la nchi ni lao Wabenyamini waliopona, lisitoweke shina moja kwetu Waisiraeli.
18Lakini sisi hatuwezi kuwapa wana wetu wa kike kuwa wake zao, kwani sisi wana wa Isiraeli tumeapa kwamba: Aapizwe atakayempa Mbenyamini mwanamke!
19Kisha wakasema: Tazameni! Mwaka kwa mwaka iko sikukuu ya Bwana huko Silo ulioko karibu ya Beteli upande wa kaskazini, ni hapo penye barabara itokayo Beteli kwenda Sikemu upande wa maawioni kwa jua, tena ni karibu ya Lebona upande wa kusini.
20Basi, wakawaagiza wana wa Benyamini kwamba: Nendeni kuvizia mizabibuni!
21Hapo, mtakapoona, vijana wa kike wa Silo wakitoka kucheza hiyo michezo, ndipo, mtakapotoka mizabibuni, mjikamatie kila mtu mkewe kwa hao vijana wa Silo! Kisha mwende zenu katika nchi ya Benyamini.
22Kama baba zao au ndugu zao watakuja kutugombeza, tutawaambia: Waacheni kuwa matunzo, mnayotupa sisi, kwa kuwa vitani hatukumpatia kila mtu mkewe. Hivyo ninyi hamtawatoa kuwapa wale; kama mngewapa wenyewe, mngekora manza.
23Wana wa Benyamini wakavifanya hivyo, wakachukua wanawake na kuwanyang'anya kwa hesabu yao kwao waliocheza michezo yao, kisha wakaenda zao, wakarudi katika nchi iliyokuwa fungu lao, wakajenga miji, wakakaa humo.
24Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka huko, wakaenda kila mtu kwa shina lake na kwa ukoo wake. Ndivyo, walivyotoka huko kila mtu kwenda mahali pake palipokuwa fungu lake.
25Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, kwa hiyo kila mtu aliyafanya yanyokayo machoni pake yeye.