The chat will start when you send the first message.
1Lisikieni neno, Bwana alilowaambia ninyi wa mlango wa Isiraeli!
2Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msijifundishe kuzishika njia za wamizimu! Wala vielekezo vya mbinguni msivistuke, kwa kuwa wamizimu wanavistuka!
3Kwani miiko ya watu wa kimizimu ni kitu pasipo maana; kwani hukata mti wa mwituni, mikono ya fundi ikautengeneza kwa tezo.[#Yes. 44:10-20.]
4Kisha huupamba kwa fedha na kwa dhahabu, akautia nguvu kwa misumari na nyundo, usitukutike.
5Huwa kama nguzo tu iliyofunikizwa, hausemi; sharti uchukuliwe, kwani hauendi. Msiiogope! Kwani haifanyi kibaya, wala haina nguvu ya kutupatia mema.
6Hakuna afananaye na wewe, Bwana! Mkuu ndiwe wewe, nalo Jina lako ni kuu lenye nguvu.
7Yuko nani asiyepaswa na kukuogopa, uliye mfalme wa wamizimu? Inakupasa kweli, uogopwe; kwani miongoni mwa werevu wote wa kimizimu, hata katika nchi za kifalme zote hakuna afananaye na wewe.
8Wote pamoja ni wajinga na wapumbavu, mafundisho yao wasio kitu ndiyo mti mtupu!
9Mabati ya fedha yaliyopigwa nyundo huletwa toka Tarsisi, nayo ya dhahabu hutoka Ufazi, mafundi huyatengeneza, kisha mikono ya wafua dhahabu huyaseneza. Mavazi yao ni nguo za kifalme, nyeusi na nyekundu. Yote pia ni kazi za mafundi wazijuao kazi zao.
10Lakini Bwana ndiye Mungu kweli, yeye ni Mungu Mwenye uzima na mfalme wa kale na kale. Ukali wake huitetemesha nchi, wamizimu hawawezi kuyavumilia machafuko yake.
11Kwa hiyo mtawaambia: Miungu isiyoziumba mbingu na nchi sharti iangamie ulimwenguni chini ya mbingu.
(12-16: Yer. 51:15-19.)12Yeye ndiye aliyeifanya nchi kwa uwezo wake, akausimika ulimwengu kwa werevu wake wa kweli, akazitanda mbingu kwa utambuzi wake.
13Huvumisha maji mbinguni kwa ngurumo na kupandisha mawingu yatokayo mapeoni kwa nchi, kisha hupiga umeme kwenye mvua na kutoa upepo huko, alikouweka.[#Iy. 38:24-30; Sh. 135:7.]
14Ndipo, kila mtu anapopumbaa tu, asijue yatokako, hata kila mfua dhahabu hupatwa na soni kwa ajili ya kinyago chake, kwani alichokitengeneza ni uwongo tu, hata pumzi haimo.
15Havina maana, ni kazi ya kuchekwa tu; siku vitakapopatilizwa huangamia.
16Lakini aliye fungu lake Yakobo hafanani navyo, kwani yeye ndiye aliyeyatengeneza yote, naye Isiraeli ni ukoo uliopata fungu kwake; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake.[#Sh. 16:5; 5 Mose 32:9.]
17Yakusanye yaliyo yako katika nchi hii, wewe ukaaye bomani bado!
18Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona mara hii, nikiwatupa kwa nguvu wakaao katika nchi hii, nitawasonga, wapate kuona!
19A, nimevunjika! Pigo langu halitapona! Nasema mwenyewe: Haya ndiyo manyonge yangu, sharti niyavumilie.[#Sh. 77:11.]
20Hema langu limeharibika, nazo kamba zangu zote zimekatika; watoto wangu wametoka kwangu, hawako; hakuna atakayelipiga hema langu tena na kuziwamba nguo zangu za hema.
21Kwani wachungaji wangu wamepumbaa, hawakumtafuta Bwana, kwa hiyo hawakuerevuka, nalo kundi lao lote likatawanyika.
22Sikilizeni! Sauti zinasikilika zinazokuja, ni uvumi mkubwa sana upande wa kaskazini! Wanataka kuigeuza miji ya Yuda kuwa mapori tu na makao ya mbwa wa mwitu.
23Ninajua, Bwana, ya kuwa mtu siye anayeilinganya njia yake, wala mtu aendaye siye anayeushupaza mwenendo wake.[#Fano. 16:9; Mbiu. 9:11.]
24Nipige, Bwana, mapigo yapasayo! Usinipige kwa ukali wako, usiniangamize![#Yer. 46:28; Sh. 6:1; Hab. 1:12.]
25Makali yako yenye moto yamwage penye wamizimu wasiokujua, napo penye koo za watu wasiolitambikia Jina lako! Kwani wamemla Yakobo, kweli wamemla na kummaliza, nayo makao yake wameyageuza kuwa mapori tu.[#Sh. 79:6.]